Ads (728x90)

Golikipa wa timu ya Mbeya City David Burhan akichupa kuunyaka mpira ulioelekezwa golini kwake, katika mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara, kati ya timu hiyo na Prison zote za Mbeya, City ilishinda Bao 1-0
Baadhi ya mashabiki wa Timu ya Mbeya City wakimzonga shabiki mmoja anayedaiwa kuwa ni wa Prison aliyeenda kwenye Jukwaa la mashabiki wa City




Waamuzi wa mechi ya Mbeya City na Prison wakiwa na mananodha wa timu hizo  Hassan Mwasapili wa City na Lugano Mwangama wa Prison muda mfupi kabla ya kuanza kwa mechi kati ya timu hizo.


Kikosi cha Timu ya Mbeya City
Kikosi cha timu ya Prison


Kocha wa timu ya Mbeya City Juma Mwambusi akiwa na Mwenyekiti wa timu hiyo Mussa Mapunda( mwenye kanzu) pamoja na kocha msadizi wakipongezana kwa aushindi walioupata dhidi ya Prison





VIJANA wa Mbeya City leo wamewapigisha kwata wazee wao Prison zote za Jijini Mbeya kwa kuwafunga Bao 1-0 kwa bila katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Goli la Mbeya City liliingia katika dakika ya kwanza ya mchezo baada ya mchezaji wa Mbeya City  Paul Nonga kuupata mpira na kuambaa ambaa nao pembeni upande wa kushoto kisha kuwachanganya walinzi wa timu ya Prison na baadaye kupachika bao lililomuacha kipa wa Prison  Benno Kakolanya akichupa bila mafanikio.
Prison imeingia uwanjani huku ikiwa na maumivu ya bao 5-0 dhidi ya Yanga ya Dar es salaam katika mchezo uliochezwa Jumatano wiki iliyopita.
Bao hilo lilionesha kuwachanganya wachezaji wa Prison ambao walianza kufanya mashambulizi ya kushitukiza katika goli la Mbeya City ambapo hata hivyo washambuliaji wa Prison walionekana kushindwa kumalizia.
Prison ilipata nafasi kadhaa za kufunga lakini washambuliaji wake Fredy Chudu,Jimmy Shoji Omega Seme na Peter Michael walionekana wakilikaribia goli la Mbeya City lakini mipira yao aidha ilitoka nje ama ilipanguliwa na golikipa David Burhani.
Hadi mapumziko Mbeya City ilitoka kifua mbele kwa bao 1 dhidi ya 0 la Prison.
Kipindi cha pili kilianza kwa kila timu kufanya mabadiliko ambapo Mbeya City ilimtoa Peter Mapunda na nafasi yake kuchukuliwa na Jeremia John na Alex Sethi aliyeingia badala ya Saad Kipanga, ilhali Prison ilimtoa Jeremiah Juma na kumuingiza  Frank William lakini hata hivyo mabadiliko hayo hayakuweza kubadilisha hali ya mchezo huo.
Katika nyakati tofauti mwamuzi wa mchezo huo Saimon Mbelwa kutoka Pwani alilazimika kutoa kadi za njano kwa wachezaji ambapo alimzawadia kadi ya njano Christian Sembuli na Saad Kipanga wa Mbeya City kwa mchezo mbaya na mchezaji Fred Chudu wa Prison ambaye pia alimzawadia kadi ya njano kwa mchezo mbaya.
Mchezo huo ambao ulikuwa ukisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa mpira wa miguu mkoani Mbeya umetoa taswira nzima ya ligi ambapo hadi sasa Mbeya City inaendelea kushikilia nafasi tatu nyuma ya timu ya Yanga huku ligi Azam ikiendelea kushikilia usukani wa ligi hiyo.
Katika mchezo wa kwanza uliozikutanisha timu hizo Prison ililala mbele ya wadogo zake hao kwa kupachikwa bao 3-0.



Post a Comment