Endavyo nyuni mwituni, na kutambaa mitini,
Rizikiye mdomoni,daima huithamini,
Hujilia vya kondeni,vilivyosazwa na nyani,
Kilio chake kidege,kwani mwamsakiani?
Kakosani kwa manani,au vinyama mwilini,
Rizikiye i jaani,hula vile vya mwishoni,
Vilobaki barazani, na kuvisaza karoni,
Kilio chake kidege, kwani mwamsakiani?
Nguvu kwake abadani, kutumia hatamani,
Kidege yu maskini, hana maguvu mwilini,
Mkosa nyama mwilini, manati awindiwani,
Kilio chake kidege,, kwani mwamsakiani?
Apurukavyo mitini,huwa yumo mawindani,
Kusaka panzi mitini, na funza wa magomeni,
Bali yu mashakani,atafutwavyo porini,
Kilio chake kidege, kwani mwamsakiani?
Fasihi(Utu)
Insi kuukosa utu,ni dalili za mijitu,
Kwamba utu shuti kitu,
Haiwi katu haiwi,
Mtu wa roho ya kutu, Si mtu ela ni jitu,
Mwenda peku hana utu, bali mvaa viatu,
Shidaze kwazo ni butu,hasaidiwi katu.
FASIHI(CHAGUZI ama CHAKUZI?)
Kenda kumi karibia, hesabu inoishia,
Ya mwanzo mwisho timia ndiyo yetu asilia.
Chaguzi tumefanyia, nchi yetu Tanzania,
Kampeni kupitia,kwao wote wagombea.
Kwetu tuliuombea,uwe mwema kuishia,
Bali yaliyojiria,vigumu kuhadithia.
Kikwete kashika njia, Ikulu kuelekea.
Tuutazame kwa kina,mengi yaliyotokea,
Unguja pemba ghasia, dosari imetutia.
Askari kuvinjari, na mitutu shadidia,
Watu wakawa sanjari, hofu kuwaingilia.
Chaguzi tuhitajia, si vita kutarazia,
Vije iwe Valantia,watu kuwakamatia?
Mchakato hafifia, tume iloandalia,
Tume yapasa jutia,kudumaza demokrasia.
Hebu sasa tuanzia,kwa safari maridhia,
Upinzani kuingia, iwe kwa mwanzo hatua.
Vijiji imarishia, elimu ya uraia,
Vitongoji, Kata pia, wananchi kuijua.
Ndesanjo, Makene haya!! mwayaona Tanzania,
Wenzenu tuko pabaya, mchango twahitajia,
Kwa blogu kutumiya,fikira kuchanganua,
Chaguzi za Tanzania,ni chaguzi au chakuzi.
Mada hino iwe nguzo, CHAGUZI ama CHAKUZI,
Tutoe pasi mzozo,kwa busara kuienzi,
Tutafakari vikwazo, upinzani wapinzani wamaizi,
Wajue pasi mabezo, nini maana uchaguzi.
Wakatabahu,
Ustaadh, Rashid Mkwinda(ngominenga)
(Malenga wa Kilwa)
Nimerudia kusoma shairi hili nikiwa nimetulia. Kazi murua. Valangati la nini kama si kudumaza demokrasia? Huenda matokeo ya uchafuzi huu ndio kile mwanablogu Nkya (http://pambazuko.blogspot.com) anaita "mkumbokrasia."
ReplyDeleteShukurani na heshima natoa kwanza awali
ReplyDeleteRisala unazotuma zimejaa maadili
Mizani unaipima na vina vya kustahili
Kwa uchache wa lawama ‘metupatia suali
Hali ninajizuwia kwa baiti kujadili
Uchaguzi Tanzania na wetu mustakabali
Shauku imeningia kuchambua yetu hali
Fasihi ‘menivutia kudondosha moja mbili
Hilino jambo ghasia tashtiti na mushkeli
Visiwani lilotokea kuchagua serikali
Siyo mwanzo kutokea yalianza tangu mbali
Na mbele naangalia siioni afadhali
Naomba tega sikio keti utulie tuli
Hayano mataradhio nayotaka kujadili
Ni kwa mifano iliyo wala isiyo batili
Na mfano nikupao ni wa safari ya meli
Kung’oa naga jahazi ni jambo lilo takili
Lenye kutaka henezi na uwingi wa akili
Wasokua na ujuzi wa kuiongoza meli
Hao huwa wachakuzi sukani hawastahili
Kwa pepo za kaskazi safari yenda sahali
Kamwe kusi haiwezi kutufikisha pahali
Wa nahodha uamuzi kutuepusha na zali
Kodo kodoa maozi utaziona fiili
Dhaifu kwenye mizizi ndoa isiyo kamili
Ilokosa uongozi shupavu bila dhalili
Kuliokoa jahazi twepuke dhoruba kali
Wasafiri yetu kazi hii dira kubadili
Abiria tuamkeni kuikataa kauli
Ya washika usukani kwamba shwari ‘tawasili
Tutue kimya chomboni na dhiki tuikubali
Ati tutunze amanijapo twajua ni ghali
Iwe yetu mazowea masihara kuhimili
Haki zetu maraia tuzitupilie mbali
Nasema demokrasia pekee si mhimili
Lengo lisiwe chagua wabunge na maliwali
Wasotaka kuamua kwa haki na maadili
Twataka wanotambua wawe kama mawakili
Wenye nia kutatua tatizo kwenye asili
Wasushe tanga mashua huu mwendo tubadili
Hapo tutanusurika kusikwa hai tungali
Tutaondokwa mashaka ya demokrasi batili
Na kupata muwafaka ukidhio pande mbili
Zogo tutaliepuka heri irejee meli
Haki yetu kuchagua zingatia neno hili
La pili ni kuzuwia ghasia na ukatili
Tusichoke tangazia walo karibu na mbali
Thanaashara natua baiti kumi na mbili
Nambiza, ukiweza bandika shairi hili pale Mwandani. Safi sana.
ReplyDeletekama kuna tunu inayopendeza ni ushairi,mkwinda,mwandani,Makene wanavaa haswa vazi la tunu hii na kupendeza, kwa kazi zenu nawasifu,lakini ni changamoto kwa Mimi, Ndesanjo nkya pamoja na Msaki na taarifa kwa michuzi kupaza sauti zetu sasa kwa kuimba kwa ghani za ufasihi na ustadi katika ulingo huu, au mnasemaje?
ReplyDeleteNyembo, Usinikumbushe mzee Athman Khalfani, saa tisa mchana jua kali, njaa kali ukitoka shule ugali umechelewa kupikwa - unamsikia mghanii Khalfani kwa sauti ya puani redioni, teknolojia hiyo ya sauti ipo
ReplyDeletetunashukurua sana mwanafasihi mkwinda kwa kazi kubwa ya kuneemeka unayofanya. wewe kweli ni kizuu cha kale....ndesanjo unaikumbuka fasihi hiyo?
ReplyDeleteninaposoma mashairi yako nasikia kama kaupepo kamepiga ubongoni na napata amani ya ajabu.
ni changamoto kwetu kama nyembo alivyosema ili sahfari zijazo tusiandike mashairi yanayoporomoka kama yale maji pale kiraracha kwa mrema. - alinishauri kaka ndesanjo nilipotia mguu kwenye fani hii!! lakini si haba alinisifia sifia kidogo!!
kaza buti mkuu mkwinda hasa kwa mashairi. bado kidogo tu itakuwa ni fani ya kulipa sana, hasa yale yaliyotungwa kimtindo wa kabla mazingira ya fasihi hayajachafuka. pia ninyi ni muhimu sana kwa ajili ya kuwapa vesi vijana wa bongo flav.
hivi ninauliza. kuna uwezo wa kuyaweka mashairi yooooooote ya RTD na uhuru/mzalendo kitabuni? ni urithi wa taifa.
cheers,
mark
Ijapo neema, neemeka,
ReplyDeleteIjapo hasara hasirika,
Ijapo faraja farijika,
Nafarijika.
Kwa kuungwa na watajika katika blogu,changamoto hino ya kifasihi, yaburudi wangu mtima.
Mwandani mja wa neema,
Fasihiyo watumia vyema, Munganishaji mkuu Ndesanjo
Sifazo hazina pima.
Nyembo, Msaki, Msangi Rama,
Na Jeff, Michuzi wanadhima,
Kwa fasihi kujituma.
Makene Mwalimu mwema,
Fasihi isije zama.
Wakatabahu
nadhani safari ijayo kina kaka ndesanjo muandae mashindano ya kuandika mashairi (kwa nchi nzima ) halafu pia muandae mashindano ya kuyaimba ili tujikumbushe hicho ambacho bwana mwandani amekisema hivi punde! mie kuandika siwezi lakini yule bwana athmani nilikuwa naweza mwigiza kuliko! kwani yule bwana yuko bado hai? halafu baada ya kipindi chake kama ni ijumaa si ndio kilikuwa kinafuatiwa na cha sheick hemed bin hemed bin jumaa? du lakini yule mzee alikuwa mwisho, maana nakumbuka masuala ya *** ndio ilikuwa kama muvu ya X! halafu wala hakuwa akiona noma ..yaani kusema kimafumbo! duh lakini ilikuwa raha. ebu mkwinda tunga shairi linalomuhusu mtoto aliyerudi shule anasubiri ugali halafu ngoma (malenga wetu) inapigwa mchana wa jua kali. changanya changanya na yale mazingira ya kutumwa chumvi na kumsaidia mama kuosha vyombo! au la mtoto yuko chini ya mti (mkenge) anapata siesta baada ya michezo mingi ya kutwa usisahau wakati huo huo ukucha umetoka sababu ya kutunguia ndochi kwenye jabali....si unajua tena mambo ya peku peku?
ReplyDeletecheers
Msaki amenikumbusha enzi zile za kukimbilia shuleni ilhali nimetoka nyumbani nimekunywa uji kikombe kimoja na kuunga chumvi, miguu imejaa magaga kwa kutembea umbali mrefu bila kiatu huku wale wadudu maarufu kwa jina la funza wakiwa wametafuna vidole kutokana na kukosa viatu.
ReplyDeleteSiku hiyo nikichelewa shule nawakuta wenzangu wako darasani wameanza kusoma mmwalimua ananitandika mboko za matakoni viboko vinainga barabara kwa kukosa kuvaa chupi ndani, wakati huo huo akina dada wakicheka kwa kupigwa viboko lahaula!!! ilikuwa ni enzi ya aina yake zama zile.
Nikirudi nyumbani mamja ananituma kuchukua makopa ya muhogo kutwanga ili yaweze kuwa unga kwa ajili ya ugali wakati huo njaa yauma kwelikweli ndipo hapo burudani pekee katika moyo inapokuwa ghani ya mashairi ya Athmani Khalfani ndani ya Redio Tanzania.
Hiyo hali inanikumbusha kule ambako tulikuwa katika zama za ujima zama za kulima pamoja na kuvuna pamoja na mazao kugawana ilhali korosho zetu tukizipeleka katika vyama vya ushirika, Msaki unajua unaweza kunisababisha nikaanza kulia kwa yale yaliyopita enzi zile hebu kwa leo niachie hapa tutaendelea siku nyingine
Big up Msaki kwa kunikumbusha enzi zile.
Mkwinda! zama chungu (ujima) lakini si zilikuwa tamu zaidi ya sasa (mwendokasi ya maisha)?
ReplyDelete