Ukitumika vyema, itaongoka jamii,
Ikiwa bora kusema,yako huyazingatii,
Insi watajalalama,Kwa kuikosa shafii,
Mdomo wata kunena,yaso yako kunenea.
Kinenea neno jema, wanenewao tatii,
Watakwenzi maulama', walopata digirii,
Uta'wa mja wa wema, uloshinda makarii,
Mdomo wata kunena, yaso yako kunenea.
Nenolo litatuama,makarii watatwalii,
Litaja dumu dawama, japo utakuwa zii,
Umeacha chumo jema, kaburi hulijutii,
Mdomo wata kunena, yaso yako kunenea.
Nena neno lenye dhima,lijesomwa kwa bidii,
Walinene watu wema, watawao ja sufii,
Lije kuongowa umma,urithi wa manabii,
Mdomo wata kunena,yaso yako kunenea.
Enyi mpendao sema chungeni kauli hii,
Midomo yenu gharama,iwapo hufikirii,
Msijepata lawama,ikiwa hamchungii,
Mdomo wata kunena,yaso yako kunenea.
Mdomo nacha kusema, kauli siifichii,
Hapa bora kutuama,niwacheni wenye fii,
Bali waadhi ni mwema,ijapo hamtulii,
Mdomo wata kunena,yaso yako kunenea.
Wakatabahu.
Post a Comment
Post a Comment