La Dodoma azimio, Makene limetulia,
Lafaa kuwa zingatio,Bloguni kutumia,
Tena liwe karipio, watakao vurugia,
Azimio la Dodoma,liwe la wanaBlogu.
Kwa uhuru twandikia, wengi wanatusomea,
Maadili kupindia, hako wa kutukemea,
Uhuru tunotumia, sote twaushere’kea,
Azimio la Dodoma,liwe la wanaBlogu.
Sheria kuiwekea, madhara kutukingia,
Uhuru uliopea,majina twajiandikia,
Msaliti kitokea,Blogu tutakimbia,
Azimio la Dodoma, liwe la wanaBlogu.
Wazo lenu wa Dodoma,mkono naliungia,
Kikao chenu ni dhima,ni mfano kuigia,
Fikira hazitokoma,wanaBlogu kuchangia,
Azimio la Dodoma, liwe la wanaBlogu.
Miruko,Kazonta,Mtangoo,jema mlofikiria,
Msaki, Msangi katika mtandao, wote wanalichangia,
Nyembo,Ndesanjo,na wengineo,hima wanaliwania,
Azimio la Dodoma, liwe la wanaBlogu.
Adabu kuzingatia, katika kuandikia,
Maadili kufatia, ya uandishi Blogia,
Wasomao jifunzia,kazi zilizotulia,
Azimio la Dodoma, liwe la wanaBlogu.
Wakatabahu kuungia,beti saba natulia,
Hima sote kubalia,la Dodoma liwe njia,
Kwamba si nadharia, kwa vitendo fuatilia,
Azimio la Dodoma,liwe la wanaBlogu.
Ndimi Mkwinda Rashid, kalamu naiachia,
Kamwe sina ukaidi,kwa hili kuliungia,
Nitafanya tashdidi, wengi kuwashawishia,
Azimio la Dodoma, Liwe la wanaBlogu.
Mkwinda mashairi yako huwa yanarejesha haraka ile tamu ya ushairi niliyowahi kuwa nayo shuleni. Wengine wanaweza kuwa hawakioni haraka. Vina na mizani yako siyo ya kulazimisha. Yachuruzika yenyewe kwa raha tele ya kusoma ama kughani. Rambirambi zikufikie.
ReplyDeleteKwa nini nisibaini, huu mwana mwenye heshima?
ReplyDeleteKwa huu wako ugani, kukiunda chetu chama
Sina lakuongezani, mkuki umeshachoma
Azimio na lidumu, mabaradhuli uani