Milio ya Bundi nyakati za usiku, ndege aina ya Kware wakiashiria  kumalizika kwa kipindi cha kiangazi sanjari na sauti za Njiwa nyakati za  asubuhi ilikuwa ni ishara tosha kwamba maeneo hayo ni ya vijijini  ambayo sifa ya watu waishio maeneo hayo ni wale wanaokosa fursa ya  kupata huduma muhimu za kijamii.
Moja ya huduma muhimu wazikosazo wananchi wa maeneo hayo ambao  asilimia themanini ni wakulima na baadhi yao wakiwa ni wafugaji ni  kupata fursa ya kuutumia mhimili usio rasmi wa dola (Mhimili wa Nne)  Vyombo vya Habari, hali iliyoonesha kama vile wanahabari hao waliamua  kukutana na wanavijiji hao kwa nia ya kufanya Tambiko la Kihabari.
Tambiko la Kihabari linatafsirika kutokana na ukweli kuwa wanahabari  hao wa Mbeya wameamua kufungua ukurasa mpya wa kukutana na wadau wasio  nasauti katika maeneo ya vijijini.
Asilimia kubwa ya wanahabari na vyombo vyao vimekuwa vikiripoti  matukio ya mjini huku wananchi hao wa vijijini wakikosa fursa hiyo  adhimu ambayo kimsingi ni haki yao ya Kikatiba ya Uhuru wa kutoa Habari  na kupata Habari.
Ujio wa wanahabari katika maeneo ya vijijini ulileta shauku wananchi  hao kukutana na washika kalamu hao ili angalau waweze kutoa madukuduku  yao ambayo kwa takribani miaka hamsini tangu Uhuru hawajawahi kupata  fursa hiyo.
Wanahabari walipata fursa ya kusafiri mwendo wa takribani kilomita 150  hadi katika kijiji cha Kalangali kijiji am ambacho kimenakshiwa na  mazingira ya asili na mandhari yanayosadifiu uumbaji wa asili uliotunza  mazingira halisi chini ya Taasisi ya Mazingira wilayani Chunya (KAEA). 
Takribani wanahabari 40 ambao waliongozwa na Mwenyekiti wa  Klabu ya Waandishi wa Habari wa mkoa wa Mbeya Bw. Christopher Nyenyembe  walifanya ziara katika kijiji hicho na kuzoea makazi ya maeneo hayo kwa  muda wa siku tatu ambazo walizitumia katika kuzoea hali halisi ya  maeneo hayo na kuishi kama wanakijiji ikiwa ni pamoja na kubadilishana  mawazo na wenyeji wa maeneo hayo kwa kuvaa uhusika halisi wa kijijini.
Wanahabari ambao kwa asilimia kubwa hutafuta habari za mijini pekee  walipata fursa ya kukutana na mtu mmoja mmoja wa maeneo hayo na kubaini  dosari zenye changamoto kwa wanahabari kutokana na kukosekana kwa habari  nyingi za vijijini katika vyombo vya habari nchini.Aidha fursa hii ya wanahabari iliwapa morari ya kuona umuhimu wa kipekee  kutembelea mara kwa mara maeneo ya vijijini bila kusubiri ziara za  viongozi wa kiserikali na kudandia magari ya viongozi hao ili kufika  huko.
Tathmini ya mtu mmoja mmoja kutoka maeneo ya vijijini  yameakisi sura halisi ya maisha yao huku nchi yetu ikikaribia  kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru ifikapo Disemba 9 mwaka huu, ambapo suala  la miundo mbinu, maji safi na salama, elimu, afya, masoko ya bidhaa  wanazozalisha  na pembejeo za kilimo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment