WAKATI Serikali ikiendelea kupambana ili madaktari waache mgomo 
wao, hali bado ni tete katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) 
kutokana na hospitali hiyo kugoma kupokea wagonjwa wapya.
MWANAFASIHI lilishuhudia jana wagonjwa hasa wajawazito wakikataliwa 
kwa madai kuwa hakuna madaktari, hivyo warejee katika hospitali zilizo 
karibu na maeneo yao.
Hali ni mbaya zaidi katika wodi ya watoto ambao wamezaliwa chini ya
 muda wao 'njiti' wakihitaji kuwa chini ya uangalizi wa madaktari.
Kutokana na hali hiyo, watoto watano waliokuwa kwenye uangalizi 
maalumu wanadaiwa kupoteza maisha juzi na idadi hiyo itaongezeka endapo 
mgomo huo utaendelea.
Ili kuonesha mgomo huo ulivyo tete, juzi saa 6 usiku Waziri wa Afya
 na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda, Naibu Waziri Lucy Nkya, Katibu 
Mkuu wa wizara hiyo, Blandina Nyoni, Mganga Mkuu wa Serikali, Deo 
Mtasiwa na viongozi wengine walifika hospitali hapo kuona huduma 
zinavyoendelea.
Imeelzewa kuwa baada ya kuingia wodi ya wazazi walipokelewa na 
kelele za wajawazito hao ambao walilalamikia kudorora kwa matibabu 
kutokana na makali ya mgomo huo.
Akizungumza na MWANAFASIHI kwa sharti la kutotajwa jina lake, mmoja 
wa wauguzi wa wodi hiyo alisema hali bado si nzuri na kwamba ni Dk. 
Kamugisha pekee ndiye anayefanya kazi baada ya wengine kugoma.
"Dk. Kamugisha Mungu aendelee kumsaidia kwani ndiye pekee 
anayefanya kazi akisaidiana na sisi wauguzi ambao tumeambiwa tutoe 
huduma kwa wagonjwa waliopo wodini pasipo kuwapokea wa nje,'' alisema 
muuguzi huyo.
Alisema hali inatisha kwenye wodi ya watoto njiti kwani ni kama 
wametelekezwa bila msaada na si wauguzi wote wanaoweza kuwaangalia 
kutokana na hali zao zilivyo.
Mjamzito, Rehema Ali mkazi wa Kiwalani, alisema jana alikuwa 
afanyiwe upasuaji wa uzazi katika hospitali hiyo na daktari wake 
aliyemtaja kwa jina la Kapona, lakini hakupokelewa kutokana na mgomo 
unaoendelea.
"Dokta wangu Kapona aliniambia siwezi kufanyiwa upasuaji hivyo 
aliniambia niende Hospitali ya Mwananyamala ambapo nitafanyiwa upasuaji 
huo leo,'' alisema.
Katika hatua nyingine, Mwandishi Wetu aliyekuwepo eneo la mapokezi 
katika wodi hiyo ya wazazi jana asubuhi alishuhudia mjamzito Ashura 
Kazeba akikataliwa kupokelewa hospitalini hapo kwa madai kwamba hakuna 
huduma.
Mjamzito huyo alinusuriwa na Dk. Kamugisha baada ya kuambiwa 
alizuiliwa ambapo alifika mapokezi na kuanza kuwafokea wauguzi 
waliokuwepo na kuamuru wampeleke wodini.
"Nani amemzuia mama huyu asipokelewe, mnamrudisha nyumbani kwa 
agizo la nani? Mwandikisheni na kisha mpelekeni wodini tusiharibiane 
kazi,'' alisema Dk. Kamgisha kwa kufoka.
Meneja Uhusiano wa hospitali hiyo, Aminiel Aligaesha akizungumza na
 waandishi wa habari jana alikiri madaktari bingwa wa hospitali hiyo 
kuazimia kusitisha huduma za matibabu mpaka hapo Serikali itakapotoa 
tamko rasmi kuhusu muafaka wa suala hilo.
Alisema wagonjwa waliopo wodini wataendelea kuangaliwa na madaktari
 wakuu wa idara na madaktari wachache waliojitolea na kuwa madaktari wa 
Jeshi la Wananchi wa Tanzania wataendelea kuwaona wagonjwa kwa dharura.
Akifafanua juu ya kufukuzwa kwa wagonjwa, alisema kwamba hakuna 
mgonjwa aliyefukuzwa kama ilivyodaiwa na vyombo vya habari kwani juzi 
takwimu zinaonesha wagonjwa 811 walipokelewa hospitalini hapo.
Alisema huduma za uuguzi zinaendelea kama kawaida na wanatoa 
shukurani kwa wauguzi wanaoendelea na kazi katika kipindi hiki cha 
mgomo.
Katika muendelezo wa matukio ya mgomo huo wa madaktari imeelezwa 
vifo katika Hospitali ya Temeke vimeongezea hasa kwa wagonjwa 
waliowapeleka hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kukataliwa.
"Tunasikitika kuona wagonjwa tunaowawapeleka Muhimbili kwa matibabu
 wakikataliwa kupokelewa na badala yake tunarudishiwa na matokeo yake 
karibu wote waliorudishwa wamepoteza maisha,'' alidai mmoja wa wauguzi 
wa hospitali hiyo.
Kutokana na hali hiyo, kwa masaa kadhaa madaktari na wauguzi 
walisimamisha kutoa huduma kwa muda ili kujua hatima ya suala hilo na 
kufanya wagonjwa kurejea nyumbani.
Mwandishi wetu aliyefika hospitalini hapo alishuhudia madaktari na 
wauguzi wa hospitali hiyo wakiwa kwenye mkutano wa dharura katika moja 
ya chumba katika ofisi ya Mganga Mkuu.
Hata hivyo, baada ya kikao hicho walionekana kurudi katika maeneo 
yao ya kazi na kuendelea kutoa huduma. Jitihada za kuonana  na Mganga 
Mkuu wa hospitali hiyo, Amani Malima ili kuzungumzia suala hilo 
hazikuzaa matunda baada ya mwandishi wetu kumpigia simu na kujibiwa kuwa
 aende ofisini na alipofika Katibu Muhtasi wake alisema yupo na wageni.
STORI NA PICHA KWA HISANI YA DOTTO MWAIBALE 
 
Post a Comment