Na Stephano Mango, Songea
KATIBU wa Halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi Itikadi na Uenezi Nape Nnauye ameitaka Serikali kurudisha Kiwanda cha kusindika tumbaku cha Songea Tobacco Processing Industry(SanTop) ambacho kimepelekwa mkoani Morogoro na kuwaacha wakazi wa Ruvuma wakilalamika kutokana na msaada mkubwa uliokuwepo wakati kiwanda hicho kikifanya kazi Songea
... Wito huo ameutoa jana wakati akizungumza na mamia ya wananchi,wanachama na viongozi wa Chama cha Mapinduzi (Ccm) waliokusanyika kumpokea Kata ya Shule ya Tanga Wilayani Songea mkoani Ruvuma ambako yupo katika ziara ya siku mbili
Nnauye alisema kuwa kiwanda hicho kilijengwa miaka mingi iliyopita na kiliwezesha kutoa ajira za muda mfupi na mrefu kwa wakazi wa mkoani humo na kusababisha kuwepo kwa mzunguko mkubwa wa fedha na kukua kwa uchumi wa Ruvuma na wananchi wake.
Alisema kuwa wakulima wa zao hilo kwa muda wote huo walikuwa wakijivunia kuwepo kwa kiwanda hicho, hali iliyowafanya kuongeza juhudi katika uzalishaji wa tumbaku na kujipatia maisha bora kutokana na shughuli yao ya kilimo
“ Inasikitisha kusikia wajanja wachache kwa kushirikiana na wawekezaji, bila aibu waliamua kukihamisha kiwanda hicho na kupeleka Morogoro, ambapo hakuna hata mche mmoja wa tumbaku unaozalishwa huko,” alisema Nnauye
Alisema tangu kiwanda hicho kilipohamishwa kutoka mjini humo, uchumi wa mkoa na watu wake umeshuka na kusababisha mateso makali kwa wananchi kutokana na kunyang’anywa fursa yao ya kujipatia kipato na kupelekea majengo ya kiwanda hicho kuwa mahame ambayo popo wanajihifadhi na wadudu wengine katika umasikini
Aliwataka viongozi wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Ruvuma kushirikiana kikamilifu na Serikali ili kuweza kukirudisha haraka iwezekanavyo kiwanda hicho ambacho kilikuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa mkoa wa Ruvuma
Katibu huyo ameanza ziara ya siku mbili mkoani Ruvuma ambako atafanya mikutano ya hadhara na wananchi, vikao vya ndani,kufungua mashina na matawi ya chama hicho pamoja na kuweka mawe ya msingi miradi mbalimbali ya chama.
Post a Comment
Post a Comment