Ads (728x90)






WIKI iliyopita rafiki yangu kutoka Fiji aliniletea jarida moja lenye picha za kihistoria ya kumbukumbu ya ubaguzi kule Marekani enzi za ubaguzi wa rangi na ukandamizaji wa mtu mweusi. Jarida lile linasononesha na kuhuzunisha ukitazama picha za waafrika waliokuwa wakiitwa ‘Negro’, walifanya kazi kucha kutwa kwenye mashamba ya mabepari wa kizungu huku wakilipwa ujira mdogo!
Kwenye kampeni za CCM, zama ambazo Amani Karume alikuwa nyota wa CCM Zanzibar.
Sehemu kama Mississippi, Alabama na nyingine waafrika walinyanyasika sana, lakini si haba juhudi za akina Malcom X, Dk. Martin Luther King Jr, Mchungaji Leon Sullivan na wapigania haki wengine, leo Marekani ni taifa lenye umoja na mshikamano na ndio taifa lenye kupigiwa mfano wa kilele cha demokrasia.

Kisa maarufu kilichomtokea Mchungaji Leon Sullivan, Mmarekani mwenye asili ya Afrika ambaye anajulikana kwa msimamo wake wa kuchukia ubaguzi wa rangi siku moja alienda kunywa soda kwenye hoteli moja kule Marekani, alipoingia akanyimwa kiti kwa vile yeye alikuwa mtu mweusi.

Kitendo hicho kilimfanya kuuchukia ubaguzi wa rangi na ubaguzi wa aina yoyote.

Tukiwa tunakaribia maadhimisho ya miaka 49 ya Mapinduzi Zanzibar na hapo baadae miaka 49 ya Muungano ni muhimu kukumbusha dhamira za Afro Shiraz Party (ASP), juu ya msimamo wake katika kupiga vita ubaguzi.

1927, safari yetu leo itaanzia Mzizima jina la asili la Dar es Salaam ya sasa. Huko waafrika wa mjini Dar es Salaam walianzisha jumuiya yao iliyoitwa ‘African Association’ kwa ajili ya kupigania haki na maslahi yao ya kijamii.

Waafrika wa Zanzibar nao walianzisha African Association yao hiyo ilikuwa 1934, pengine ni kutokana na ushawishi wa ndugu zao wa Dar es Salaam. Nao Waafrika wa Zanzibar wakawashawishi Waafrika wa Dodoma ambao nao walianzisha ya kwao.





Rais wa kwanza wa Zanzibar na baba ya rais wa sita, Abeid Karume.


Upepo wa mabadiliko ulikuwa ukivuma katika sehemu nyingi za dunia na hasa Afrika wakitaka kuwa huru kutoka kwa wakoloni. Hali hiyo ilifanya 1954 kuzaliwa Tanganyika African National Union (TANU), chama kilichoanzishwa Tanganyika kutokana na Tanganyika African Association, kwa ajili ya kudai uhuru kwa upande wa Tanganyika.

Zanzibar nako 1957 ilianzishwa Afro Shirazi Party (ASP), kutokana na kuungana kwa African Association na Shirazi Association iliyokuwa imeundwa 1938. Kuundwa kwa ASP kulishuhudiwa na Rais wa TANU, Marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere pale Mtaa wa Mwembe Kisonge. ASP ilizaliwa katika mazingira yaliyokwisha andaliwa kisiasa na African Association (AA) na Shirazi Association (SA), vyama ambavyo vilikuwa nusu vya siasa na nusu vya kijamii kupigania maslahi ya watumishi wa Kiafrika kazini.

Hata baada ya kuundwa kwake, ASP na TANU katika ilani zao zilisisitiza suala zima la ushirikiano, umoja na mshikamano katika dunia ambapo ASP toka enzi za mapambano ya kudai uhuru ilikuwa na vipengele vya kutaka umoja wa Afrika.
Inastaajabisha leo kuna watu Zanzibar wamejivika joho la U Afro Shirazi kupinga maridhiano, kubeza Serikali ya Umoja wa Kitaifa na wengine kumfuja, kumkejeli na hata kumtusi mama yake mzazi, Rais Mstaafu wa Zanzibar Awamu ya Sita Dk. Amani Abeid Karum, kwa maoni yake aliyoyatoa mbele ya mkutano mkuu wa CCM Dodoma na hatua yake kuasisi maridhiano na umoja Zanzibar.



Mansour Yusuf Himid, mmoja wa waungaji mkono wa umoja wa Wazanzibari akiwa ndani ya CCM.


Sijui ni ASP ipi inayoelezwa kuwa haikutaka umoja, mshikamano, kwani wakati wa harakari za kutafuta uhuru, ASP pamoja na vyama vingine vya ukombozi Afrika vilishiriki kikamilifu katika majukwaa yote yaliyowaunganisha Waafrika wa nchi mbali mbali katika kudai uhuru kwa lengo la kuja kuziunganisha nchi hizo baada ya uhuru. Kwa mfano, TANU na ASP zilikuwa wanachama wa PAFMECA na baadae PAFMECSA, vyombo ambavyo viliviweka pamoja vyama vilivyokuwa vikidai uhuru kutoka nchi mbali mbali za eneo la Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika.

Mwasisi wa Taifa la Zanzibar, Abeid Amani Karume na Jamal Ramadhan Nasib ambao wote sasa ni marehemu waliwahi kushiriki mikutano mara kadhaa katika nchi za Ghana,Misri na Ethiopia, je tuwahukumu kwa suala hilo? Watu wenye busara kamwe tutawakumbuka kwa mchango wao kutaka umoja na mshikamano.

Katibu Mkuu wa kwanza wa ASP, Sheikh Thabiti Kombo Jecha katika kitabu cha “Masimulizi ya Sheikh Thabit Kombo Jecha,kilichoandikwa na Minael-Hosanna Mdundo(DUP 1999) Sheikh Thabit Kombo ananukuliwa kusema kwamba “Wazo la Muungano ni wazo la Afro-Shirazi tokea mwanzo, katika Manifesto yetu tulisema kuwa tukipata Uhuru azma ya ASP ni kuona kuwa Afrika yote inakuwa moja yenye nguvu”.


Waasisi wa Maridhiano ya Wazanzibari mwaka 2009, Amani Karume na Maalim Seif Sharif Hamad.

Akiamini katika Umoja wa usawa,Sheikh Thabit Kombo na waasisi wengine wa ASP waliingia katika kuiunganisha Zanzibar na Tanganyika kutaka nguvu si za kupigana bali za kiuchumi na ndio maana suala la uchumi halikuwa katika orodha ya mambo ya Muungano. Mzee Karume na Sheikh Thabit Kombo walisimama katika nguzo ya nia njema,tunapoadhimisha miaka 49 ya Mapinduzi tuna kila sababu ya kuwaenzi na kudumisha misingi yao.

Je wale wanaodai kuwa CCM imesalitiwa kwa kuwepo GNU iliyozaliwa kutokana na maridhiano ya kisiasa Zanzibar wana lipi la kusema na kujinasib ikiwa CCM ni zao la vyama vya ASP na TANU? Hivyo basi wafahamu kuwa sikio siku zote halizidi kichwa, Wahafidhina ni ASP ipi mnayoitetea? Hii iliyoasisiwa na Mzee Karume, Sheikh Thabit Kombo Jecha au nyingine maana wazee wetu hawa walichukia sana ubaguzi.

Wapo baadhi ya watu wamekuwa wakiwasingizia baadhi ya viongozi waliotangulia mbele ya haki. Wengi utawasikia kama angekuwepo Mzee Karume, Seif Bakari, Mzee Thabit Kombo, au Said Bavui , wasingekubali mseto au maridhiano haya!


Hii si kweli,ni kujaribu kuwalisha maneno maiti badala ya kuwarehemu. Mzee Karume alikuwa Waziri wa Afya katika Serikali ya Mseto iliyoundwa na Vyama vya ZNP na ASP kabla ya Mapinduzi, sasa Karume anayesikingiziwa uzushi huo ni yupi huyu wa sasa au wa zamani?


Karume mkubwa na mdogo wote ni waumini wa umoja na maridhiano na ndio maana Baraza la kwanza la Mapinduzi lilijumuisha watu wenye nasaba tofauti.

Itakumbukwa pia kuwa mara tu baada ya Mapinduzi mwaka 1964,Mzee Karume huyo huyo kama ilivyo kwa Sullivan na Mwalimu Nyerere naye alichukia sana ubaguzi na ndio maana aliongoza kampeni ya ndoa za mchanganyiko wa rangi na makabila mbalimbali Zanzibar.


Mzee Karume hakulazimisha watu kuoana bali aliwataka wazazi wawape watoto wao uhuru wa kuoa na kuolewa na wawapendao. Waarabu hawakutaka mabinti wao waolewe na Waafrika ilhali wanawapenda na kinyume chake baadhi ya Waafrika nao walikataa watoto wao kuoa Waarabu.


Shafi Adam Shafi ameeleza katika kitabu chake cha Vuta N’kuvute suala la ndoa za aina hiyo,” akapeleka posa kwa Gulam. Gulam alipojidai kumtilia nakshi Kermali akibwata na kufoka kuikataa posa ya golo,Kermali akamwambia “ho! Mbona wewe unaye golo umemficha Vikokotoni”


Mwenyewe Karume akaanza kuoa Waarabu akifuatiwa na Wajumbe wengine wa Baraza la Mapinduzi(MBM) ambao walioa wake wa makabila mbalimbali , Ramadhan Haji Faki, Brigedia Yussuf Himid, Khamis Darwesh, Ibrahim Amani, Thabit Kombo Jecha na wengine ambao vizazi vyao ndio leo wanachama wa CCM na wengine ni viongozi.

Je unambagua mtoto au mjukuu wa Mzee Thabit Kombo Jecha kwa misingi ipi? kwasababu Mahmoud Thabit Kombo mama yake ni Mzanzibari mwenye asili ya kihindi au Mahfoud Ali Mahfoudh ambaye mamake Bi Naila Jidawi ana asili ya kiarabu ? ambao leo ni makamanda wa mstari wa mbele ndani ya Jeshi kubwa la CCM katika kutafuta ushindi kwenye uchaguzi.


Mzee Karume alishawishi watu kuwa wamoja na kwa kweli baadhi ya wazazi wakashawishika na kuanza kuunga mkono dhana ya ndoa za mchanganyiko ambapo faida yake baada ya miaka takriban 49 sasa tunaiona matunda ya ndoa hizo wengine ni viongozi na raia wa kawaida wasiojigamba kwa rangi na nasaba zao, bali kwa uzalendo wa Uzanzibari.

Ndoa hizo hazikuwa za kulazimishana kama inavyodaiwa na baadhi ya watu wapinga umoja na maelewano. Katika kuthibitisha hilo soma kitabu cha Vuta ni nkuvute katika ukurasa wa 275, Shafi Adam Shafi ameeleza kwa kina suala hilo akihusisha ndoa ya Bukheti Madoriani na Yasmin.


Kwa kuwa ndani ya CCM hivi sasa wapo watoto, wajukuu na vitukuu vya waasisi wa ASP na hata CCM yenyewe,hoja ya kupinga GNU,kumkejeli Rais mstaafu Karume inapata nguvu wapi ikiwa Gulam na Kermali walizika tofauti zao na kushirikiana katika shughuli ya arusi? ASP iliungwa mkono na Waarabu,Wahidi na watu wengine. TANU nayo ilikuwa na watu kama hao kina Alnoor Cassum,Derek Bryson, Amir Habib Jamal, Habib Punja na wengineo.

Kuna baya lipi lililofanywa na CCM kushirikiana katika kuendesha nchi na Chama cha CUF ambacho cha Wazalendo wenzao? Mawaziri wote ni Wazanzibari ambao naamini wanafanya kazi kwa mujibu wa katiba na sheria kuwatumikia wananchi wenzao.

Wakati Tanga la jahazi la wataka mabadiliko katika mfumo wa muundo wa Muungano limeshiba upepo wa Kaskazi hivi sasa na kusi hapo baadae, komamanga imelala upande mmoja inakata maji kama papa,huku wanamageuzi wa kweli wkaiwa wamesimama tezi wakiangalia Mji wa uhasama,chuki na ubaguzi ukitoweka ambapo katika upeo wa macho yao nuru ya matumaini kutapa mabadiliko katika Muungano ikianza kujichomoza,tuna kila sababu ya kutetea hoja ya mabadiliko.

Jahazi la wapinga mabadiliko linakumbwa na misukosuko ya bahari,upepo wa kaskazi unavuma sijui kama watapona maana tanga lao bovu,foromali chakavu huku hali ya bahari ikichafuka sijui kama papa wenye njaa wanaoranda randa katika upwa wa kisiwa chao kama watawaacha.


Hakuna ubishi kwamba katika dunia ya sasa mambo yote hadharani,Msondo Ngoma wameimba katika wimbo wao wa mambo hadharani, tumeshuhudia mchakato wa utoaji maoni mambo yakiwa hadharani, wanaotaka mabadiliko ya muundo wa Muungano wanasema na wale wanaopinga nao wanaeleza hoja zao,mwisho wa siku tutakumbana kwenye kura ya maoni.

Rais Jakaya Kikwete aliwahi kusema kuwa Wazanzibari ni wamoja hakuna haja ya kugombana. Sasa wewe unaeshabikia siasa za chuki na uhasama unapingana na Mwenyekiti wako wa CCM na Halmashauri Kuu yako ya Taifa iliyoamua kule Butiama kuhusu Serikali ya umoja wa Kitaifa? Bila shaka katika maneno hayo kuna mafundisho makubwa yanapatikana kwa muumin wa kweli wa kiislamu ambapo naamini genge la Wahafidhina asilimia kubwa kama si yote ni Waislamu. Mwenyezi Mungu anasema na hawakumbuki ila wenye akili.


Marekani, ilikuwa ndoto kwa Mmarekani mwenye asili ya Afrika kutawala katika nchi hiyo, lakini tumeshuhudia mwiko huo ukivunjwa Januari 20, 2009, pale Barack Obama alipoapishwa kuwa rais wa 44 wa Marekani na hivi karibuni ameshinda tena Uchaguzi. Hivi leo dhambi kuu ya baadhi ya wanasiasa hasa Zanzibar wanaopenda kuwashawishi watu katika njia za ukabila na ujimbo kama utambuzi mkuu katika kuungwa mkono ili kulinda maslahi yao ya kuweko kwenye nafasi bila kujali athari za baadae wanafaa kusikilizwa au kupuuzwa?


Ni muhimu pia kuuliza Viongozi wa CCM na hata wale waliomo ndani ya SMZ kuwa ushupavu wa kutetea uamuzi uliofanywa na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM Zanzibar kuhusu kumalizika kwa mpasuko wa kisiasa Zanzibar.


Bila shaka Amani Karume ni Kiongozi shupavu ambaye hakuchukua ubinafsi kama dira na mwelekeo wake katika maisha yake ya siasa. Kwa wale wataalam wa Tasnia ya Manajimenti wanaelewa vyema msamiati wa “The Courage of Leadership.” Ushupavu wa Uongozi. Tuwe wepesi kutambua maslahi yetu katika mabadiliko hayo, na tuwe wepesi kubuni mikakati ya kutetea maslahi hayo. Tuwe shupavu kama Chama kuwaiga rafiki zetu Wachina. Uchumi wa dunia ya leo ni uchumi wa soko. Ni kujidanganya kufikiri tunaweza kuukwepa.”


Bila shaka Karume ni aina ya Kiongozi katika jamii ambaye hakutaka kubeba mizigo yenye harufu mbaya na kuifanya ni mwelekeo mbadala katika siasa na maendeleo kwani katikaduania ya utandawazi inayioendelea kwa kasi majadiliano na kufikia maafikiano ndio nguzo na silaha madhubuti.

Pengine tuwaulize Viongozi waliokuwamo katika GNU kutoka CCM wana ushupavu unaohitajika au walitaka uongozi kwa maslahi binafsi, lakini je CCM kinao ushupavu wa uongoz iunaohitajika katika mazingira ya sasa ya Serikali ya GNU? Mbona hatuwasikii kuelezea umuhimu wa maridhiano katika siasa za ushindani wa vyama vingi?

SOURCE;Zanzibar Daima

Post a Comment

Post a Comment