Ads (728x90)

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kimesema kuwa kitalazimisha maandamano nchi nzima iwapo Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Naibu wake hawatakubali kujiuzulu kwa kusababisha anguko la elimu nchini.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na maelfu ya wakazi wa Jiji la Mbeya kwenye uzinduzi wa Baraza la Uongozi kanda ya Nyanda za Juu, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama hicho Freeman Mbowe, amesema kuwa,watayalazimisha maandamano hayo hata kama jeshi la polisi na vyombo vingine vya usalama vitayazuia.

Bw. Mbowe amesema kuwa anajua wazi Jeshi la Polisi litatumia kuyadhibiti maandamano hayo na kueleza kuwa CHADEMA haitawaogopa polisi wala mabomu ya machozi na kwamba wamejiandaa kwa lolote litakalotokea.

Aidha Bw. Mbowe amesema kuwa katika kuthibitisha kuwa wanachokisema wamedhamiria aliwahamasisha wananchi kuchangia fedha kwa ajili ya kukabiliana na mabomu ya machozi na majeruhi watakaotokea baada ya kupigwa na polisi ambapo jumla ya sh. milioni 3.2 zilichangwa na wananchi kusaidia wahanga wa maandamano ya siku hiyo ambayo alisema ataitangaza rasmi.

Amewataka wananchi wa mikoa ya Iringa, Njombe, Ruvuma na Mbeya kujitokeza kwa wingi mkoani Mbeya ambako ndiko kwenye makao makuu ya kanda hiyo kufanya maandamano ambapo pia aliwataka wamachinga, wanafunzi askari polisi na watu wengine kujitokeza barabarani kwa ajili ya kuwashinikiza Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dkt. Shukuru Kawambwa na Naibu wake Philipo Mulugo kuachia ngazi.

Amesema kiwaaango cha elimu nchini kimeshuka kwa asilimia 94 na kusababisha idadi kubwa ya watoto kubaki mitaani hali ambayo amesema imesababishwa na serikali kutojali watoto wa masikini ambao kipato chao ni kidogo.

Katika Maandamano hayo ambayo yaliongozwa na Mbowe yaliyoanzia katika eneo la Uhasibu Mafiat hadi katika Uwanja wa Ruanda Nzovwe,Mbowe aitembea kwa mwendo wa kilomita tano ambapo makundi ya waendesha bodaboda, baiskeli na watembea kwa miguu walijitokeza kwa wingi kuunga mkono maandamano hayo.


















Post a Comment

Post a Comment