WANAHABARI WAKIWA WAMEJIBANZA KATIKA KITUO CHA POLISI MJINI TUNDUMA |
ASKARI WA KIKOSI CHA MBWA WAKIJIANDAA KUKABILIANA NA LOLOTE KATIKA VURUGU HIZO |
ASKARI POLISI MARA BAADA YA KUWATAWANYA WATU WANAOSADIKIWA KUWA NI WAUMINI WA DINI YA KIKRISTO WALIOSHINIKIZA KUFUNGWA KWA MABUCHA YA WAISLAMU |
KUNDI la watu wanaosadikiwa kuwa ni waumini wa dini ya Kikristo jana wamedaiwa kuvamia bucha za nyama zinazomilikiwa na waislamu na kulazimishwa kufungwa kwa bucha hizo kutokana na madai ya kuwekwa kwa uwiano sawa wa uchinjaji baina ya waislamu na wakristo.
Kundi hilo la waumini walikuwa wakipita katika
barabara kadhaa za mji mdogo wa Tunduma kushinikiza kufunguliwa kwa mabucha ya
wakristo na kuibua taharuki kwa baadhi
ya wafanyabiashara wa maeneo hayo ambao walilazimika kufunga maduka baada ya
askari kuanza kurusha mabomu kutawanya watu hao.
Vurugu hizo ambazo ziliambatana
na vijana hao kuziba barabara na kuchoma matairi zilianza kutawanya kwa mabomu
ya machozi ilhali kundi hilo
la watu nalo lilianza kuwarushia mawe askari waliokuwemo kwenye magari ya doria
na kusababisha askari mmoja aliyekuwa akiendesha gari la polisi kujeruhiwa.
Kutokana na hali hiyo mpaka
wa Tanzania na Zambia
ulilazimika kufungwa ili kupisha vurugu hizo ambazo zimedumu kuanzia saa 4;00
asubuhi mpaka majira ya saa 11 jioni.
Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa polisi
mkoa wa Mbeya Diwani Athumani ambaye alifika kwenye eneo la tukio alisema kuwa
vurugu hizo zinaonekana kuwa na ushawishi wa kisiasa kutokana na ukweli kuwa
hazikupaswa kufikia hatua hiyo.
Kamanda Athumani amesema kuwa
jeshi la polisi linawatafuta Mchungaji wa kanisa la KKKT la mjini Tunduma
aliyefahamika kwa jina la Gidioni Mwamafupa na Diwani wa Kata ya Tunduma Frank
Mwakajoka kutokana na kudaiwa kuhusika kwa namna moja ama nyingine juu ya
kutokea kwa tukio hilo.
Amesema kuwa mbali na watu
hao jeshi la polisi linawashikilia zaidi ya watu 40 ambao wanaendelea kusakwa
kutokana na kusababisha vurugu hizo ambazo zimesababisha kukwamishwa kwa
shughuli mbalimbali za kibiashara mjini humo.
Awali inadaiwa kuwa baadhi ya
waumini wa dini ya Kikristo walipeleka barua kwenye uongozi wa serikali ya mji
huo wakitaka wapewe ridhaa ya kuchinja kama
vile ambavyo waumini wa dini ya kiislamu wanafanya.
Katika madai yao ambayo yalimfikia mkuu wa wilaya hiyo
Abihudi Saideya walihitaji kupata kibali cha kuchinja ambapo hata hivyo kwa
mujibu wa Mkuu wa wilaya yalilikuwa yakifanyiwa kazi ngazi ya Taifa.
Amesema kuwa hata hivyo
waumini hao walianza kuchinja kabla hawajapewa kibali cha serikali na
kusababisha kuwepo kwa mgongano wa kimaslahi baina ya waumini wa dini hizo.
Post a Comment
Post a Comment