Mtoto Anna Mwakyoma anayedaiwa kutelekezwa na baba yake kilabu cha pombe za Kienyeji. |
-Adaiwa kuelekea kwenye machimbo ya dhahabu
MSICHANA
Anna Mwakyoma(13) mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya Msingi Majengo
iliyopo wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa ametelekezwa katika kilabu cha Pombe za kienyeji
na baba yake mzazi aliyemtaja kwa jina la Fred Mwakyoma.
Tukio hilo la unyanyasaji limetokea huku kukiwa na mkakati wa kupinga unyanyasaji na ukatili wa kijinsia na taasisi mbalimbali kikiwemo Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA limetokea mwishoni mwa wiki baada ya mwandishi wa habari hizi aliyekuwa akifuatilia vitendo vya ukatili wa kijinsia kufika wilayani humo.
Akisimulia mkasa
huo katika ofisi ya Ofisa Ustawi wa Jamii wilayani hapa Binti huyo ambaye
alikuwa ameambatana na Ofisa wa polisi kutoka Kitengo cha Dawati la jinsia Majuto
Khalfani, alisema kuwa alifika wilayani humo na baba yake wakitokea Sumbawanga
kupitia mkoani Mbeya.
Alisema baba
yake ambaye ametengana na mama yake mzazi aliyemtaja kwa jina la Asha
Mwanandeje mkazi wa Majengo mjini Sumbawanga alimfuata na kuondoka naye kwa
madai kuwa alitaka kumkutanisha na kaka yake ambaye wameachana miaka mingi.
‘’Baba
alinifuata Sumbawanga, akasema nije naye Mbeya nionane na kaka John, sikuonana
na kaka tukapanda gari kuja huku Chunya, tangu aliponiacha hapa kilabuni sijamuona
tena,’’alisimulia kwa masikitiko msichana huyo ambaye kwa wakati huo alikuwa chini
ya uangalizi wa Dawati la Jinsia la Polisi wilayani Chunya.
Aliendelea
kusimulia kuwa awali alikutana na baba yake akiwa darasa la kwanza walipokuwa
wakiishi mjini Tunduma lakini baadaye ulitokea ugomvi ambao ulisababisha baba
na mama yake watengane na yeye kwenda kuishi na mama yake mjini Sumbawanga.
Alisema kuwa
kwa kipindi chote ambacho alikuwa akiishi na mama yake mjini Sumbawanga
hajawahi kukutana na baba yake hadi alipofika hivi karibuni na kumtaka waondoke
pamoja kuelekea Mbeya.
‘’Alipokuja mama
alikuwa yupo kwenye biashara zake za kuuza mpunga alinichukua alfajiri
tukapanda Basi hadi Mbeya, hata mama sikumuaga,’’alisema msichana huyo.
Akizungumza
mazingira ya kupatikana kwa mtoto huyo Ofisa Ustawi wa Jamii wilaya ya Chunya
Bi. Macrina Mayage alisema kuwa kwa mujibu wa maelezo ya msichana huyo baba
yake alimtorosha kutoka kwa mama yake ambapo walipofika Mbeya waliondoka naye hadi
Chunya na kumtelekeza bila msaada wowote na yeye kutokomea kusikojulikana.
Alisema hadi
sasa msichana huyo amehifadhiwa katika kituo cha Polisi wilayani Chunya kitengo
cha Dawati la Jinsia wakijaribu kutafuta mawasiliano katika shule aliyokuwa
akisoma mjini Sumbawanga.
Naye Ofisa
wa polisi kutoka Dawati la Jinsia wilayani humo Bi. Majuto Khalfani alisema
kuwa msichana huyo alikabidhiwa kwao kutoka kwa mama mmoja ambaye aliletwa na
vijana katika eneo lake la biashara za pombe za kienyeji usiku wa manane.
Kwa mujibu
wa Bi. Khalfani ni kwamba, msichana huyo aliachwa stendi na baba yake kuanzia
mchana hadi saa sita za usiku ndipo alipoingia katika eneo la pombe za kienyeji
ambako alikutana na mama huyo ambaye alimhifadhi nyumbani kwake hadi asubuhi
alipompeleka kituo cha Polisi.
''Hatujui alipo baba yake hadi sasa,hatujapata taarifa za ajali au kifo, tumeenda hospitali ya wilaya hatujaona majeruhi au mtu yoyote aliyeripotiwa kufariki dunia, inawezekana ameelekea kwenye machimbo ya dhahabu na kumtelekeza mwanaye, kitendo alichokifanya hakifai katika jamii,''alisema Bi. Khalfani.
Chama Cha
Waandishi wa Habari wanawake TAMWA kimekuwa mstari wa mbele kupinga ukatili
unaofanywa dhidi ya wanawake na watoto na kulazimika kuwatuma baadhi ya
waandishi wa habari kufuatilia na hatimaye kuibua matukio ya aina hii maeneo
mbalimbali nchini.
Kwa mujibu
wa Mkurugenzi Mkuu wa TAMWA Bi. Valerie Msoka ni kwamba matukio mengi ya
ukatili wa kijinsia yanayofanyika maeneo ya pembezoni hayaripotiwi katika
vyombo vya habari hivyo kutoa fursa kuendelea kwa matukio hayo bila kuchukuliwa
hatua za kisheria.
Post a Comment
Post a Comment