Ads (728x90)


Rais Jakaya Kikwete anakabiliwa na mzigo mzito wa Mawaziri Mzigo wanaotakiwa kuwajibika kutokana na Ukiukwaji wa Haki za binadamu katika Operesheni Tokomeza Ujangili.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye anaelezwa kuwa naye alipaswa kuwajibika kutokana na kushindwa kuwasimamia vyema mawaziri wa chini yake ikiwa ni pamoja na utendaji usiotukuka.
Khamis Juma Suedi Kagasheki, aliamua kujiuzulu nafasi yake ya Waziri wa Mali Asili na Utalii baada ya kujionea kwa macho yake picha za udhalilishaji, mauaji na unyama uliotekelezwa wakati wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
Shamsi Vuai Nahodha alitenguliwa nafasi yake ya Uwaziri, Mwenyewe adai ni ''Ajali Kazini''
Emanuel Nchimbi pamoja na kulazimishwa kutenguliwa nafasi yake ya Uwaziri wa Mambo ya Ndani adai, ''Nimeonewa sihusiki na kashfa hiyo, watekelezaji walikuwa ni Jeshi''


Mathayo David Mathayo, pamoja na kulazimishwa kujiuzulu alidai kuwa, ameonewa na anamtupia Mungu, Tume haikumhoji''
James Daud Lembeli(57) Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge iliyoundwa kuchunguza Operesheni Tokomeza,adai kamati ilifanyakazi katika mazingira magumu kwa kiu njaa na jua na walifanya kazi kwa uadilifu na siri kubwa.

Na Rashid Mkwinda
WAKATI wa kikao cha 14 cha  Bunge la  Jamhuri wa Muungano kikiendelea fikra na hisia za wananchi zilielekezwa katika kadhia nzima ya unyama ulioendeshwa wakati wa 'Operesheni Tokomeza Ujangili' ambao ulilazimika kuwa wazi kutokana na mazingira ya udhalilishaji na ukiukwaji wa haki za binadamu ambayo hayakupaswa kuvumiliwa katika jamii yoyote.

Madhila na madhara yaliyotokea katika Operesheni hiyo yametafsiri aina ya watendaji waliopo kwenye nyadhifa mbalimbali katika serikali yetu ambao aidha wamekuwa na nia ya kuyanakshi maovu yanayotokea katika jamii na kuyaweka katika taswira inayopendeza na kuwavutia wananchi, ama wameamua kutumia nafasi zao za uongozi kama mwamvuli wa kuendeleza maovu.

Aina hii ya utendaji wa viongozi unapaka matope sifa nzuri ya baadhi ya watendaji wazuri waliopo serikalini na hivyo kuibua tafsiri ya uongozi mzima kushindwa kuwajibika ipasavyo kutokana na wachache wanaoharibu.

Operesheni iliyoendeshwa imesababaisha vifo, ubakaji,uharibifu wa mali, makazi ya wananchi na mifugo na hata kusababisha kero na madhila makubwa kwa raia ambao kwa mtazamo wamejenga chuki na dhana mbaya kwa serikali yao wakitafakari mustakabali wa maisha yao na hatima yao kuwepo chini ya uongozi unaoumiza na kunyanyasa raia wake kwa kiwango hiki.

Kadhia hii ya aina yake kutokea katika nchi yetu imeharibu sifa ya Uongozi wa Juu wa Serikali na hata kuonesha ni namna gani viongozi wanaoteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali wanakosa vigezo vinavyostahili  na hata kulitia doa Taifa letu.

Mara baada ya kadhia hii na mengi yaliyojiri katika sakata hili, Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye ndiyo Kiongozi Mkuu wa shughuli za Serikali ndani ya Bunge alitajwa kutowajibika ipasavyo na hata baadhi yao wakimtaka ajiuzulu nafasi ya Uwaziri Mkuu kwa kushindwa kuwajibika na kuwasimamia vyema Mawaziri wa chini yake.

Kulingana na ripoti iliyotolewa na Tume iliyotumwa kuchunguza Unyama na ukatili huu uliopitiliza zilionekana picha nyingi za kutisha ikiwemo, watu waliouawa kwa kupigwa risasi, waliopigwa na kuteshwa na hata taarifa za ubakaji zilizoripotiwa mbele ya tume hiyo ambapo hata hivyo inadaiwa kuliibuka mizengwe ya kutaka kulindana ili kuficha maovu yaliyojiri dhidi ya raia.

Hatimaye kufuatia kwa unyama huu Mawaziri watatu walitenguliwa nafasi zao za Uwaziri na mmoja kujiuzulu na hivyo kuonesha ni namna gani wapo Mawaziri Mzigo ambao wanampa Mzigo Mkubwa Rais Jakaya Kikwete katika utendaji wake.

Mawaziri waliotenguliwa nyadhifa zao ni Waziri wa Mambo ya Ndani Emanuel Nchimbi(42) Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Shamsi Vuai Nahodha(51) Waziri wa Mifugo Mathayo David Mathayo(44) na Waziri wa Maliasili na Utalii Khamis Juma Suedi Kagasheki(62)ambaye kutokana na hali halisi alilazimika kujiuzulu wadhifa wake.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika vyanzo mbalimbali ni kwamba Kagasheki aliyezaliwa Agosti 30 1951 aliona picha za watu walioteswa na kwamba kutokana na mazingira ya Operesheni hiyo haoni sababu ya kuendelea kuwa Waziri ilhali Mawaziri wengine Nahodha, Nchimbi na Mathayo wakionesha wazi kutokubali kuwajibika kutokana na kile kilichoelezwa kuwa hawakuhusika moja kwa moja na tukio hilo.

Kwa upande wake Nchimbi aliyezaliwa Desemba 24 1971 alinukuliwa akisema kuwa Operesheni hiyo iliendeshwa na Jeshi na ripoti za Operesheni zilikuwa zikiwakilishwa kwa Mkuu wa Majeshi na kuwa yeye haoni mahala ambapo anahusika kufuatia kadhia hiyo.

Naye Mathayo David aliyezaliwa Julai 20, 1969 yeye alielezea wazi msimamo wake bungeni mara baada ya Balozi Kagasheki kutangaza kujiuzulu ambapo alitakataa  kujiuzulu akidai kuwa yeye haoni sababu ya kufanya hivyo kwa kuwa hakuhusika kwa lolote katika kadhia hiyo.

Kwa upande wake Nahodha ambaye aliwahi kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambaye aliingia katika Bunge la Muungano kufuatia uteuzi wa Rais Jakaya Kikwete kwa kile kilichoonekana apate fursa ya kuwemo katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya Jamhuri ya Muungano, amepata doa kutokana na kadhia hii kutokana na kutenguliwa nafasi yake ya Uwaziri.

Nahodha aliyezaliwa Novemba 20 1962 ameingia katika kadhia hiyo kutokana na nafasi yake kuwa ndiye mdhamana mkuu wa Jeshi la Wananchi na lile la Kujenga Taifa ambapo kwa mujibu wa taarifa zilizopo ni kwamba Operesheni hiyo iliendeshwa na Jeshi.

Kama walivyo Mawaziri wenzie, Nchimbi na Mathayo hakuweza kujiuzulu kwa kile kilichoelezwa kuwa yeye binafsi hakuhusika moja kwa moja na kadhia hiyo ingawa baada ya kutenguliwa kwake amekubali na kuuelezea umma kuwa hana kinyongo na ataendelea kuwatumikia wananchi kwa hali na mali na kuwa kilichotokea dhidi yake ni sawa na ajali iliyomkuta akiwa kazini.

Matukio haya yamebainishwa kutokana na kufahamika na kuundiwa tume kufuatilia, yapo mengi mfano wa haya ambayo hayafahamiki na wananchi wamekuwa wakilalamika pembeni bila kuweka hadharani yaliyowafika.

Ipo mifano mingi ya unyanyasaji katika Operesheni mbalimbali zinazoendeshwa kama vile, Operesheni ya kuwahamisha wafugaji katika maeneo ya ardhi Oevu na mengine mengi ambayo wakulima na wafugaji wamekuwa wakilalamika juu ya utendaji usiozingatia haki za binadamu na unyanyasaji uliokithiri.

Utendaji wa watendaji Mizigo wamekuwa wakitoa taswira hasi za uwajibikaji juu ya serikali inayoongozwa na Rais Kikwete na hata kumpa mzigo mzito wa kuwawajibisha watendaji ambao hawafuati kanuni na sheria kwa kuzingatia Utawala Bora. (Picha kwa hisani ya mtandao, makala kutoka vyanzo mbalimbali)
ILANI: MAKALA HII YA UCHAMBUZI NI MALI YANGU HURUHUSIWI KUCOPY  BILA IDHINI YANGU.


Post a Comment

Post a Comment