Binti wa kwanza Marehemu Dkt. Wilbert Kleruu, Eva Wilbert Kleruu akizungumza na mwandishi wa makala haya. |
Mnara wa kumbukumbu eneo la Mkungugu Isimani Iringa mahala alipofia aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Iringa Dkt.Wilbert Kleruu, mwaka 1971 |
Eva Kleruu akifuta machozi baada ya kukumbuka jambo juu ya mauaji ya baba yake miaka 43 iliyopita |
Eva Kleruu mtoto wa kwanza wa marehemu Dkt. Wilbert Kleruu aliyeuawa akipigania siasa ya ujamaa na Kujitegemea huko mkoani Iringa |
‘’NI vigumu,
kuvumilia hali hii, bali naamini haya ni
matokeo na ni mipango ya Mungu kuifanya hali hii,baba yetu alikuwa ni Muumini
wa Ujamaa na Kujitegemea aliyesimamia sera za Ujamaa na kujitegemea kama
ilivyokuwa kwa wakati ule enzi za Mwalimu Nyerere’’
‘’Serikali
ilikuwa inahimiza vijiji vya Ujamaa, ili wanananchi washiriki kwa pamoja kwenye
Kilimo cha Kufa na Kupona, baba alifuatilia kwa kina maagizo ya Mwalimu,
inawezekana hili ndilo lililosababisha kuuawa akiamini alichosimamia kilikuwa sahihi,’’anasema
Eva Wilbert Kleruu huku akibubujikwa na machozi.
‘’Samahani
umenikumbusha mbali sana miaka 43 sasa baada ya kifo cha baba yangu, nilikuwa
bado binti mdogo miaka ile ya mwanzo ya miaka ya 70, baba alikuwa ni mfuasi wa
Ujamaa na Kujitegemea na alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa aliyeagizwa
kusimamia siasa ya Ujamaa na Kujitegemea,’’anasema.
Anasema ni
hali ambayo imekuwa ngumu kuisahau kutokana na aina ya tukio lenyewe
lilivyojiri na kwamba ingekuwa kifo kile kilitokana na ugonjwa jambo hilo
lingezoeleka kwa haraka, bali hata hivyo anaamini kilichotendeka kilitokana na
uelewa mdogo juu ya mpango wa serikali kuimarisha vijiji vya Ujamaa na
kujitegemea.
Anafafanua
kuwa anaamini kifo cha baba yake kilikuwa ni sawa na kujitolea mhanga katika
harakati za Ujamaa na Kujitegemea kwani baba yake alikuwa ni miongoni mwa
waumini wa Ujamaa ambao walisimamia na kuamini kuwa siku moja nchi inaweza
kujitegemea kwa sera ya ujamaa na Kujitegemea.
Anasema
serikali wakati ule ilisimamia mpango kwa nia ya kuboresha huduma za wananchi
wka pamoja na kuondoa ukiritimba wa ubepari kwa mtu mmoja kuhodhi eneo kubwa la
ardhi jambo ambalo baadhi ya watu wasioenda maendeleo walikuwa wakilipinga.
Aidha
anasema hata hivyo anayofursa ya kuishukuru serikali kwa kuwajali na
kuwasomesha kwa ngazi ya juu ya elimu ambapo yeye alisoma hadi nchini Burgaria
na mdogo wake alipelekwa nchini Urusi katika nchi zilezile zilizokuwa zinaamini
siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.
Anasema pamoja
na tukio hilo kukatisha mapenzi baina ya baba na familia yake kwa kukatishwa
maisha kikatili serikali ilikuwa bega kwa bega na familia ya marehemu Dkt Kleruu kwa hali na
mali ambapo Mwalimu Julius Nyerere, Mzee Abeid Karume ambapo kwa bahati mbaya
mzee Karume aliuawa akiwa katika harakati za kuendelea kuienzi familia hiyo.
‘’Mzee
Karume alikuwa upande wetu sana alijitahidi kwa hali na mali kuhakikisha
tunaishi kwa upendo, amani na utulivu, lakini bahati mbaya naye aliuawa mwaka
uliofuatwa kwa risasi,’’anazungumza Eva huku akibubujikwa na machozi.
Anasema hata
mrithi wa Marehemu Karume Mzee Aboud Jumbe naye aliendeleza mahusiano ya
kuijali familia yetu ambapo pia Mzee Rashid Kawawa na Mama Getrude Mongela nao
walikuwa mstari wa mbele katika kutufariji.
‘’ Mama yetu
bado yupo hai amestaafu alikuwa akifanya kazi katika ofisi ya Mkuu wa mkoa,
baada ya kutoka Iringa kufuatia mauaji yale tulirudi Moshi, tukaendelea
kusomeshwa na serikali Mzee Karume alikuwa mstari wa mbele kutusaidia.
‘’Mama yetu
kwa sasa anaishi Moshi, niko na wadogo zangu, watatu, mmoja anaitwa Andrew,
mwingine Carmen ambaye ni Bibi Afya na
Edwin ambaye ni mjasiriamali wote tulisomeshwa kwa ngazi za juu, tunaishukuru
serikali kwa kutujali,’’anabainisha.
Kadhalika
anasema kuwa katika kuendelea kujisahaulisha tukio lile la kikatili
lililofanywa dhidi ya baba yake amepanga kukutana na familia ya marehemu
Mwamwindi ambaye ndiye aliyemuua baba yake, ili wazungumze na kuanzisha ukurasa
mpya wa maisha.
‘’Unajua
visasi vinarithishwa kimaumbile, bila kukutana na familia ile vizazi vyetu
vinaweza kujikuta vikiingia katika dhambi isiyotarajiwa, napenda nikutane na
mtoto mkubwa wa Mzee Mwamwindi, ili tufungue ukurasa mpya wa maisha, hatujawahi
kukutana hata mara moja wala hatujuani,’’anasema Eva.
Anasema nia
ya kukutana naye ni kuanzisha uhusiano mpya ambao ulitoweka kwa zaidi ya miaka
40 huku viongozi wa wakati huo Mwalimu Nyerere, na Mzee Karume nao wakiwa
wametangulia mbele ya haki hivyo anaamini kwa kukutana na wanafamilia hao
utaanzishwa uhusiano chanya wenye lengo la kudumisha amani na utulivu.
‘’Sifikirii
wala sijawahi kufikiria kulipiza kisasi, tulikaa kama familia tukamuomba Mungu
atulinde na vitendo vya kishetani, tunaamini Mungu anaendelea kutulinda na
kilichotokea kilikuwa ni dhamira iliyosukumwa na vitendo vya kishetani,’’anasema
Eva.
Post a Comment
Post a Comment