Magoli 2-1 yaliyoongozwa na timu ya Rhino Rangers dhidi ya Prison hadi kipindi cha kwanza cha mchezo kati ya timu hizo yalianza kubashiri majaliwa ya Prison kubaki ama kushuka daraja kucheza ligi kuu msimu ujao.
Wapenzi wa soko Jijini Mbeya ambao walizoea kuziona timu mbili za mkoa huu zikicheza ligi kuu walianza kuonesha kukata tamaa na kutoa maneno ya vitisho dhidi ya wachezaji na kocha wa maafande hao wa Prison iwapo wangeshindwa kuonesha ubabe wa kuwafunga maafande wa Rhino ya mjini Tabora.
''Leo tutawatandika viboko uwanjani, haiwezekani kila mwaka mkoa ukae vikao vya kuinusuru timu ya Prison, safari hii mtalala nacho na viboko tutawatandika hapa hapa uwanjani, ''zilisikika kauli za mashabiki zikijirudia rudia mara kwa mara wakati timu hizo ziko katika vyumba vya mapumziko.
Hali hiyo ya kukata tamaa kushinda mechi hiyo yalianza kuonekana dakika ya 19 ya mchezo baada ya mchezaji wa Rhino Rajab Twaha kupiga mchomo mkali uliomwacha kipa wa Prison Jamal Abdul akichupa bila mafanikio na kuhesabu bao la kwanza kwa timu ya Rhino.
Goli hilo lilidumu hadi dakika ya 43 ambapo mchezaji wa Peter Michael aliposawazisha bao hilo kwa mkwaju iliowapita walinzi wa Rhino na hivyo kuwainua mashabiki ambao walionesha kuikatia tamaa timu ya Prison katika mchezo wa leo.
Hata hivyo goli hilo la Prison liliamsha machamchaka kwa maafande wa Rhino ambao walianza kulishambulia goli la Prison kama nyuki na kusababisha kupata goli dakika 45 bao lililofungwa na Salum Majid kutokana na uzembe wa golikipa wa Prison ambaye aliudaka mpira na kuutema.
Wakati wa mapaumziko mashabiki wa mpira wa Jiji la Mbeya walionesha hisia zao za hasira wakiamini kuwa timu hiyo huenda itashindwa kufanya vyema na kwa mchezo huo ingekuwa ni tiketi yao ya kushuka daraja wakiungana na wapinzani wao Rhino.
Kipindi cha pili kilianza ambapo Kocha wa timu ya Prison David Mwamwaja aliamua kufanya mabadiliko ya kumtoa golikipa Jamal Ali na kumuingiza Beno Kakolanya.
Kipindi hicho cha pili kilianza kwa kasi ambapo dakika ya 47 Prison ililiona lango la Rhino baada Peter Michael kwa mara nyingine kuchomoka na mpira upande wa kushoto na kuwatoka walinzi wa Rhino Amani Juma,Ali Mwanjiro, Abdallah Said na Julius Masunga na kupiga shuti iliyompita golikipa wa Rhino Abdulkarim Mtumwa na kuingia wavuni na kufanyaa matokeo kuwa 2-2.
Goli hilo liliwapa uhai mashabiki na washangiliaji wa Prison waliokuwa wakiongozwa na kikosi cha Brass Band ya Magereza, huku wakicheza kwa kujiamini na kuonesha mbwembwe za matumaini ya kuongeza bao jingine.
Matumaini hayo yalikatishwa dakika ya 63 baada ya mchezaji wa Rhino Julius Masunga kuipatia bao la 3 timu yake kwa njia ya penalt baada ya mchezaji wa Prison kumfanyia madhambi mchezaji wa Rhino katika eneo la adhabu.
Ilikuwa ni dakika ya 77 mchezaji machachari wa Prison Fred Chudu aliyewanyanyua mashabiki uwanjani kwa kusawazisha bao hilo baada ya kupokea pasi kutoka kwa Bryton Mponzi aliyeingia kipindi cha pili na kusababisha kashkash katika lango la Rhino.
Baada ya goli hilo kila timu ilianza kutafuta bao la ushindi huku bahati ikiangukia kwa wenyeji Prison ambao dakika ya 82 ya mchezo mchezaji Ibrahim Hassan aliwanyanyua mashabiki wa Prison kwa kupachika bao na wachezaji hao kushangilia hadi nje ya uwanja na kuwafuata wachezaji wa timu Mbeya City aliokuwepo uwanjani hapo na kupeana mikono ikiwa ni dalili kuwa wamenusurika kushuka daraja na kwamba wataendelea kuwa pamoja katika ligi hiyo msimu ujao.
Hadi Kipenga cha mwisho kinapulizwa Prison ilitoka kifua mbele kwa bao 4-3.
Kwa upande wake kocha wa timu ya Prison ambaye kwa muda wote wa mchezo alikuwa katika wakati mgumu kwa timu yake kucheza vibaya alionekana akiwa ma sura ya matumaini na kueleza kuwa mchezo ulikuwa mgumu ingawa timu ya Rhino ilionesha kucheza kwa kurelax ikijua wazi kuwa iko mkiani mwa timu zote zinazocheza ligi Kuu.
Naye kocha wa Rhino ambaye awali aliwahi kuifundisha Prison Jumanne Chale alisema kuwa mchezo huo ulikuwa mzuri ingawa timu yake imeshindwa katika mchezo huo na kusema kuwa dalili za ushindi kwa timu yake zilikuwa wazi isipokuwa makosa madogo yaliyofanywa na wachezaji wake yametumiwa na Prison kupata ushindi.
Kesho katika uwanja huo wa Sokoine timu mbili zenye upinzani wa aina yake zinaingia dimbani Mbeya city wakiwakaribisha Azam ya Jijini Dar, katika mzunguko wa kwanza timu hizo zilitoka sare ya bao 2-2 katika uwanja wa Azam Complex Chamazi Jijini Dar es salaam..
Post a Comment
Post a Comment