Baadhi ya Waandishi wa Habari wakiwa katika kikao na Mkuu wa mkoa wa Mbeya ofisini kwake leo asubuhi. |
Mkurugenzi wa Sayansi ya Makosa ya Jinai na Vinasaba kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Gloria Omar akifafanua jambo juu ya utambulisho wa dawa za kulevya |
Wakili kutoka Tume ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini Charles Malamula(katikati) wakati wa taarifa ya siku ya Dawa za Kulevya nchini itakayofanyika Kitaifa mkoani Mbeya. |
BAADA ya
kimya cha takribani miaka kumi tangu watu
wanaodaiwa kuwa ni Vigogo wanaohusishwa na usafirishaji na uingizaji wa Dawa za
Kulevya nchini majina yao kupelekwa kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam
Yusuf Makamba, Tume ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini imeendelea kusuasua kutaja majina ya Vigogo hao.
Taarifa za
kuwepo kwa Vigogo 12 wa Dawa za Kulevya ziliibuliwa Mkoani Mbeya
mwaka 2014 ambapo baadhi ya watumiaji wa dawa hizo maarufu kwa jina la‘mateja’
waliodai kujihusisha na Dawa hizo waliyapeleka majina ya vigogo 12 kwa Makamba ambaye
hadi anastaafu hajawahi kuyataja majina hayo.
Akizungumza
katika kikao na waandishi wa habari katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas
Kandoro,juu ya taarifa za maadhimisho ya siku ya Dawa za Kulevya Nchini yanayofanyika
kesho Jijini Mbeya,Mchambuzi Mkuu kutoka Tume ya Dawa za Kulevya January Ntisi
alisema majina ya Vigogo hao yaliwasilishwa katika tume na yanaendelea
kufanyiwa kazi kupata uthibitisho wa uhusika wao.
‘’Majina yalifika Tume, tuliyapokea lakini
hatuwezi kuyataja, baadhi yao walishakamatwa na kesi zao zimefikishwa katika
mahakama zetu na zile za nje, zipo taratibu ambazo zinaendelea kuhusiana na sheria
za kimataifa juu ya suala hili,’’alisema Ntisi.
Alisema kuwa
wapo ambao walitajwa majina yao ambao bado wanaendelea kutafutwa na kwamba hata
hivyo udhibiti wao umekuwa ni mgumu kutokana na kuwa na mtandao mkubwa watu
matajiri wenye uwezo mkubwa wa kutumia vifaa vya kisasa ikiwemo Boti ziendazo
kasi.
‘’Wana
mtandao mkubwa sana, wanatumia Boti ziendazo kasi, tunaendelea kuwasaka kwa
kushirikiana na baadhi ya nchi za kigeni, suala hili linahitaji umakini mkubwa,’’alifafanua
Ntisi.
Kuhusu
kuachiwa huru kwa baadhi ya watuhumiwa wa Dawa za Kulevya na vidhibiti vya dawa
za kulevywa vinavyofikishwa mahakamani kupotea na kuoneka ni feki Mkurugenzi wa
Sayansi ya Makosa ya Jinai na Vinasaba Gloria Omar alisema kuwa taarifa zote
zinazofika kwa mkemia mkuu zinafanyiwa kazi kulingana na ushahidi.
‘’Taarifa
zinazoletwa kwa Mkemia Mkuu zinafanyiwa kazi kitaalamu na kuthibitishwa
kulingana na ushahidi,’’alisema.
Akizungumza
kwa njia ya simu kutoka Jijini Dar es salaam Mwanaharakati wa kupigania Haki za
Binadamu na Vita Dhidi ya Dawa za Kulevya Mchungaji William Mwamalanga alisema kuwa Tume
ya Kudhibiti Dawa za Kulevya haina uwezo tena wa kusaidia tatizo hili na badala
yake zielekezwe nguvu katika kitengo cha Jeshi la Polisi.
‘’Tume
imefeli katika hili, watuhumiwa waliotajwa kuhusika na Dawa za kulevya miaka
kumi iliyopita wamerejea kwa kasi na wanaedeleza biashara hizi,Uwanja wa ndege
wa Mwalimu Nyerere umekuwa uchochoro wa kupitisha mihadarati,’’alibainisha.
Alisema kuwa
kati ya Viwanja vya Ndege vya Kimataifa katika nchi za Afrika Mashariki uwanja
wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere ndio uwanja dhaifu kuliko viwanja
vyote ambapo umekuwa ukitumika kuingiza na kusafirisha Dawa za Kulevya bila
udhibiti makini.
Alisema kuwa
usafirishaji na uingizaji wa mihadarati umeongezeka mara tatu kwa kipindi cha miaka
kumi na kwamba idadi ya vifo na ongezeko la watumiaji limekuwa ni tishio kubwa
na kwamba tume imeshindwa kudhibiti hali hiyo kwa kipindi chote tangu
ianzishwe.
Kwa mujibu
wa Mchungaji huyo wa Kipentekoste alisema kuwa hadi kufikia Juni mwaka huu kulingana na
utafiti uliofanywa na wanaharakati wa mapambano dhidi ya Dawa za kulevya nchini
ni kwamba jumla ya vijana 6708 wamefariki kutokana na Dawa za kulevya katika
Jiji la Dar es salaam pekee.
Alisema kuwa Jiji la Mbeya jumla ya vijana 48
wamekufa ilhali katika Miji ya mipakani ya Tunduma na Kyela jumla ya vijana 104
wamefariki dunia na katika mji wa Tanga jumla ya vijana 71 wamefariki dunia
ilhali Jiji la Mwanza jumla ya vijana 36 wamefariki kutokana na matumizi ya
dawa za kulevya.
Post a Comment
Post a Comment