JUMLA ya
miradi 124 imekaguliwa na Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) katika mikoa
mitatu ya Nyanda za Juu kusini ya Mbeya, Rukwa na Katavi kwa kipindi cha miezi
miwili ya Julai na Agosti mwaka huu.
Miradi iliyokaguliwa
ni pamoja na Migodi 42,Viwanda 13,Vituo vya Mafuta 56, Hoteli 2, Mashamba 3 na
miradi mingine ipatayo 8 ambayo ni mchanganyiko wa shughuli mbalimbali za
kijamii.
Akizungumza
wakati wa mkutano wa NEMC na wadau wa mazingira kwenye ukumbi wa Mkapa Jijini
Mbeya, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Mazingira nchini Mhandisi Bonaventure Baya
alisema kuwa lengo la ukaguzi huo ni kufuatilia utunzaji wa mazingira katika
miradi mbalimbali ya uzalishaji na maendeleo.
Alisema
Baraza la Mazingira liliunda vikosi kazi ili kufuatilia kwa kina
utekelezaji wa shughuli za mazingira kwa lengo la kubaini viwango vya
uzingatiaji wa sheria ya mazingira pamoja na kanuni mbalimbali za uendeshaji wa
miradi.
Mhandisi
Baya alisema kuwa vikosi kazi hivyo vilifanya ukaguzi wa kina katika mikoa ya
kanda ya Ziwa, baadhi ya miradi katika mkoa wa Dar es salaam, kanda ya
Mashariki na kaskazini na kuwa ukaguzi huo wa miradi ya mazingira umekusudiwa
kuwa endelevu kwa kuhusisha kanda zote nchini.
Alisema
kuwa miradi iliyokaguliwa imegawanyika katika makundi matatu ambayo
itatekelezwa kwa kufuata matakwa ya sheria, kanuni na taratibu za utunzaji wa
mazingira, miradi iliyokuwa ikijitahidi kufuata sheria na taratibu za mazingira
na miradi isiyokuwa na mpango madhubuti wa hifadhi ya mazingira.
Alibainisha
kuwa miradi isiyokuwa na mpango madhubuti wa hifadhi imesababisha kuvunja
sheria, kanuni na taratibu za usimamizi na utunzaji wa mazingira na kuwa kati
ya miradi 124 ni asilimia mbili tu ya miradi ndiyo iliyotekelezwa kwa kufuata
sheria za mazingira.
Baya
alisema kuwa asilimia 11 ya miradi ina vibali vya mazingira lakini
haikuzingatia utekelezaji wa sheria na mpango wa kutunza mazingira(EMP) ambapo
asilimia 87 ya miradi iliyopo inatekelezwa bila vyeti.
Awali
akifungua mkutano huo Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro aliwataka viongozi wa
ngazi mbalimbali za kijamii kushiriki kwa pamoja katika uhifadhi wa mazingira
ili kuweka mustakabali mzuri wa maisha ya binadamu na maendeleo yake.
‘’Jukumu
la utunzaji wa mazingira ni letu sote tunapaswa kuwa wakereketwa wa mazingira
kwa maslahi yetu na vizazi vijavyo,’’alisema Kandoro.
Alifafanua
kuwa upo uwiano mkubwa katika ya afya za binadamu na uhifadhi wa mazingira na
kuwa iwapo mazingira yataharibiwa afya za binadamu nazo zitakuwa hatarini.
|
Post a Comment
Post a Comment