Mshereheshaji mashuhuri nchini Charles Mwakipesile akimfariji mfiwa Nicco Mwaibale mara baada ya kuwasili kijiji cha Newland Kiwira, Tukuyu kwa ajili ya mazishi. |
Mmoja wa watoto wa marehemu Nicco Mwaibale akijifuta machozi huku akifarijiwa na kaka yake Kulwa Mwaibale mara baada ya kuwasili kijijini |
Kulwa Mwaibale akimfariji shangazi yake kwa kumfuta machozi ke mara baada ya kuwasili msibani hapo wakati wa mazishi |
Kulwa(kulia) na Dotto Mwaibale wakati wa mazishi ya mama yao mpendwa |
Vijana wa Skauti wakiusindikiza mwili wa Bibi Twitikege Mlagha katika nyumba yake ya milele. |
Vijana wa Skauti wakiwa wamebeba mwili wa marehemu Twitikege wakiusindikiza kwenye nyumba yake ya milele |
Baadhi ya watoto na wajukuu wa Bibi Twitikege wakilia kwa uchungu wakati wa mazishi yaliyofanyika kijiji cha Newlanda Kiwira. |
Jeneza lenye mwili wa marehemu Twitikege likishushwa kwenye nyumba yake ya milele |
Baadhi ya watoto wa marehemu wakiweka shada la maua kwenye kaburi la mama yao kipenzi |
Umati wa waombolezaji waliohudhuria mazishi ya Bibi Twitikege katika kijiji cha Newland Kiwira Tukuyu wilayani Rungwe. |
Na Rashid Mkwinda
Asubuhi ya Disemba 13, 1940 zaidi ya miaka 70 huko
katika kijiji cha Katumba wilayani Rungwe, familia ya mzee Mafumo Mlagha
ilikuwa katika furaha kwa kumpata mtoto wa kike baada ya kiu ya muda
mrefu ya kuwa na mtoto wa kike.
Ilikuwa ni siku ambayo familia hii
ilibahatika kuwa na mtoto wa kike waliyempa jina la Twitikege.
Anga la kijiji cha Katumba lenye jua lililowakia
mandhari nzuri ya kijani kwenye kijiji kilichoshamiri kilimo cha Migomba na
Chai binti wa kike
alizaliwa,Ndege wa angani na vipepeo wenye rangi nzuri walioruka kutoka mti mmoja kwenda mti mwingine walionesha furaha yao ni kama ilikuwa ni sehemu ya kukamilisha uzawa wa binti huyo,nderemo ziligubika familia hiyo na kijiji kwa
ujumla.
Twitikege aliliona jua kwa mara ya
kwanza, familia ya Mzee Mafumo Tabulo Mlagha wa kijiji cha Katumba wilayani
Rungwe walijipatia mtoto wa kike waliyempa jina la Twitikege,walijivunia kuwa
na uwiano wa watoto wa jinsi mbili, kutokana na kuwa na mtoto wa kiume katika zao la kwanza.
Twitikege kama walivyo watoto wengine wa
familia ya kabila la Kinyakyusa alikuzwa na kulelewa katika maadili yanayoshabihi
mila na desturi za wenyeji wa maeneo
hayo.
Aliishi na kulelewa katika familia ya ukoo
wa kichifu,makuzi yake yalikuwa ni sawa na makuzi ya watoto wengine wa kiafrika
waishiyo maeneo ya vijijini.Katika zama hizo neema ilitawala kutokana na ardhi
ya kaya hizo kustawi kila aina ya chakula na hivyo kumfanya binti Twitikege
akue katika neema.
Maeneo mengi ya vijijini kwa zama hizo
ardhi`ilikuwa na rutuba tele na hivyo kusheheni mazao ya kila aina na hivyo kufanya uzawa wa wakati huo kuwa
na maisha yenye afya bora kutokana na wingi wa chakula kilichopatikana katika
maeneo hayo.
Kama ilivyo desturi na mila za kiafrika
binti anapofikisha umri wa kuvunja ungo aliangaliwa na kutunzwa kwa kila hali
ambapo Twitikege kulingana na makuzi ya kimaadili aliyokulia alipofikisha umri
wa miaka 13 mwaka 1953 alichumbiwa na kijana wa kijiji jirani na nyumbani kwao.
Alikuwa ni Anyitike Mwakwama Mwaibale ambaye kama walivyo
vijana wengi wa wakati huo naye alitokea katika familia iliyostaarabika ya
wazazi wachamungu walioishi kwa maadili kulingana na mila na desturi za maeneo
hayo.
Baada ya kufunga ndoa Twitikege na mumewe
Anyitike alichukua dhamana ya kumlea Twitikege wakaishi vyema nao walirithi
desturi njema ya wazazi wao,waliishi kwa wema na uadilifu na kuahidi kuishi kwa
raha mustarehe katika kipindi chote cha Uhai wao.
Matunda ya ndoa yao yalibarikiwa na
hatimaye wakajaaliwa kupata watoto wake kwa waume ambao nao waliwalea na
kuwasomesha kama walivyolelewa wao enzi za ujana wao.
Kwa takribani miaka 50 ya ndoa yao walifanikiwa kupata watoto 9 wa kike na kiume,watatu
kati yao walitangulia mbele ya haki na kubaki watoto sita.
Kama ilivyokuwa katika malezi yao katika
familia zao Twitikege na Mwaibale waliwalea watoto wao kwa maadili na miongozo
ya dini bila kusahau mila na desturi za Kinyakyusa ambazo ziliwafanya
wamudu kuishi na watu tofauti na kabila tofauti.
Mwaka 2007 ni siku ambayo Bimkubwa huyo Twitikege Mlagha akiwa ametimiza jumla ya miaka 53 ya ndoa yake
na mumewe alipata pigo ambalo kamwe hakuweza kulisahau katika maisha yake.
Alimpoteza mumewe Mzee Anyitike Mwakwama Mwaibale
ambaye alifariki na kumuachia ukiwa, ingawa alipata faraja kwa uwepo wa wajukuu
na vitukuu lukuki waliotokana na watoto wake yeye na mumewe bali pengo la kumpoteza mumewe kamwe halikuweza
kuzibwa.
Halikuzibwa pengo la mumewe ndani ya moyo
wake, majonzi na fikra za kumpoteza mwenzi wake vilitawala katika fikra zake
ingawa alipata faraja ya kutembelewa na wanawe waliokuwa wakiishi maeneo ya
mbali na kijijini kwake.
Mara kadhaa niliwasikia wanawe wakihitaji
kuomba ruhusa katika kazi zao ya kuja kumuona mama yao na kumpa faraja, ilikuwa
ni katika jitihada za kumsahaulisha machungu aliyokuwa nayo ya kumpoteza mwenza
wake aliyeishi naye tangu akiwa kijana hadi anazeeka.
Alimkumbuka Anyitike, alikumbuka
walivyokuwa vijana, alikumbuka siku ya kwanza kuchumbiwa na Anyitike, alikosa
raha akajikuta akilia peke yake na kuongezeka majonzi ya kumkosa mumewe ambaye
kadri walivyoishi walizoeana na hata kufikia hatua ya kuwa kama ndugu
waliotokana na baba na mama mmoja.
Ni takribani miaka saba tangu aondoke
mumewe Anyitike, Twitikege kwa kipindi cha miaka miwili alianza kukumbwa na
maradhi ya Uzee na hivyo kushindwa kujihudumia kwa shughuli alizozoea
kujihudumia mwenyewe na kujikuta akilazimika kuomba msaada kutoka kwa wajukuu
na wanawe walio karibu.
Bimkubwa huyo aliendelea kuugua na kupata
matibabu katika hospitali mbalimbali za ndani na nje ya mkoa wa Mbeya na
hatimaye mwaka 2014 alichukuliwa na wanawe kuelekea Jijini Dar es salaam kwa
ajili ya matibabu.
Ijapokuwa alikuwa katika maradhi bali
aliendelea kuwa faraja kwa wanawe kila walipomuona wakiwa pamoja wakizungumza naye
hili na lile.
Kila mtoto alipenda kuwa karibu na mama
yao ili apate baraka zake hata hivyo kutokana na maradhi aliyokuwa nayo
hakumudu kukaa kwa watoto wote kwa wakati wote bali alianza kuzidiwa na homa na
kulazimika kulazwa hospitali kwa ajili ya matibabu.
Kila nyumba ya wanaye alipoenda kuishi
nyumba hiyo iligubikwa na furaha na Baraka,wajukuu na watoto wakitamani kuwa
naye wakati wote wakifurahia uwepo wake katika familia hizo.
Kulazwa kwake kuliacha simanzi kwa wajukuu
na watoto wakikumbuka ucheshi wake na matarajio yao ya kumuombea walau arejee
katikasiha njema ili arejeshe furaha na Baraka katika nyumba zao kama
ilivyokuwa awali.
Haikuwa bahati tena kwa vitukuu, wajukuu na
watoto kumuona Bimkubwa huyu akiwa katika hali yake ya awali,Mwenyezi Mungu
aliamua kumuita.
Kama ilivyokuwa wakati wa kuzaliwa
kwake,tarehe ileile aliyozaliwa ya Disemba 13 ndiyo hiyo hiyo Disemba 13, 2014 akiwa
na jumla ya miaka 74 aliaga dunia usiku wa saa 5:00 Jijini Dar es salaam
akiacha majonzi makuu na vilio kwa vitukuu, wajukuu na wanawe sita waliopo.
Marehemu aliagwa Jijini Dar es salaam na
mwili wake kusafirishwa Mkoani Mbeya katika kijiji cha Newland kilichopo kata
ya Kiwira wilayani Rungwe na kuzikwa Disemba 17,2014 katika makaburi yaliyopo katika mashamba ya
familia mkabala na kaburi la mumewe kipenzi.Apumzike kwa amani!!Aamen!!
Post a Comment
Post a Comment