Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Ahmed Msangi akiwa pamoja na waombolezaji wakati wa kuusafirisha mwili wa Sajent Patrick aliyejiua kwa kujipiga risasi |
Patrick Kondwa enzi za uhai wake |
Waombolezaji wakiwa msibani katika kota za Jeshi la Polisi mjini Vwawa wilayani Mbozi |
Ndugu jamaa na marafiki wakipita kutoa heshima mbele ya jeneza lenye mwili wa Sajent Patrick kabla ya kusafirishwa mwili huo kuelekea Mkoani Katavi wilayani Mpanda kwa ajili ya mazishi |
Kamanda Msangi akiteta jambo na mmoja wa maofisa wa Polisi wilayani Mbozi |
Waombolezaji wakishiriki kusaidia kuliweka vyema jeneza lililobeba mwili wa Sajent Patrick katika gari kabla ya kuusafirisha mwili huo. |
Kamanda wa Polisi Ahmed Msangi akitoa maelekezo kwa dereva anayesafirisha mwili wa marehemu |
Gari ya Polisi ikianza safari kuusindikiza mwili wa Sajent Patrick mkoani Katavi |
''Naendelea kusisitiza ndugu zangu Waandishi wa Habari tunaendelea kufanya uchunguzi juu ya kifo hiki, bado hatujajua chanzo cha yeye kujitwanga risasi'' |
NI vigumu kuamini!!! lakini ndio ukweli halisi wa tukio hili, wala si maigizo katika sinema bali ni tukio halisi la mauaji ya kusikitisha na kuacha simanzi kwa wanafamilia na ndugu rafiki na jamaa wa askari
Polisi wa mjini Vwawa wilayani Mbozi mkoani Mbeya Patrick Kondwa(54)
mwenye cheo cha Sajenti.
Askari huyo mwenye nambari ya utambulisho wa kazi D4176 aliamua kujitoa uhai kwa kujilazimisha kwa kujitwanga risasi iliyopitia mdomoni na kutoboa kisogo chake majira ya saa 9:00 usiku, huku akiacha maswali lukuki ya sababu za kujikatisha uhai wake ilhali alikuwa akitegemewa na familia na dola.
Kujiua kwa askari huyo mbali na kuacha maswali lukuki kwa jamii inayomzunguka imegubika utusi tusi kutokana na marehemu kutoacha ujumbe wowote wa sababu za kujitoa uhai wake huku akiwa amebakiza muda mfupi kustaafu kwa mujibu wa sheria kulingana na umri wake wa miaka 54.
''Hakuna aliyedhania kuwa Afande huyu kama angeweza kufanya jambo hili sote tupo katika taharuki, hatuelewi sababu za hatua hii aliyochukua,''alisema Askari mwenzie katika kituo hicho ambaye hakupenda kutajwa jina lake kwa kuwa si msemaji wa Jeshi la Polisi.
''Jamaa tulikuwa naye lindoni usiku, tumefanya naye kazi hadi saa 6 usiku,hatukujua kama alikuwa na siri kubwa ndani ya nafsi yake iliyotuachia majonzi wenzie,''alisema askari mmoja wa kike ambaye naye anafanya kazi katika kituo hicho cha Vwawa wilayani Mbozi.
Inaelezwa kuwa askari huyo ambaye ameacha mjane na watoto wanne alikuwa ni msimamizi katika ghala la silaha na vielelezo vya Jeshi la Polisi katika kituo hicho kidogo cha polisi ambacho kinahudumia wilaya ya Mbozi na Momba na kwamba usiku wa tukio hilo aliingia katika chumba chake cha kazi na kujitwanga risasi kupitia mdomoni ambayo ilijitokeza kisogoni.
Awali akizungumzia tukio hilo kwa njia ya simu kabla hajafika eneo la tukio Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya Ahmed Msangi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo la kujiua kwa askari huyo na kusema kuwa chanzo cha kifo cha askari huyo kinachunguzwa.
Akizungumza
kwa njia ya simu kutokea Jijini Mbeya Kamanda wa Polisi mkoani humo Ahmed
Msangi alisema kuwa amepata taarifa za kifo cha askari huyo ambacho kimetokea usiku
wa kuamkia jana.
Kamanda
Msangi alisema kuwa ingawa kuna minong'ono mingi juu ya tukio hilo la kifo bali Jeshi la Polisi bado linafanya uchunguzi kujua sababu za askari huyo kujiua akiwa katika chumba chake cha kazi.
‘’Sina
taarifa za ziada juu ya kifo hicho zaidi ya taarifa hizi ninazokupa, askari
huyo mwenye cheo cha Sajenti alikuwa kwenye lindo kama kawaida aliondoka
lindoni akielekea nyumbani kwake,kabla ya kufika kwake alipitia kwenye chumba
cha vielelezo huko akajipiga risasi ya mdomoni ikatokea kisogoni na kufariki dunia,’’alisema Kamanda Msangi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na usalama wilayani Mbozi ambaye ni Kaimu Mkuu
wa wilaya hiyo Rosemary Senyamule alisema kuwa tukio hilo limeibua taharuki kwa
jeshi la polisi na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya.
Alisema kuwa
askari huyo amekutwa akiwa amekufa katika chumba cha kuhifadhia vielelezo vya
polisi akiwa amejipiga risasi kichwani na kuwa baadhi ya watu walieleza kuwa
aliweka mtutu wa bastola mdomoni na kuifyatua bastola na kusababisha kifo
chake.
Hata hivyo
Senyamule alisema kuwa tukio hilo la kuchukua maamuzi ya kujitoa uhai halifai katika
jamii na kuwa hata kama marehemu alikuwa ana msongo wa mawazo alipaswa
kutochukua uamuzi huo mbaya.
‘’Ni tukio
la kusikitisha halipaswi kuchukuliwa na mtu yoyote, ni dhambi kwa Mungu na
linaacha athari mbaya kwa wanafamilia na jamii iliyobaki, hatupaswi kuchukua
maamuzi ya aina hiyo hata kama tuko katika matatizo,’’alisema.
Hata hivyo
baadhi ya watu ambao hawakupenda kutajwa majina yao walielezea kuwa huenda kifo
hicho kimetokana na upotevu wa silaha katika kituo hicho ambao unaelezwa
kutokea hivi karibuni jambo ambalo limekanushwa na Kamanda Msangi.
Kamanda
Msangi alisisitiza kuwa bado Jeshi la Polisi linachunguza tukio hilo na kuwa
taarifa zilizosambaa hazijathibitishwa na Jeshi hilo.
Kwa upande
wao baadhi ya waombolezaji walidai kuwa tukio hilo ni la kusikitisha ambalo
halikupaswa kufanywa na mtu ambaye ana dhamana na ulinzi wa amani na mali za
raia.
‘’Ni tukio
la kusikitisha, hatuna jinsi, ila marehemu alichukua uamuzi usiofaa kujitoa
uhai wake,’’alisema Joseph Samson ambaye ni askari Magereza wa Gereza la
Mahabusu Vwawa wilayani Mbozi.
Marehemu
Kondwa ameacha mjane na watoto wawili ambapo mwili wake umesafirishwa jana
kuelekea wilayani Mpanda mkoani Katavi.
Post a Comment
Post a Comment