Wachina wa pembe za Faru wakisindikizwa mahakamani ya hakimu mkazi mkoa wa Mbeya kusomewa hukumu ya kesi inayowakabili ya kukuitwa na nyara za serikali pembe 11 za Faru |
Gari iliyotumiwa na wachina kusafirisha pembe za Faru kutokea nchini Malawi |
MAHAKAMA ya
hakimu mkazi mfawidhi mkoa wa Mbeya imewahukumu kwenda jela miaka 20 watalii wanne raia wa nchini China ambao wamekutwa na nyara za
serikali pembe za Faru 11 zenye thamani ya dola za kimarekani 418,000 zenye
uzito wa kgm 53.3 kinyume cha sheria.
Akisoma
hukumu hiyo iliyochukua takribani saa 4 kuanzia saa 5:00 asubuhi hadi saa 9:45
alasiri Hakimu wa mahakama ya hakimu mfawidhi mkoa wa Mbeya Michael Mtaite
alisema kuwa adhabu hiyo ya kifungo cha miaka 20 inakwenda pamoja na kulipa
faini zaidi ya dola 800.
Hakimu Mtaite amesema kuwa washitakiwa hao Song Lei(32)Xiao Shaodan(29)Chen
Jianlian(33)na Hu Liang kwa pamoja walikutwa na nyara hizo pembe za Faru Novemba
6 kwenye mpaka wa Tanzania na Malawi, Kasumulu wilayani Kyela wakati wakijaribu
kuvuka mpaka kuingia nazo nchini.
Amesema washitakiwa hao ambao walikuwa na gari aina ya Toyota
Hilux Surf yenye namba za usajili T 103 DER ambapo katika gari hilo
walitengeneza sanduku maalumu la chuma chenye kufuri na bawaba na kuhifadhi
pembe hizo kwa nia ya kuziingiza nchini.
Hakimu Mtaite ambaye alikuwa akisoma hukumu hiyo kwa
Kiswahili huku ikitafsiriwa kwa lugha ya Kichina na mkalimani Mtanzania
Manifred Lyoto amesema kuwa raia hao wa China wanatiwa hatiani kutokana na
ushahidi uliotolewa mahakamani kujiridhisha na ushahidi uliotolewa na upande wa
mashtaka.
Aidha amesema kuwa mahakama imezingatia kiini cha kosa na
kujiridhisha kuwa washatikiwa walipanga kutekeleza kosa la jinai kwa kuingiza
nchini nyara za serikali pembe 11 za Faru bila kibali,kutekeleza kuingiza pembe
hizo nchini na kukutwa nazo wakizimiliki bila kibali kutoka kwa mkurugenzi wa
wanyama pori.
Awali kabla ya kutoa hukumu hiyo wakili wa serikali Wankyo Simon
ameitaka mahakama hiyo kutoan adhabu kali dhidi ya washtakiwa kutokana na
kukithiri kwa vitendo vya uhalifu na ujangiri dhidi ya wanyama pori walio
hatarini kutoweka.
Wakili Simon amesema kuwa kitendo cha washtakiwa hao pia
kinakiuka mkataba wa Kimataifa unaolinda na kuhifadhi wanyama walio mbioni
kutoweka ikiwa ni pamoja na sheria za
Uhujumu uchumi na kuitaka mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa raia
wengine wanaosingizia kuingia nchini kwa ajili ya utalii.
Amesema raia hao waliingia nchini kwa nia ya kufanya utalii
na kuwa badala yake wamekuja kufanya uhalifu jambo ambalo linapaswa kuchukuliwa
kuwa ni mfano kwa adhabu kali ambayo mahakama inapaswa kutoa dhidi ya
washtakiwa.
Naye Wakili wa upande wa utetezi Ladslaus Rwekaza amesema
kuwa mahakama iangalie uwezekano wa kuwapunguzia adhabu hasa ikiangaliwa
mahusiano ya urafiki baina ya Tanzania na China na kuwa kutokana na kosa hilo
kuwa ni la kwanza na kutokuwa na historia ya makosa ya aina hiyo kwa
washtakiwa, mahakama itoe adhabu kwa jicho la huruma.
Hata hivyo Hakimu Mtaite ambaye aliahirisha hukumu hiyo kwa
saa nzima amesema mahakama inawahukumu jumla ya miaka 38 jela kwa makosa matatu
ambapo adhabu hiyo itakwenda kwa pamoja na kutumikia jumla ya miaka 20 jela
huku wakitakiwa kulipa faini ya dola zaidi ya 800,000.
Post a Comment
Post a Comment