BAADHI ya askari Polisi
waliokuwepo ndani ya chumba cha Mahakama Kuu Kanda ya Iringa wakati askari mwenzao
Pacificius Cleophace Simoni akitiwa hatiani kwa kosa la mauaji ya bila
kukusudia ya mwanahabari Daudi Mwangosi, walivuruga utulivu wa mahakama hiyo
baada ya simu zao kupigwa wakati Jaji Paulo Kiwehlo akiendelea kusoma maelezo
ya kesi hiyo.
Hatua hiyo iliyowashangaza
wanahabari na raia wengine waliojitokeza kusikiliza hukumu hiyo, ilitokea muda
mfupi baada ya mmoja askari Polisi aliyekuwepo ndani ya mahakama hiyo kutoa
tangazo liliwatisha watu wengine kabla shughuli ya mahakama hiyo haijaanza.
Huku akionekana ana
hasira, kwa sauti ya ukali askari huyo alimtaka kila mtu aliyepo ndani ya
mahakama hiyo azime simu yake na shughuli ya mahakama itakapokwisha anyanyuke
kimyakimya na kutoka nje kwa utulivu kama hataki kukutana na nguvu ya jeshi
hilo ambalo waliokuwepo mahakamani hapo jana walishuhudia jinsi lilivyokuwa
limejipanga kukabiriana na raia wasio na hatia waliokwenda kushuhudia
kilichokuwa kikiendelea mahakamani hapo.
Barabara mbili za
kuingilia mahakamani hapo, ile inayotokea hospitali ya mkoa wa Iringa na ile
inayotokea kwa mkuu wa wilaya Iringa zilikuwa zimesheheni askari waliokuwa na
silaha kali, mobomu na magari kadhaa yenye bendera nyekundu likiwemo gari lao
kubwa maarufu kama gari la washawasha.
Wakati wanahabari na
raia wengine waliokuwepo mahakamani hapo wakitii amri ya askari huyo, askari
wenzao hawakutii amri hiyo na simu zao zilipoita hawakuchukuliwa hatua yoyote
ile.
Rais wa Umoja wa Klabu
za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Deo Nsokolo alisema; “Nadhani amri ile
ilikuwa ikiwalenga wanahabari na wananchi wengine waliofika mahakamani hapa. Na
kama ingetokea simu ya mwanahabari ingeita hata kwa bahati mbaya nadhani
pasingetosha.”
Makamu Mwenyekiti wa
Jukwa la Wahariri Tanzania, Deodatus Balile alisema ni kama amri ile ilikuwa
ikiwalenga wanahabari ambao wamekuwa wakipata misukosuko mingi katika kipindi
chote kesi hiyo itakayotolewa hukumu yake kesho Julai 27, ilipokuwa ikifikishwa
mahakamani.
Balile alisema
watahakikisha wanakutana na Inspekta Jenerali wa Polisi na Jaji Kiongozi ili
kuwasilisha malalamiko ya namna shughuli za kimahakama zinavyoingiliwa na
askari Polisi.
Taarifa iliyotolewa na
wanaharakati wa haki za binadamu inaonesha katika maeneo mengine mawakili
wamekuwa wakizuiwa na jeshi la Polisi kufanya kazi zao.(STORI NA PICHA KWA HISANI YA BONGOLEAKS BLOGU)
Post a Comment
Post a Comment