Baadhi ya waumini wa Kiislamu wilaya ya Namtumbo wakishiriki kwa pamoja kulima shamba kwa ajili ya kupanda Ufuta na Mbaazi |
Baadhi ya akina mama wa Kiislamu wakiandaa chakula cha mchana wakiwa shambani wanakoshiriki kwa pamoja kilimo cha Ufuta na Mbaazi. |
WAUMINI wa dini ya Kiislamu wanaofuata Itikadi za Answar na
wale wanaofuata itikadi za BAKWATA wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma wameungana
na kuwa kitu kimoja kwa kulima shamba la Ufuta na Mbaazi ili kujikwamua
kiuchumi.
Waislamu hao kutoka katika msikiti wa Najaat na msikiti wa
Nurullahi yote iliyopo kata ya Rwinga wilayani humo wamejitokeza kwa wingi
kulima shamba lenye ukubwa wa hekari 3 kwa nia ya kulima mazao ya Ufuta na
Mbaazi.
Wakizungumza shambani hapo maimamu wa misikiti hiyo wamesema
kuwa wanaunganishwa na imani ya dini yao na kuweka kando itikadi zao ambazo
hata hivyo haziathiri Umoja wao wa Kiislamu unaolindwa na maneno ya Mwenyezi
Mungu yaliyomo kwenye kitabu cha Koran Tukufu na hadithi za Mtume Muhammad(SAW).
Imamu wa BAKWATA mtaa wa Rwinga Shekhe Juma Nalunya amesema
kuwa wameungana na waislamu wenzao wa msikiti wa Najaat kwa ajili ya kulima
shamba hilo kwa nia yaa kujikwamua kiuchumi na mahitaji mbalimbali
wanayokumbana nayo kila siku.
Naye Imamu wa msikiti wa Najaat uliopo chini ya Taasisi ya
Dhiynurain Sheikh Said Makunguru amesema kuwa awali waislamu wa maeneo hayo
walipandikizwa chuki na kugawanywa makundi kutokana na itikadi na uelewa na
kuwa kwa sasa hali hiyo imeanza kutoweka baada ya kuwepo kwa ushirikiano kwa
kila jambo linalowahusu waislamu.
Amesema kuwa jambo kubwa linalowapaswa waislamu ni
kushikamana katika njia ya Mwenyezi Mungu bila kufarakana kwa kuwa mfarakano
unasababisha waislamu wazidi kudidimia kiuchumi na kifikra.
Kwa upande wake Katibu wa BAKWATA wilaya ya Namtumbo Yassin
Kinonono amesema kuwa ushirikiano uliooneshwa na waumini hawa unapaswa
kuambukizwa katika maenep mengine kwa kuwa kukosekana kwa umoja ndiko
kunakosababisha mgongano na migogoro katika Uislamu.
Amesema kuwa Umoja huu wa waislamu wa kata hii utakuwa ni
mfano kwa waislamu wa wilaya nzima ya Namtumbo na kuwa wao wameonesha njia
nzuri ambayo BAKATWA inapaswa kuwaunga mkono na kutoa elimu ya mshikamano kwa
waislamu wote ili wawe kitu kimoja.
Shamba hilo la hekari tatu lipo katika kijiji cha Migelegele
kata ya Rwinga wilaya ya Namtumbo ambalo
waislamu wamedhamiria kulima mazao ya biashara ya Ufuta na Mbaazi.
Post a Comment
Post a Comment