Ads (728x90)

Mratibu wa michuano ya maadhimisho ya siku ya Kisukari Duniani  Waziri Mohamed Ngwangwa akimuomba katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Juma Malik  Akili kuzikagua timu ya Wizara ya Kazi na Wizara ya Afya katika ufunguzi wa michuano hiyo inayoendelea uwanja wa nje wa Aman Mjini Zanzibar


Kikosi cha Timu ya Wizara ya Afya Zanziabar kabla ya pambano lao la ufunguzi.


Kikosi cha Timu ya Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto.


Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Juma Malik Akili akikagua timu ya Wizara ya Kazi na Wizara ya Afya kabla ya kuanza mechi ya ufunguzi wa mashindano ya maadhimisho ya siku ya kisukari Duniani katika  uwanja wa nje wa Amani mjini Zanzibar.


Na Mwandishi wetu,ZANZIBAR

Timu ya Wizara ya Afya Zanzibar imeyaaga mashindano hayo katika mchezo  wa ufunguzi baada ya kufungwa na timu ya Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na watoto kwa mikwajuni ya penelti katika Uwanja wa nje wa Amani.

Michezo hiyo inayoshirikisha Timu  nane za Wizara za Serikali ya Mapnduzi ya Zanzibar  inachezwa kwa mtindo wa mtoano na fainali itachezwa Novemba 13 mwezi huu, siku moja kabla ya kilele cha maadhimisho hayo yanayofanyika  Novemba 14 ya kila mwaka.

Timu hizo zilimaliza dakika 90 zikiwa zimefungana bao 1-1 mabao yote yakipatikana kipindi cha kwanza . Wizara ya Kazi ilipata bao lake dakika ya 26 kupitia kwa mchezaji wao Ali Seif na  Wizara ya Afya ilisawazisha kwa njia ya penelti iliychongwa na Ahmed Rashid dakika ya 35.

Kipindi cha pili kilianza kwa mashambulizi ya kila upande lakini hakuna timu iliyoweza kuona nyavu za mwenzake huku wachezaji wa timu zote mbili wakikabiliwa na wakati mgumu wa kuanguka mara kwa mara kutokana na utelezi ulisababshwa na mvua kubwa iliyonyesha kwa muda mrefu kabla ya  pambano hilo.

Muda wa penati tano ulipowadia kila timu ilipoteza mbili na hatua ya kupigiana penati moja moja ikaendelea na ndipo wenyeji wakajikuta wanapoteza penelti yao muhimu na kuipa michuano hiyo mkono wa kwaheri.

Akizindua michuano hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Juma Malik Akili alisema lengo la maadhimisho ya siku ya kisukari duniani ni kuunga mkono jitihada za Kimataifa katika kupambana na maradhi hayo yanayoongezeka  kwa kasi duniani kote.

Alisema asilimia 3.7 ya Wazanzibari wanaugua maradhi ya kisukari na wengine wengi wako katika hatari ya kupata maradhi hayo iwapo hawatafanya juhudi za kujikinga.
Hata hivyo alisema tiba kubwa ya maradhi ya kisukari ni  watu kuweka utaratibu wa  kufanya mazoezi na kuweka utaratibu mzuri wa vyakula kwani ndiyo vinavyochangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la maradhi hayo.

Katibu Mkuu aliwashauri wafanyakazi wa Mawizara maidara taasisi za Serikali na binafsi na jamii kwa jumla kuhamasisha katika kufanya mzaoezi na kutenga wakati wa mapumziko ili kuweka mzunguruko mzuri wa damu na kupunguza uzito.

Timu zinazoshiriki michuano hiyo ni Wizara ya Afya, Wizara ya Kazi, Wizara ya Habari, Utalii Utamaduni na Michezo, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Wizara ya Biashara Viwanda na Masoko, Wizara ya Kilimo Maliasili Uvuvi na Mifugo na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

 

Post a Comment

Post a Comment