Mche wa mahindi ulionyauka kwa kukosa mvua eneo la Likonde Namtumbo |
Mkulima Ayubu Makuti wa eneo la Migelegele Namtumbo akiangalia shamba lake la mahindi lililoathiriwa na jua baada ya kukosa mvua kwa wiki tatu |
Mkulima wa Likonde Namtumbo Omari Mangoto akiwa katika shamba lake lililoathiriwa na jua kwa kukosa mvua kwa wiki tatu. |
Wakulima wakipalilia shamba lililoathiriwa na jua katika kijiji cha Migelegele Namtumbo |
-Mazao
yaliyopandwa yaanza kukauka
-Jua kali
launguza mazao, mvua yasimama
Na Rashid
Mkwinda, Namtumbo
HOFU ya
kufikwa na Baa la njaa katika msimu wa mavuno wa 2017 wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma imetanda
miongoni mwa wakulima baada ya jua kali linalowaka kukausha mazao yaliyopandwa
ambayo yalitegemea mvua iliyotarajiwa kuanza kunyesha mwezi Novemba na Disemba
msimu wa kilimo wa 2016-17.
‘’Kipindi
hiki ndicho ambacho mvua hunyesha na kurutubisha mazao yaliyopo mashambani,
mwaka huu mvua imegoma kabisa mazao yanakauka shambani, kuna dalili kubwa ya
njaa msimu huu,’’alisema mkulima mmoja mkazi wa Namtumbo anayelima eneo
yalipokuwa mashamba ya NAFCO aliyejitambulisha kwa jina la Kassim Said.
Alisema kuwa
kwa kipindi cha miaka mingine wakati huu mahindi yangekuwa yamefikia urefu wa
kima cha futi 4’ hadi futi 5’ na baadhi ya maeneo yangekuwa yameanza kuchanua
lakini kutokana na tatizo la mvua hadi sasa mahindi yaliyoanza kuota yamekauka.
Alisema kuwa
kwa mbegu za mahindi za muda mfupi
zinatumia muda wa siku 60 ambapo kwa mvua inayonyesha kuanzia mwezi Novemba
sasa hivi mahindi yangekuwa yameanza kuchanua bali kwa mbegu ya kawaida
inayotumia siku 90 sawa na miezi mitatu kwa sasa ingekuwa imefikia urefu wa
futi 5’.
Kwa upande
wake mkulima Ayubu Makuti(50) mkulima wa kijiji cha Migelegele wilaya ya
Namtumbo alisema kuwa kuna dalili ya njaa mwaka huu kwa kukosa mvua kwa kuwa
yeye alianza kupanda mvua za kwanza zilipoanza kunyesha lakini hadi sasa
mahindi hayajafika hata urefu wa futi 1’ hali ambayo inaashiria madhara katika
msimu huu wa kilimo.
‘’Tuliambiwa
kuwa mvua za kwanza ni za kupandia, watu wamepanda mazao yao mapema, mvua
imegoma kunyesha kinachofuatia baada ya hapa ni njaa, ukifika shambani wakati
wa jua kali mahindi unayaona yakiwa yamenyauka kwa jua,’’alisema Makuti.
Naye mzee
Abedi Parahane(80) mkulima wa kijiji cha Migelegele alisema kuchelewa kwa mvua
kuna madhara makubwa kwa wakulima wa mazao ya mahindi, mpunga na tumbaku na
iwapo haitanyesha hadi ifikapo Januari 10 mwakani wakulima wa Namtumbo
watakumbwa na njaa.
‘’Tulijitahidi
kuwahi kulima kama desturi yetu, tofauti na mwaka jana watu waliwahi kulima na
mvua ilinyesha kwa wakati, unyeshaji wa mvua wa aina hii ni dalili ya njaa’’
alisema Mzee Ali Kilosa(78) mkazi wa kijiji cha Rwinga.
Akizungumza
hivi karibuni katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma
Dkt.Binilith Mahenge, Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Luckiness Amlima aliwataka
wananchi kutouza chakula chote walichovuna msimu uliopita kutokana na
kukosekana kwa mvua ya kutosha msimu huu.
Alisema
kukosekana kwa mvua ya kutosha kunaweza kusababisha kuibuka kwa njaa hivyo ili
kuepuka fedheha hii ya baa la njaa wananchi wanapaswa kutokuwa na tamaa ya
kuuza chakula chote ili kiwasaidie iwapo mvua itaendelea kunyesha kwa kusuasua.
Baadhi ya
maeneo ambayo wananchi wamekuwa wakitoa malalalamiko ya mazao yao kukauka na
jua ni pamoja na Masuguru, Mtonya, Luegu, Litola, Lusewa,Rwinga,
Mandepwende,Likuyu,Mputa na Namtumbo ambako ndiko kunakotegemewa kwa ajili ya
mazao ya chakula na biashara kama vile Mahindi, Mpunga,Tumbaku, Mbaazi na
Ufuta.
Post a Comment
Post a Comment