Tamu ishindayo hamu, si tamu yenye ugumu,
Ni tamu yenye nidhamu, iletayo balaghamu,
Tamu ni tunu adhimu, na ladhaye ni adimu,
Hizi ndo tungo tamu, ziburudivyo uoni.
Zenye utungu si tamu, 'kukari' zaisha hamu,
Tungo zilizo hitimu, ztukuzwa na walimu,
Hutokwa umaamumu,na kutambia kaumu,
Hizi ndo tungo tamu ziburudivyo uoni.
Zilo murua nudhumu,hutakasisha kalamu,
Hu'kari' wenye ilimu, kwa kuchambua muhimu,
Tungo walotaqadamu, fani waliiheshimu,
Hizi ndo tungo tamu,ziburudivyo uoni.
Tungo ziso na nidhamu, fatahize si timamu,
Ni mithali ya sanamu, urari wake hanamu,
wengi wanotunga humu, huteza yalo lazimu,
Hizi ndo tungo tamu. ziburudivyo uoni.
Tungo zenye idghamu, 'amba' zina irhamu,
Hujiweka maalumu,hubezwa na wenda wazimu,
zinaleta ufahamu, na kubeza udhalimu,
Hizi ndo tungo tamu, ziburudivyo uoni.
Tungo tamu ni mwalimu, tungu ni mbovu dawamu,
Betize ni kama sumu, ijapo zatoka humu,
hufarikisha kaumu, insi wakamwaga damu,
Hizi ndo tungo tamu, ziburudivyo uoni.
Kumanya tungu na tamu,kwataka mwenye ilimu,
Wa kupembua magumu,ya guni pamwe nudhumu,
Beti hizi ni salamu, zifike hadi Kisumu,
Hizi ndo tungo tamu, ziburudivyo uoni.
Tamati tungu na tamu, ta'lamidhi na walimu,
Tungo hizi ni adimu, zaja kwenu kwa msimu,
Hima shikeni kalamu, kuyachukua magumu.
Hizi ndo tungo tamu, ziburudivyo uoni.
Wakatabahu.
Ahsante, shairi limetulia kwa kituo.Na lugha unaitumia.
ReplyDelete