Na, Rashid Mkwinda.
KWA muda mrefu kumekuwepo na ushirikiano baina ya vyombo vya dola, waandishi wa habari na wananchi na hivyo kuweka utatu muhimu katika jamii ambayo imekuwa ikihitaji taarifa za uhakika zinazotokea sehemu mbalimbali nchini.
Utatu huu uliopo baina ya dola,waandishi na wananchi umekuwa ukiinufaisha jamii na hivyo kujua kila linaloendelea na kutoa chachu kwa jamii kukosoa ama kutekeleza lile ambalo wakati ule wa ukiritimba wa utoaji na upashaji wa habari vilikuwa ni nadra kujulikana.
Kuwepo kwa vyombo huru vya habari kumechangia kuibua vyombo vingi vya habari, vyuo vingi vya uandishi wa habari sanjari na waandishi wengi wa habari, jambo ambalo linatia faraja ambapo ukifika katika meza ya magazeti unaweza kubabaika kuona takribani magazeti 20 yanayotolewa kila siku yakiwa na habari moto moto zinazosisimua.
Hili limechangia kwa kiasi fulani vigogo ambao hapo awali walikuwa wakijisahau katika mambo yao kuwa waangalifu kutokana na kuzagaa kwa waandishi wa habari kila kona ya nchi,kwa hali hiyo tunaweza kusema kuwepo kwa vyombo vya habari kumechangia kuwarekebisha tabia baadhi ya vigogo.
Ingawa kumekuwa na misukosuko ya baadhi ya vyombo binafsi kupata vitisho kutoka kwa baadhi ya vigogo kiasi cha vigogo hao kutamani kurejea kwa zama zile za ukiritimba wa upatikanaji na upashaji wa habari kwa kulinda maslahi binafsi ikiwa ni pamoja na kuficha maovu yao kiasi cha kutishia kuvifungia baadhi ya vyombo vinavyotishia maslahi yao.
Upashaji wa habari wa zama hizi ni tofauti kabisa na ule upashaji wa habari wa zamani ambapo ni vyombo vichache vilivyokuwa vikiripoti matukio likiwemo gazeti moja la chama tawala, gazeti lililokuwa likimilikiwa na Jumuiya ya wafanyakazi wakati huo JUWATA na moja la serikali ambalo huchapishwa kwa lugha ya kiingereza.
Uchache wa vyombo vya habari wa enzi hizo ulichangia kwa asilimia kubwa kukosekana kwa habari na hivyo kuwa na mazingira ya ukiritimba ambapo ni vigumu kuamini lakini ndio ukweli wenyewe, uwepo wa uhuru wa vyombo vya habari umeleta chachu ya maendeleo kwa kuwa hadi mwanzoni mwa miaka ya tisini nchi yetu ilikuwa kama iko katika karne ya 19 kihabari.
Tulikuwa kama tuko karne ya 19 kutokana na uelewa tuliokuwa nao kihabari,kwa zama zetu za sasa za mfumuko wa vyombo vingi vya habari imefikia hatua hii kujijengea heshima kubwa kama ni moja kati ya mihimili mikuu ya Taifa ambapo wadau mbalimbali wamekuwa wakitoa ushirikiano na sekta hii ikiwa ni pamoja na kutumia vyombo vya habari kujitangazia mambo yao.
Hili limekuwa likifanywa pia na serikali hususan vyombo vya dola ikiwemo Wizara ya mambo ya ndani ya nchi ambayo imekuwa karibu na vyombo vya habari kwa kila hali hususan katika kutoa ama kutangaza mafanikio ya utendaji wa jeshi la Polisi katika vita dhidi ya uhalifu unaotendeka katika jamii.
Tukio lililojiri hivi karibuni Mkoani Mbeya la waandishi wa habari kususia kuandika habari za jeshi la Polisi kutokana na kile kilichodaiwa Kamanda wa Polisi Bw. Suleiman Kova kukosa uaminifu dhidi ya waandishi hao kilikuwa ni cha kusikitisha jambo ambalo lingevuruga utatu muhimu kwa jamii.
Lakini hata hivyo kutokana na jitihada za kidiplomasia za jeshi hilo nchini hususan kwa kuthamini mchango wa vyombo vya habari kwa jeshi hilo na kwa jamii uliagiza makamanda wote wa mikoa kuhakikisha usalama wa waandishi wa habari na mali zao,hili ni jambo kubwa kwa jeshi la Polisi kuwafanyia waandishi nchini ingawa ni wajibu wao kikazi.
Wajibu wa jeshi hilo ni kulinda usalama wa raia na mali zao wakiwemo waandishi wa habari, hivyo kwa kauli hiyo ya kipekee nadhani jeshi hilo litatumia fursa hiyo kwa waandishi kutokana na ukaribu wao kwa jeshi la Polisi kiutendaji ikiwa ni pamoja na kuwaonya baadhi ya watendaji wao wa chini ambao wamewafanya waandishi ni sawa na maadui zao.
Nasema hivi kutokana na uzoefu uliopo baina ya mahusiano ya askari wa ngazi ya chini wa jeshi hilo na waandishi wa habari, nadhani kwa kutofahamu kwao umuhimu wa sekta ya habari katika jamii ama kutokana na wao kuwa ni miongoni mwa wale ambao wanapiga vita vyombo hivyo kutokana na maovu yao wameamua kutumia kofia zao kuwadharau waandishi.
Nadhani kwa hili la uongozi wa jeshi la Polisi nchini kutamka wazi kwamba waandishi wapewe ulinzi na kuhakikishiwa usalama wa maisha yao na mali zao utachukuliwa ni sawa na hatua ya mwanzo ya kurejesha uhusiano mwema wa taaluma hizi za kijamii zinazoshabihiana lakini zinazotofautiana kimtazamo.
Kwa ujumla sakata la waandishi wa habari wa Mkoa wa Mbeya limeamsha hisia mpya kwa jeshi hilo nchini kote ambapo naamini kuanzia sasa,waandishi wataheshimiwa kulingana na maadili na mipaka yao ya kazi kadhalika askari polisi wataheshimiwa kulingana na maadili na mipaka yao ya kazi.
Sidhani kama kuna askari anaweza kudiriki kumtishia Mwandishi wa habari wakati akimhoji kutokana na jambo fulani lililojiri katika jamii kadhalika sidhani kama mwandishi wa habari atasita kutoa ushirikiano kwa jeshi la Polisi kutokana na kile kilichojiri katika jamii kwa kuhofia vitisho vya kiaskari.
Huu ndio utatu na utatuzi muhimu kwa Vyombo vya dola, waandishi wa habari na jamii ambayo jamii inahitaji usalama wao na mali zao kutoka kwa jeshi la Polisi na kuhabarishwa kila kinachotokea katika mazingira na maisha ya kila siku.
Aidha napenda kuchukua fursa hii kumpongeza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya kwa kukiri kwake makosa mbele ya waandishi wa habari na kuweka msimamo wa kukutana mara kwa mara na waandishi kujaribu kubadilishana mawazo na kuondoa tofauti… hicho ndicho ambacho tulichokitarajia.
Kwani aghalabu wakosanao ndio wapatanao na kilichotokea si kukosana kama ilivyodhaniwa na baadhi ya watu, bali ilikuwa ni kujenga heshima ya kila mmoja kwa nafasi yake ikiwa ni pamoja na kuwekana sawa kutokana na hitilafu zilizotokea ambazo ziligusa maisha ya watu.
Msimamo wa Kamanda Kova kutokana na hili ni wa kuigwa, kwani ameonesha upeo mkubwa na uelewa mpana juu ya kile kilichowatokea waandishi wa habari na kwamba huo ndio uungwana na mara nyingi ‘muungwana akivuliwa nguo huchutama’ kuficha aibu yake.
Kikao cha waandishi wa habari wapatao 30 wa jiji la Mbeya na Kamanda Kova kimeonesha ni namna gani jeshi hilo lina kila dalili ya kuthamini mchango wa wanahabari na hivyo kutoa chachu ya viongozi wengine wa juu kuthamini kazi za waandishi wa habari nchini.
Kwa upande wa waandishi wa habari, tatizo hili liwe ni fundisho kwa kulinda na kuzingatia maadili ya kazi ipasavyo na kujitambua kwamba kuwepo kwao katika jamii ni muhimu kwa maslahi ya wananchi na taaluma yao ya habari.
WAKATABAHU.
Karibu sana bwana Mkwinda.
ReplyDeleteMakala yako ya utatu iko fresh sana ila napenda niseme machache juu yake.
1.Ninaandika kutoka Uganda, nchi iliyojaa udikteta haswa ukilinganisha mataifa matatu ya afrika mashariki.
Nataka tu nikwambie kitendo cha waandishi kugoma kuandika habari ni sawa na hongo juu ya walengwa au wahusika wa habari ile.Napata picha kwamba waandishi wetu hawataandika habari ya kukosoa jeshi la polisi kwani wamewekeana mkataba wa utatu ni hatari kwa habari zenye kujenga hazitakaa ziandikwe.
2.Vyombo vya habari ni sawa na jeshi la polisi lakini kumbuka vyombo vya habari ni askari wenye kutumia kalamu dhidi ya maovu katika jamii. Nani asiyejua kwamba jeshi la polisi ni kati ya wala rushwa wakubwa.Sasa kama waandishi wetu wanawekeana mikataba na polisi hii ni hatari sana.
3.Hapa Uganda vyombo vya habari havigomi ila vinapambana kuandika habari kwa kuchunguza sio kutegemea kwenda maofisini kuwahoji viongozi manake wao watatoa taarifa za upande mmoja tu.
Ndio maana sishangai Tanzania kuna magazeti mengi na redio na TV nyingi sana lakini ukiangalia ni habari za kusifia viongozi hakuna michezo michafu kuanikwa hadharani, ni mara chache sana.
Mwisho sisemi kwamba waandishi kazi yao ni kufichua maovu tu ila huu utatu wa waandishi sio habari njema.Kwa mfano siku kadhaa zilizopita waandishi waligombana na jeshi la magereza na wakatishia eti hawataandika habari nzuri za jeshi la magereza. Hii ilidhihirisha kumbe wanaficha maovu na wanasubiri watawala wakosane nao. Unaonaje hili?
TUMEKWISHA KWA HAYA