Pichani ni Alhaj Ali Hassan Mwinyi(rais mstaafu awamu ya pili na Sheikh Gorogosi mwenye miwani) wakiwa katika moja ya ibada za swala ya ijumaa(picha kwa hisani ya JAMII FORUM)
Namkumbuka Sheikh Suleiman Gorogosi (pichani juu mwenye miwani)akiwa na Rais Mstaafu wa awamu ya Pili Alhaj Ali Hassan Mwinyi katika moja ya ibada za swala ya Ijumaa jijini Dar es salaam), Sheikh Gorogosi ambaye amefariki kwa ajali mkoani Mtwara jana alasiri akitokea jijini Dar es salaam,kama walivyo masheikh wengi alikuwa na msimamo barabara wa kuimarisha imani ya kiislamu kwa itikadi alizoamini ndizo zinazostahili kwa mtazamo wa waumini wa dini ya kiislamu nchini Tanzania.
Alikuwa ni miongoni mwa masheikh wenye mtazamo wa KIBAKWATA hususani katika hitilafu mbalimbali ambazo hutokea baina ya waislamu, mathalani kuhusu mwandamo wa Mwezi wakati wa Ibada ya saum ya Ramadhan na Ibada ya Sunna ya Hijja.Alisimamia mtazamo wake wa kupinga wale wasio kuwa na msimamo kama wake juu ya suala hili ambalo kwa miaka mingio masheikh na wanazuoni wakubwa wa kiislamu wamekuwa wakiweka midahalo na kujadili hatima ya hitilafu hizi zinazotokea.
Sheikh Gorogosi alikuwa ni miongoni mwa waumini wakuu wa itikadi ya Kadiria ambao huwa na msimamo wa kusimamia jambo katika namna ya utekelezaji wa ibada jambo ambalo hupingwa na watu walio na msimamo tofauti, Namkumbuka pia Sheikh huyu mzaliwa wa mkoani Lindi na Sheikh mkuu wa mkoa huo kwamba alikuwa ni miongoni mwa masheikh lukuki waliojiotokeza kuwania nafasi ya Mufti mkuu wa Tanzania mara baada ya kufariki dunia kwa aliyekuwa Mufti wa Tanzania Sheikh Hemed Bin Jumaa Bin Hemed na baadaye Sheikh Issa Bin Shaaban Bin Simba hatimaye akawa ni Mufti mkuu wa Tanzania(BAKWATA).
Alikuwa ni miongoni mwa masheikh waliokuwa na msimamo ndani ya Baraza hata kuna wakati aliwahi kuondoka katika nafasi ya uongozi wa Baraza hilo kutokana na mgogoro wa ndani wa Baraza ambapo baadaye alirejea tena na kuwa Kaimu Mufti Mkuu (BAKWATA).
Watazungumza mengi juu ya kifo chake hususani katika kipindi hiki ambacho kila mtu ametanguliza mbele maslahi binafsi katika sekta mbalimbali za uongozi iwe katika medani za kisiasa na hata kidini ila jambo moja linalopaswa kuelezewa hapa ni kwamba Sheikh Gorogosi ahadi yake imetimia na siku zake zimehesabika na huo ndio mwisho wake, hatuwezi kumtia tena machoni mwetu.
INNA LILLAHI WAINNA ILAYHI RAJIUWNA!!!sisi sote tumetoka kwa Mwenyezi Mungu na Marejeo yetu ni kwake.
Post a Comment
Post a Comment