Ads (728x90)



HISIA TOFAUTI ZAGUBIKA KIFO CHA KANALI MOAMMAR EL GHADHAFI
Anatajwa kuwa shujaa aliyetetea maisha ya wananchi wa Libya!,anatajwa kuwa kiongozi shupavu aliyelinda rasilimali za wananchi wa Libya!! anatajwa kuwa ni kiongozi aliyejali maisha ya wananchi wa hali ya chini! anatajwa kuwa ni Dikteta na muuaji aliyesababisha vifo vya wananchi wa Libya.
Ni sura mbili za rais wa zamani wa Libya  ni Kanali Moammar  El Ghadhafi ambapo taarifa za namna  kifo chake kilivyokuwa zinahitilafiana huku zingine zikieleza kuwa ameuawa na mashambulizi ya angani ya majeshi ya NATO na zingine zikieleza ameuawa wakati akitoroka na msafara wake kupitia mtaro wa shimo la takataka Jijini Sirte mahala alipozaliwa.


Taarifa za kuhitilifiana zinaeleza kuwa aliuawa baada ya kukamatwa wakati kitaka kutoroka na msafara wake akiwa ndani ya mtaro wa shimo la takataka katika Jiji la Sirte mahala alipozaliwa Ghadhafi na kuuawa kwa kupigwa risasi huku taarifa zingine zikielezwa kuwa aliuawa kwa kushambuliwa msafara wake ukiwa angani na majeshi ya NATO.
Inaelezwa kuwa sababu za kifo chake zinatokana na majeraha makubwa ya risasi yaliyokuwepo kichwani na miguuni ambapo alifariki akiwa ndani ya gari wakati akikimbizwa katika hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Kifo chake kinaelezwa kuwa ni utabiri wake alioufanya miaka mitatu iliyopita ambapo pia aliahidi kupigana hadi tone la mwisho la damu yake kwa ajili ya kuihami nchi yake dhidi ya watu aliowataja kuwa ni maharamia wa nchi za Magharibi, Hata hivyo pamoja na mashambulizi makali ya majeshi ya NATO dhidi yake hakuthubutu kuikimbia nchi yake ingawa alikuwa na fursa ya kufanya hivyo.



Baadhi ya wanafamilia wake akiwemo mkewe na wanawe waliondoka nchini Libya mapema na kwenda kuishi Uhamishoni nchini Algeria bali yeye na mwanaye Motas Ghadhafi ambaye anaelezwa kupigwa risasi na kujeruhiwa kichwani na kuvunjwa fuvu lake kwa risasi walisalia Jijini Sirte kwa ahadi ile ile ya kuoigana hadi tone la mwisho la damu yake akitetea nchi yake kutovamiwa na mabeberu wa Kimagharibi.

Mwanaye Motas aliuawa pamoja na babaye kwa kupigwa mkono wake wa kuume na baadaye kushambuliwa risasi mfululizo mgongoni zilizosababisha kupoteza maisha yake.
Kifo cha Ghadhafi aliyeongoza nchi hiyo kwa miaka 42 kinaelezwa na Waziri Mkuu wa serikali ya Mpito ya Libya Bw. Mohamed Jibril kuwa alikamatwa akiwa mzima wa afya huku akiwa amevalia singlend na suruali ya kawaida akiwa na silaha yake mkononi,wapiganaji watiifu wa Ghadhafi walianza mashambulizi na wapiganaji wa serikali ya Mpito ya Libya.
Bw.Jibril anaeleza kuwa katika mapigano hayo alilengwa risasi ya mkono wa kuume na risasi kichwani iliyomjeruhi na kufa baadaye wakati akipelekwa hospitali.
Kifo cha Ghadhafi kinaelezwa kuwa ni mwanzo wa machafuko katika nchi hiyo huku marafiki wa kiongozi huyo ambao ni nchi za Afrika zikiwa zimenyamaza kutotoa tamko lolote kwa kile kilichoelezwa kuwa ni hofu ya uvamizi kutoka nchi ya Marekani.
Utawala wa Ghadhafi ambao ulijaa mbwembwe na vituko vya hapa na pale alipokuwa akitembelea baadhi ya nchi za Afrika umeacha historia ya kukumbukwa huku walinzi wake wasichana Bikra walioelezwa kuwa ni warembo kupindukia wakiacha gumzo kila mahala alipotembelea kiongozi huyo.
Ghadhafi alizoea kutembea na hema lake na kukaa chini akikoka moto wa kuni na kufanya mazungumzo huku akiburudika kwa kunywa kahawa na viongozi wenzie wa Afrika kama vile Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania.
Alitamani siku moja nchi za Afrika zingeweza kuwa nchi moja na kuunda Muungano wa nchi hizo yaani United State Of Africa (USA) hali ambayo inaelezwa kutishia utawala wa Marekani hata kusababisha kuibuliwa kwa chuki dhidi yake kutoka nchini Marekani.
Kifo hicho cha Kanali Ghadhafi kinaelezwa kuwa ni pigo kwa wanachi walionufaika na utawala wake kama anavyoeleza Dkt.Peter Mtasigwa aliyewahi kuwa Mwalimu nchini Libya ambaye alirejea nchini miezi miwili iliyopita aliyesema kuwa tatizo la uchumi na maisha ya wananchi wa Libya litasababisha kumkumbuka.
Alisema kuwa wananchi wa Libya walikuwa wakinufaika kwa rasilimali za nchi yao huku umeme na maji wakilipia kwa gharama ndogo na mara nyingine kutolipia kabisa na kuwa utawala mgeni unaweza kusababisha mdororo wa kiuchumi kutokana na mtazamo mpya wa serikali mpya ya nchi hiyo.
Kanali Ghadhafi pia atakumbukwa namna alivyoweza kuenzi Maisha ya vijana wengi wa Libya ambao walipata fursa ya kupatiwa mitaji ya kuanzia maisha mara wanapofikia umri wa kuoa ikiwa ni pamoja na kupatiwa vyombo vya usafiri na makazi mazuri, Waliishi kama peponi.
Nchini Uganda Kanali Ghadhafi atakumbukwa kwa kudumisha urafiki na nchi hiyo tangu enzi za utawala wa Idd Amin Dada na baadaye Yoweri Museveni ambapo ipo kumbukumbu ya msikiti mkubwa maarufu kwa jina la msikiti wa Ghadhafi na chuo huku kukiwa na barabara na mtaa maalumu uliopewa heshima ya jina la kiongozi huyo.
Kufuatia kifo cha Kiongozi huyo baadhi ya miji ya nchini Libya wananchi wameibuka kwa furaha shangwe na vifijo wakipiga risasi juu kwa furaha,honi za magari barabarani na meli bandarini zikihanikiza maeneo mengi nchini humo huku baadhi ya wananchi  wakielezea kuwa utawala wa Libya ulisababisha waishi katika maisha ya dhiki kwa kipindi chote.
Mtazamo wake kwa baadhi ya viongozi wa Afrika Kanali Ghadhafi alimkubali sana rais wa Zimbabwe kutokana na msimamo wake dhidi ya watu wa nchi za Magharibi waliodaiwa kuwa ni mabeberu wanaoeneza ubeberu wao katika nchi zenye manufaa na ustawi wa jamii.
Aidha mtazamo wa baadhi ya wachambuzi wengi ni kuwa kifo cha Kanali Ghadhafi kimeanzisha mgogoro mpya na vita visivyomalizika ndani ya nchi hiyo.
Mhadhiri wa chuo cha Kiislamu cha Morogoro (Mmum) Jafar Siraji anaelezea kuwa kifo cha Kanali Ghadhafi kimefanyika ili kuuendeleza ubeberu dhidi ya nchi zenye mafanikio ya kiuchumi na kuwa huo ni mwanzo wa mgogoro usioisha kwa nchi hiyo.
Kwa upande mwingine baadhi ya watu wanaelezea kuwa hawapaswi kuamini moja kwa moja kuhusiana na kifo hicho kwa kuwa upo uwezekano wa propapaganda za nchi za kimagharibi kuhusiana na kifo hicho jambo ambalo linafanywa makusudi kuvuruga mahusiano.
(HABARI KWA MSAADA WA VYANZO MBALIMBALI VYA NDANI NA NJE)

Post a Comment

Post a Comment