Dkt.Shein
aridhia mchango wa WHO
Na Mwandishi Maalumu, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Ali Mohamed Shein amesema Shirika la Afya Duniani (WHO),limekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha sekta ya afya nchini hatua ambazo zimeweza kusaidia kupambana na maradhi kadhaa yakiwemo Malaria.
Dkt.Shein alisema, mbali na WHO kuwa na historia ya muda mrefu ya kuiunga mkono Zanzibar katika sekta ya afya pia imekuwa ni mdau mkubwa wa kuiasaidia Zanzibar katika sekta ya afya kwa kuwajengea uwezo madaktari kupitia uwezeshwaji wa mafunzo mbalimbali.
Hayo aliyasema jana Ikulu mjini Zanzibar wakati akifanya mazungumzo na, Dkt.Rufaro Chatora ambaye ni Mwakilishi Mkazi wa WHO nchini Tanzania akiwa amefuatana na Ofisa Ushirikiano wa shirika hilo, Dkt.Pierre Kahozi Sangwa anaefanyia kazi zake mjini Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo, Dkt.Shein alimueleza Mwakilishi huyo wa WHO nchini Tanzania kuwa, Zanzibar imekuwa ikipata ushirikiano na misaada mbalimbali kutoka shirika hilo ambayo imeweza kusaidia katika kuimarisha sekta ya afya sanjari na kuwajengea uwezo wafanyakazi wa sekta hiyo.
Alieleza kuwa Zanzibar imeweza kupata ushirikiano mzuri kutoka shirika hilo kwa miaka mingi ikiwa ni pamoja na kuungwa mkono katika mradi wa mwanzo dhidi ya kupambana na Malaria hatua ambayo imewasaidia kwa kiasi kikubwa.
Alieleza kuwa mafunzo kwa madaktari yatasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha sekta ya afya nchini na kueleza kuwa Serikali itaweka mipango madhubuti ya kutoa mafunzo kwa madaktari wake.
Rais Shein alitoa pongezi kwa shirika hilo pamoja na Serikali ya Marekani katika kusaidia kuiunga mkono Zanzibar katika mapambano dhidi ya Malaria.
Alisema, shirika hilo limeweza kusaidia katika utoaji wa mafunzo kwa madaktari kadhaa wa Zanzibar kwa kuweza kuwadhamini katika masomo yao ambapo baada ya kurudi wameweza kufanya kazi vyema nchini.
Alieleza kuwa kipaumbele zaidi hivi sasa kimewekwa katika kuwapatia mafunzo
madaktari hapa nchini hivyo uungaji mkono wa shirika hilo katika jambo hilo
kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha sekta ya afya.
Dkt.Shein alieleza kuwa wengi waliopata nafasi hizo za masomo kupitia WHO wameweza kuisaidia sekta hiyo kwa kiasi kikubwa na kuweza kutoa huduma ya afya katika kada kadhaa ikiwa ni pamoja na kupunguza vifo vya akina mama na watoto.
Katika maelezo yake pia, Dkt.Shein alimueleza mwakilishi huyo kuwa wananchi walio wengi hapa nchini wamepata mwamko wa kupambana na Malaria na wamekuwa wakichukua juhudi kubwa za kujikinga licha ya juhudi zinazochukuliwa na Wizara.
Kutokana na hatua hiyo Dk.Shein alisema, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara yake ya Afya itaendelea kuthamini na kutambua umhimu mkubwa WHO katika kuimarisha sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kuimarisha uwanachama wake ndani ya shirika hilo.
Naye Mwakilishi wa Shirika hilo Tanzania, Dkt.Rufaro Chatora, alimueleza Dkt.Shein kuwa WHO litaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya kwa kutambua juhudi kubwa inazozichukua katika kuimarisha sekta hiyo.
Dkt.Chatora alimueleza Rais kuwa WHO inatambua juhudi za Zanzibar katika
kupambana na maradhi mbalimbali na kutoa pongezi kwa hatua ilizozichukua katika kupambana na maradhi ya Malaria na kupelekea Zanzibar kuwa mfano wa kuigwa katika nchini zilizopo chini ya Jagwa la Sahara.
Kutokana na juhudi hizo mwakilishi huyo alitoa pongezi kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya uongozi wa Dkt. Shein katika kufikia hatua hiyo na kusifu sera na mikakati iliyowekwa katika kuimarisha sekta ya afya nchini.
Mwakilishi huyo alimueleza Dkt.Shein kuwa WHO imeridhishwa na hatua za Serikali katika kuimarisha sekta hiyo na kusifu mikakati yake ya kupamba na maradhi sugu.
Awali Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Mohamed Jidawi akiwatambulisha wageni hao kwa Rais, alieleza kuwa WHO ni miongoni mwa shirika la Umoja wa Mataifa ambalo limekuwa likitoa ushirikiano mzuri katika sekta ya afya nchini.
CHANZO; GAZETI LA MAJIRA
Post a Comment
Post a Comment