Mkurugenzi Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Ananilea Nkya |
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Blandina Nyoni |
Daktari Mkuu wa Serikali Dkt. Deogratias Mtasiwa |
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt.Hadji Mponda |
Dar es salaam.
SAKATA la mgomo wa madaktari limezidi kuchukua sura mpya
baada ya wanaharakati kutoka asasi 12 zisizo za kiserikali kufunga barabara
katika Jiji la Dar es Salaam wakishinikiza Serikali imalize mgomo huo haraka
ili kuokoa mamia ya Watanzania kuendelea kupoteza maisha.
Tukio hilo
lilitokea jana jijini baada ya wanaharakati zaidi ya 60 kuzuia magari
katikamakutano ya barabara za Ally Hassan Mwinyi na Ocean Road karibu na daraja la
Salender.
Wanaharakati walifunga barabara katika eneo hilo
kuanzia saa 8 mchana ambapo shinikizo hilo
lilidumu kwa muda wa saa 1 na kusababisha adha kubwa kwa watumiaji wa barabara
hizo.
Walikuwa na mabango yenye ujumbe tofauti huku wakidai lengo
lao ni kuishinikiza Serikali kumaliza mgomo huo kwa kukaa meza moja na
madaktari ili kuokoa roho za Watanzania zinazopotea bila kuwa na hatia.
Baadhi ya mabango waliokuwa wamebeba wanaharakati yalionesha
kusikitishwa jinsi Serikali inavyoshughulikia suala hilo na kuwataka viongozi wote wakuu
wanaongoza Wizara ya Afya wawajibishwe kwa kufukuzwa kazi.
Akizungumza katika eneo la tukio kwa niaba ya wanaharakati
hao, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania(TAMWA),
Ananilea Nkya, alisema wameamua kufanya hivyo ili kufikisha ujumbe kwa
Serikali.
Nkya alisema haiwezekani Serikali kukaa kimya wakati
wananchi wanakufa na kuongeza mgomo huo ni janga linahitaji kutafutiwa ufumbuzi
wa haraka ili madaktari warejee kazini.
Mkurugenzi alisema wanaharakati hao baada ya kuona
hatua ambazo zinafanyika katika kushughulikia mgomo huo waliamua kuwasiliana
kwa kutumia njia ya simu hadi wakafika na kufunga barabara ili ujumbe wao
ufike.
Alisema hatua waliyofanya haikuwa ya kufanya vurugu ndiyo
maana Polisi walipofika eneo hilo
hawakuwafanya lolote zaidi ya kukaa pembeni.
Nkya alisisitiza kukerwa na namna mgomo huo
unavyoshughulikiwa na Serikali na kubainisha kama hakutakuwa na mazungumzo ya
kumaliza tatizo hilo
watakwenda Ikulu kwa nia njema hadi upatiwe ufumbuzi.
" Hatufanyi vurugu ya aina yoyote hapa tulipo, tumeamua
kufunga barabara kwa saa moja na baada ya hapo tutaondoka kwani ujumbe wetu
utakuwa umefika kwa Serikali.
Wanaharakati tunataka kuona suala hili linapatiweufumbuzi na
kumalizika haraka.
" Tunamshangaa Spika wa Bunge, Anne Makinda ambaye yeye
ni mwanamke na anatambua matatizo ya wanawake lakini anaona suala la kufa kwa
Mtanzania si jambo la dharura.|Amekataa wabunge wasijadili suala la mgomo wa
madaktari, tumeshindwa kumuelewa," alisema Nkya.
Nkya alihoji ingekuwaje kama
ni vita halafu Mtanzania mmoja amekufa Serikali ingeendelea kukaa kimya? na
kubainisha kuwa maisha ya Watanzania ni muhimu kuliko kitu chochote kile.
Aliongeza kuwa Serikali inatakiwa kutambua kuwa uhai wa
Mtanzania ukiondoka hakuna anayeweza kuurudisha na kwamba wanaharakati
hawatakaa kimya wakati maisha ya wananchi yapo hatarini.
STORI KWA HISANI YA DOTTO MWAIBALE
Post a Comment
Post a Comment