Ads (728x90)


 
WAKATI Serikali ikiendelea kupambana ili madaktari waache mgomo wao, hali bado ni tete katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kutokana na hospitali hiyo kugoma kupokea wagonjwa wapya.


MWANAFASIHI lilishuhudia jana wagonjwa hasa wajawazito wakikataliwa kwa madai kuwa hakuna madaktari, hivyo warejee katika hospitali zilizo karibu na maeneo yao.


Hali ni mbaya zaidi katika wodi ya watoto ambao wamezaliwa chini ya muda wao 'njiti' wakihitaji kuwa chini ya uangalizi wa madaktari.


Kutokana na hali hiyo, watoto watano waliokuwa kwenye uangalizi maalumu wanadaiwa kupoteza maisha juzi na idadi hiyo itaongezeka endapo mgomo huo utaendelea.


Ili kuonesha mgomo huo ulivyo tete, juzi saa 6 usiku Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda, Naibu Waziri Lucy Nkya, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Blandina Nyoni, Mganga Mkuu wa Serikali, Deo Mtasiwa na viongozi wengine walifika hospitali hapo kuona huduma zinavyoendelea.


Imeelzewa kuwa baada ya kuingia wodi ya wazazi walipokelewa na kelele za wajawazito hao ambao walilalamikia kudorora kwa matibabu kutokana na makali ya mgomo huo.


Akizungumza na MWANAFASIHI kwa sharti la kutotajwa jina lake, mmoja wa wauguzi wa wodi hiyo alisema hali bado si nzuri na kwamba ni Dk. Kamugisha pekee ndiye anayefanya kazi baada ya wengine kugoma.


"Dk. Kamugisha Mungu aendelee kumsaidia kwani ndiye pekee anayefanya kazi akisaidiana na sisi wauguzi ambao tumeambiwa tutoe huduma kwa wagonjwa waliopo wodini pasipo kuwapokea wa nje,'' alisema muuguzi huyo.


Alisema hali inatisha kwenye wodi ya watoto njiti kwani ni kama wametelekezwa bila msaada na si wauguzi wote wanaoweza kuwaangalia kutokana na hali zao zilivyo.


Mjamzito, Rehema Ali mkazi wa Kiwalani, alisema jana alikuwa afanyiwe upasuaji wa uzazi katika hospitali hiyo na daktari wake aliyemtaja kwa jina la Kapona, lakini hakupokelewa kutokana na mgomo unaoendelea.


"Dokta wangu Kapona aliniambia siwezi kufanyiwa upasuaji hivyo aliniambia niende Hospitali ya Mwananyamala ambapo nitafanyiwa upasuaji huo leo,'' alisema.


Katika hatua nyingine, Mwandishi Wetu aliyekuwepo eneo la mapokezi katika wodi hiyo ya wazazi jana asubuhi alishuhudia mjamzito Ashura Kazeba akikataliwa kupokelewa hospitalini hapo kwa madai kwamba hakuna huduma.


Mjamzito huyo alinusuriwa na Dk. Kamugisha baada ya kuambiwa alizuiliwa ambapo alifika mapokezi na kuanza kuwafokea wauguzi waliokuwepo na kuamuru wampeleke wodini.


"Nani amemzuia mama huyu asipokelewe, mnamrudisha nyumbani kwa agizo la nani? Mwandikisheni na kisha mpelekeni wodini tusiharibiane kazi,'' alisema Dk. Kamgisha kwa kufoka.


Meneja Uhusiano wa hospitali hiyo, Aminiel Aligaesha akizungumza na waandishi wa habari jana alikiri madaktari bingwa wa hospitali hiyo kuazimia kusitisha huduma za matibabu mpaka hapo Serikali itakapotoa tamko rasmi kuhusu muafaka wa suala hilo.


Alisema wagonjwa waliopo wodini wataendelea kuangaliwa na madaktari wakuu wa idara na madaktari wachache waliojitolea na kuwa madaktari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania wataendelea kuwaona wagonjwa kwa dharura.


Akifafanua juu ya kufukuzwa kwa wagonjwa, alisema kwamba hakuna mgonjwa aliyefukuzwa kama ilivyodaiwa na vyombo vya habari kwani juzi takwimu zinaonesha wagonjwa 811 walipokelewa hospitalini hapo.


Alisema huduma za uuguzi zinaendelea kama kawaida na wanatoa shukurani kwa wauguzi wanaoendelea na kazi katika kipindi hiki cha mgomo.


Katika muendelezo wa matukio ya mgomo huo wa madaktari imeelezwa vifo katika Hospitali ya Temeke vimeongezea hasa kwa wagonjwa waliowapeleka hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kukataliwa.


"Tunasikitika kuona wagonjwa tunaowawapeleka Muhimbili kwa matibabu wakikataliwa kupokelewa na badala yake tunarudishiwa na matokeo yake karibu wote waliorudishwa wamepoteza maisha,'' alidai mmoja wa wauguzi wa hospitali hiyo.


Kutokana na hali hiyo, kwa masaa kadhaa madaktari na wauguzi walisimamisha kutoa huduma kwa muda ili kujua hatima ya suala hilo na kufanya wagonjwa kurejea nyumbani.


Mwandishi wetu aliyefika hospitalini hapo alishuhudia madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo wakiwa kwenye mkutano wa dharura katika moja ya chumba katika ofisi ya Mganga Mkuu.


Hata hivyo, baada ya kikao hicho walionekana kurudi katika maeneo yao ya kazi na kuendelea kutoa huduma. Jitihada za kuonana  na Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Amani Malima ili kuzungumzia suala hilo hazikuzaa matunda baada ya mwandishi wetu kumpigia simu na kujibiwa kuwa aende ofisini na alipofika Katibu Muhtasi wake alisema yupo na wageni.

STORI NA PICHA KWA HISANI YA DOTTO MWAIBALE

Post a Comment

Post a Comment