Ads (728x90)

WAZIRI wa Mambo ya Ndani Bw.Shamsi Vuai Nahodha amekumbana na zahama ya kuzomewa kutoka kwa kundi la watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA alipofanya ziara yake ya kichama katika mji mdogo wa Tunduma mkoani Mbeya.
Zomea zomea hiyo iliibuka mara msafara wa Waziri Nahodha ulipofika eneo maarufu la biashara kwa vijana wanaobadilisha fedha za kigeni ambapo kundi la vijana waliosimama pande mbili za barabara kuu iendayo Sumbawanga walianza kupiga mayowe na kuuzomea msafara huo.
Sauti za vijana hao zilisikika zikihanikiza hewani zikisema, ‘’ aache kutumia rasilimali za serikali kwa shughuli za CCM..hilo ni jasho la walipa kodi,’’
Wakati kundi hilo la vijana likizomea mmoja wa vijana ambaye hakutambulika jina lake alijikuta katika wakati mgumu wa kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi na vijana wa Green Guard kwa madai kuwa wakati akizomea alikuwa akitaka kurushia mawe msafara huo.
Kijana huyo ambaye hakuweza kupatikana jina lake alichezea mkong’oto kutoka kwa vijana Green Guard na askari ambao walijichanganya katika kundi la vijana wa CHADEMA ambao walikuwa wakipeperusha bendera za chama chao.



Akizungumza wakati akimkaribisha Waziri Nahodha ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa CCM,Mwenyekiti wa CCM kata ya Tunduma Bw. Daniel Mwashiuya alisema kuwa kuna kundi la watu wachache ambao wamejipanga kuvuruga amani katika mji huo kwa kisingizio cha siasa.
Bw. Mwashiuya alisema kuwa CCM iko imara katika kukabiliana na vurugu hizo ambazo zinatishia amani na utulivu wa watu na mali zao.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na kundi la wanachama wa CCM Bw.Nahodha alisema kuwa amejionea mwenyeqwe hali ya uvunjifu wa amani na kwamba kwa kuwa yeye ndiye Waziri mwenye dhamana ya ulinzi wa wananchi na mali zao hawezi kufumbia macho ambapo alimuagiza Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya kushughulikia hali hiyo ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku biashara haramu eneo hilo.
Tukio la aina hii katika eneo hilo ni la tatu ambapo tukio la kwanza lilikuwa ni wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2009 uliolazimika kubadilisha njia wakati yalipotokea mauaji ya mfanyabiashara wa mjini Tunduma ambapo mtu wa tatu kukutana na zahama ya kuzomewa alikuwa ni mke wa Rais Mama Salma Kikwete ambaye alikuwa katika ziara ya kampeni za uchaguzi mwaka 2010.

Post a Comment

Post a Comment