Ads (728x90)


Na, MwanaFasihi Wetu Mbozi

SHEREHE za kuukaribisha mwaka mpya 2012 zilizoenda sanjari na maadhimisho ya siku ya Mwanamke zilizoandaliwa na Taasisi isiyo ya kiserikali ya Wanawake wilayani Mbozi (WADF Mbozi) iliingia dosari mwishoni mwa wiki baada ya mgeni rasmi aliyealikwa kujisaidia haja ndogo ukumbini.

Sherehe hizo ambazo zimefanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa Kanisa katoliki wa ‘Mkonongo’ ziliwahusisha viongozi mbalimbali wa chama tawala na serikali ambapo Mgeni rasmi aliingia ukumbini humo huku akiwa amelewa chakari akiwa amevaa suruali aina ya Cool Dry.

Kiongozi huyo wa juu serikalini aliyeonekana akiwa na dalili za kupata kilevi aliingia ukumbini majira ya saa 1:30 na kupita moja kwa moja kwenye meza kuu na kuungana na viongozi wengine waliokuwa wakiendelea kufurahia sherehe hiyo ya akina mama.

Muda mfupi baadaye kiongozi huyo alionekana akiwashika shika akina mama walioketi meza kuu sehemu mbalimbali za miili yao na kusababisha kero miongoni mwa waalikwa wa sherehe hizo ambapo baadaye alisimama kwa ajili ya kuelekea msalani huku eneo aliloketi likiwa limelowa maji.

Bwana mkubwa kabla hajafika katika mlango wa kuelekea msalani alijikuta akimalizia haja zake aliposimama na kuongeza ubichibichi katika suruali yake aliyovaa huku baadhi ya viongozi walioketi meza kuu wakitaharuki kuona namna ambavyo mwakilishi huyo wa wilaya akiwa katika hali ya ajabu.

Baadhi ya waalikwa na viongozi wengine wa serikali na chama tawala walistaajabishwa na kitendo cha kiongozi huyo na kujikuta wakifumba macho kwani kila hatua aliyotembea iliacha alama za maji maji yaliyendelea kuchuruzika katika suruali yake na kufanya ukumbi mzima kushika tama kutokana na heshima aliyokuwa nayo kwa wananchi kiongozi huyo.

Wakizungumzia tukio hilo baadhi ya wananchi waliohudhuria sherehe hizo walisema kuwa tabia za kiongozi huyo zimewatia aibu wanawake waliomualika na kuwa hafai kuwa kiongozi kwani ameonesha dalili za utovu wa nidhamu na kutojiheshimu.

Akizungumzia lengo la sherehe hizo Mratibu wa taasisi hiyo ya wanawake wilayani Mbozi Bi. Happiness Kwilabya alisema kuwa waliamua kufanya sherehe hizo ikiwa hitimisho la shughuli mbalimbali za kijamii ambazo wamekuwa wakizifanya tangu mwaka mpya uanze.

Alisema kuwa awali walitembelea vituo mbalimbali vya kulelea watoto yatima na kula nao chakula,walifanya shughuli mbalimbali za usafi katika maeneo ya huduma za kijamii ikiwemo hospitali ya wilaya ya Mbozi pamoja na kuwatembelea wagonjwa na kuwapa matumaini.

Post a Comment

Post a Comment