Wabunge 70 wa CCM wanajiandaa kuvua Gamba ili wavae Magwanda?
MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema kuna zaidi ya
wabunge 70 kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), wameomba kujiunga na chama
hicho cha upinzani.
Akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika kwenye Viwanja vya
NMC, Unga Ltd, jijini Arusha jana, Mbowe alisema katika orodha hiyo,
wamo mawaziri saba waliotajwa katika Baraza lililotangazwa juzi na RaisJakaya Kikwete.
“Sasa wanaowataja akina Ole Millya, Bananga na wengine watashangaa kusikia orodha na majina ya wana CCM watakaojiunga Chadema,” alisema Mbowe.
Alitumia mkutano huo kuwatoa hofu wana Chadema wanaotilia shaka wimbi la viongozi na wana CCM wanaojiengua na kujiunga na chama hicho kikuu cha upinzani kuwa Chadema iko imara na hakiwezi kuhujumiwa wala kupenyezewa mamluki kama baadhi wanavyodhani.
Mbowe alitamba kuwa ameongoza harakati za upinzani kwa zaidi ya miaka
20 sasa ambayo imeanza kuzaa matunda kwa Watanzania kukiamini Chadema hivyo hawezi kukubali kuruhusu mtu yeyote yule anayetumia njia ya wazi au ya kificho kukidhoofisha.
“Kuna watu walipata hofu na kunitumia hadi sms kuhoji iwapo akina Ole Millya wametumwa na Lowasa (Edward Lowasa, Mbunge wa Monduli) kuja kukipeleleza Chadema, najua baadhi mko hapa na ninawatoa hofu kuwa
chama chetu ni taasisi imara isiyoweza kuhujumiwa na mtu au kundi la watu kwa nguvu wala mbinu yoyote,” alitamba Mbowe.
Aliwataka wanaofikiri Lowassa na wengine wenye ukwasi kuweza kununua viongozi wa Chadema kujiuliza kwanini hawakuweza kufanya hivyo kipindi chote walichokitumia kukijenga chama hicho ambacho ni tishio kwa CCMna mafisadi wote nchini.
Mbowe alitumia fursa hiyo kuponda uteuzi wa Baraza la Mawaziri akisema Rais Kikwete amevunja katiba kwa kuwateua watu ambao hawajaapishwa kuwa wabunge kushika nafasi za uwaziri.
Licha ya kuvunja katiba kwenye uteuzi, Rais pia amekiuka kwa kuwateua Wazanzibari kwenye wizara ambazo siyo za Muungano kama Afya aliyokabidhiwa na Dk Husein Mwinyi.
Makada wapokewa
Waliokuwa makada wa CCM waliojiengua na kuhamia Chadema walipokelewa na wote kuahidi kutumia uzoefu, juhudi na maarifa yao kisiasa kukijenga chama chao kipya kwa kushirikiana na wanachama na viongozi
wote.
Ole Millya aliahidi kudhihirisha kuwa hakua mzigo CCM kama wanavyodai baadhi ya viongozi mara alipotangaza kujiunga upinzani kwa kukifanyia chama hicho kitu ambacho hakitasahaulika milele akianzia na kuipenyeza
Chadema kwa jamii ya Wamaasai.
“Vijana wengi walioko ndani ya CCM wanaishi kwa matumaini ya kupewa vyeo kama ukuu wa wilaya na nyadhifa mbalimbali badala ya kusimamia haki na ustawi wa taifa,” alisema Ole Millya
Mila na laana kwa Ole Millya akigeuka
Kabla ya viongozi kuanza kuhutubia, wazee wa kimila wa jamii ya Wamaasai waliendesha sala ya Mila hiyo kwa kumkalisha kwenye kigoda Ole Millya na kumpa laani iwapo atageuka na kukisaliti Chadema.
“Mungu amekutuma wewe Ole Millya kuwakomboa Wamasaai kutoka kwenye utumwa waliokaa nao kwa miaka 50 kama ambavyo alimtuma Mussa kuwakomboa Waisraeli kutoka kwenye utumwa wa miaka 40 Misri. Usiwe
kinyonga kwa kugeuka, angalia huu umati ulioko mbele yako,” alisema Mzee Naftali Mollel
Kwa upande wao aliyekuwa Diwani wa Kata ya Sombetini, Alphonce Mawazo na Ally Banganga aliyekuwa mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM waliojiunga Chadema walisema chama hicho tawala tayari imekufa na kinasubiri kuepelekwa chumba cha kuhifadhia maiti kusubiri mazishi.
“Wanaohoji kwanini tumetoka CCM kwanza watueleze hicho chama kilipo kwa sababu tayari kimekufa mioyoni mwa wa Watazanania,” alisema Mawazo huku akishangiliwa
Akihutubia mkutano huo uliohudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Arusha, Godbless Lema aliwataka wanaCCM wanaotaka kukihama chama hicho na kujiunga Chadema kufanya haraka kwa
sababu mlango wa ‘neema’ unakaribia kufungwa.
“Kuna kipindi kinakuja siku siyo nyingi ambapo kujiunga Chadema itakuwa dili. Wanaotaka kuja na wafanye hivyo sasa kabla hatujafunga milango,” alisema Lema
Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa, alisema moto uliowashwa na Operesheni ‘Vua gamba, vaa gwanda’ ulioanzia Arusha, sasa umeanza kuenea nchi nzima akitaja matukio ya madiwani na wanachama
kadhaa kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa kuhamia Chadema.
Golugwa alisema baada ya mkutano wa jana Jijini Arusha, mikutano ya Operesheni ya Movement for Change inahamia wilaya za Longido, Ngorongoro, Simanjiro na kumalizikia Monduli.
Katika mkutano huo, Mbowe alikabidhi kadi za uanachama kwa Ole Millya, Bananga, Mawazo na viongozi kadhaa wana CCM waliojiunga Chadema ambapo kwa niaba ya wenzao.
Hamasa kubwa iligubika umati uliohudhuria baada ya mwana CCM mwenye asili ya kiasia aliyejitambulisha kwa jina la Adil Dewji alipopanda jukwani kurejesha kadi ya CCM na kujiunga Chadema.
Wengine waliojiunga Chadema kutoka CCM ni pamoja na wenyeviti kadhaa wa Serikali za mitaa kutoka Wilaya za Arusha, Monduli, Arumeru, Ngorongoro na Longido ambao waliwakilishwa na Ignas Mfinanga aliyekuwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Themi, jijini Arusha.
Post a Comment
Post a Comment