WAKILI maarufu nchini ambaye pia aliwahi kuwa
Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Mbeya Bw.Sambwee Shitambala amechukua na
kurejesha fomu ya kuwania nafasi ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa
(NEC)na kuendelea kuwabeza wapinzani kwa kutokuwa na mikakati endelevu ya
maendeleo kwa wananchi.
Bw.Shitambala ambaye amekuwa ni miongoni mwa
wanachama kadhaa wa CCM waliojitokeza kuwania nafasi hiyo ameendelea kuviponda
vyama vya upinzani na kusema kuwa ni ndoto kwa vyama hivyo kushika dola kwa
kuwa wanaendelea kupandikiza chuki kwa wananchi dhidi ya serikali na hivyo
kusababisha kudorora kwa maendeleo.
Bw. Shitambala amekuwa ni miongoni mwa
wanasiasa machachari wakati akiwa katika kambi ya upinzani ambaye pia amewahi
kugombea Ubunge kwa tiketi ya CHADEMA katika jimbo la Mbeya vijijini akichuana
na mgombea wa CCM na baadaye aliamua kujiunga na CCM April Mwaka jana mjini
Dodoma mbele ya Rais Jakaya Kikwete.
Amesema kuwa ameamua kujichimbia zaidi ndani ya
uongozi wa juu wa CCM ili kuweka mikakati na mizizi imara itakayofanya chama
hicho kising’oke madarakani na kwamba ukongwe wa chama hicho unakisaidia
kukifanya kiendelee kuongoza nchi kwa karne nyingi zijazo.
Amesema kuwa nia yake ya dhati ni kuona CCM haing’oki madarakani,kwa kuwa ina uwezo mkubwa ambapo ikitupwa itakuwa imetupwa
hazina ambayo haiwezi kupatikana tena nchini.
Amefafanua kuwa ameingia katika uongozi kama
mwakilishi mwaminifu na makini kwa ajili ya kuitumikia nchi na kwamba wale
wanaodai kuwa CCM itakufa wanajidanganya nafsi zao kwa kuwa hawaijui vyema CCM.
Amezidi kubainisha kuwa chama chochote chenye
viongozi makini kila kinapomaliza uchaguzi kinarejea kwenye utekelezaji wa
ilani zake kwa maslahi na tija ya wananchi na si kuendeleza malumbano na
maandamano ambayo yanaibua chuki na uhasama baina ya wananchi na serikali yao.
Wengine waliojitokeza kuwania nafasi hiyo hadi leo mchana ni pamoja na mkulima aliyewahi kuingia katika mchuano wa kura za
maoni kugombea nafasi ya Urais ndani ya CCM mwaka 1995 Bw.Agrey Mwasanguti
ambaye pia amerejesha fomu yake jana katika ofisi za CCM wilaya ya Mbeya mjini.
Post a Comment
Post a Comment