MKAZI WA MYUNGA AKIELEZEA MATUKIO YA MAUAJI YANAYODAIWA KUFANYWA NA MFANYABIASHARA ANAYEDAIWA KUKUMBATIWA NA SERIKALI
Na, Rashid Mkwinda, Momba
WAKATI zoezi la sensa ya watu na makazi
likiendelea nchini kote wakazi wa kijiji cha Myunga kata ya Myunga wilayani
Momba mkoani Mbeya wamesisitiza azma yao ya kutohesabiwa hadi pale serikali
itakapotoa tamko juu ya kulindwa kwa mtuhumiwa wa mauaji ya njia za ushirikina
yaliyodaiwa kufanywa na mfanyabiashara mmoja kijijini hapo.
Wananchi hao walizungumza katika kikao maalumu
cha kutathmini mauaji yaliyotokea kijijini hapo na kusababisha uvunjifu
wa amani uliotokana na kuuawa kwa wakazi wa kijiji hicho na kunyofolewa sehemu
za siri ambapo hata hivyo mtuhumiwa wa mauaji hayo alitimuliwa kijijini hapo
baada ya wananchi wenye hasira kubomoa na kuchoma nyumba yake.
Madai ya kuwepo kwa mauaji ya kishirikina yaliibuliwa
mwezi Machi mwaka huu ambapo jumla ya watu saba waliuawa na miili yao kukutwa
pembezoni mwa mto Momba ambapo mara baada ya wananchi hao kupiga kura
walimbaini mfanyabiashara huyo (jina tunalo) kuwa anahusika na mauaji hayo.
Wakielezea ushahidi wa kuthibitisha kuhusishwa
kwa mfanyabiashara huyo wakazi wa kijiji hicho walisema kuwa baadhi ya nguo za
watu waliouawa zilikutwa nyumbani kwa mfanyabiashara huyo zikiwa zimetapakaa
damu huku kukiwa na baadhi ya silaha kama vile visu na mapanga ambayo yanadaiwa
kutumika kufanya mauaji.
Jofrey Simwanza mkazi wa kijiji cha Lwasho
katika kata ya Myunga alisema kuwa mmoja wa vijana waliouawa
aliyefahamika kwa jina la Shati Sichula mwili wake ulikutwa chini ya daraja la
mto Momba huku mwili wake ukiwa umeondolewa baadhi ya viungo kama vile sehemu
za siri, macho na ulimi.
Alisema kuwa matukio ya mauaji hayo yaliendelea
ambapo mwezi Juni mwili wa msichana mmoja ulikutwa ukielea katika mto Momba
huku ukiwa umekatwa matiti na kunyofolewa ulimi,macho na sehemu za siri
ambapo matukio hayo yalisababisha wananchi kuhoji sababu za mfanyabiashara huyo
kutochukuliwa hatua za kisheria.
Akizungumzia matukio hayo kijijini hapo Ofisa
mtendaji wa kata hiyo Salum Jonas alisema kuwa kata hiyo yenye wakazi
wanaokadiriwa kufikia 1,200 na kaya 200 wanaishi katika hofu kutokana na mauaji
yaliyotokea ambayo yanahusishwa na imani za ushirikina hali ambayo inawafanya
wakimbie nyumba zao na kuishi porini.
Alisema kuwa mara baada ya kutokea kwa mauaji
hayo wananchi walivamia nyumba tatu za watu wanaohisiwa kuwa ni wauaji na
kuzichoma moto na kisha kubomoa na kusababisha upotevu wa mali zilizokuwemo
katika nyumba hizo.
Alisema kuwa hatua hiyo ilisababisha jeshi la
polisi kuwakamata wananchi wapatao 45 wakiwemo wafanyakazi wanaojenga barabara
ya Tunduma- Sumbawanga ambao wanaishi kijijini hapo na kwamba hata hivyo baadhi
yao waliachiwa huru na kubakizwa watuhumiwa 13 ambao wanahusishwa na kosa la
jinai la kuvunja na kuiba.
Kwa upande wao wananchi wa kijiji hicho walidai
kuwa utaratibu uliotumika kuwakamata watuhumiwa hao haukuwa wa kibinadamu kwa
kuwa askari waliotumwa kuwakamata walivamia nyumba na kubomoa milango na
kuwakamata baadhi ya akina mama wakiwa uchi na kuwapakiza katika gari la polisi
nyakati za usiku.
Walisema kuwa kitendo hicho kinashindwa
kuwabaini watu wema na wahalifu ambapo hata watu watakaokuja kuhesabu sense
wanadaiwa kuja nyakati za usiku hali ambayo bado itajenga hofu kwa wao kutoa
ushirikiano kwa makarani wa sensa.
Mmoja wa akina mama hao aliyejitambulisha kwa jina
la Anna Nakamanga alisema kuwa askari walivamia nyumbani nyakati za usiku na
kuwatoa nje wakiwa uchi kisha kuwatandika viboko na kusema kuwa kitendo hicho
ni udhalilishaji mkubwa uliofanywa na askari polisi kwa raia wasio na hatia.
Naye kiongozi wa Kanisa la Pentekostal la
kijijini hapo aliyejitambulisha kwa jina la Mchungaji Nsokolo alisema kuwa
matatizo yaliyopo kijijini hapo yamesababishwa na mauaji ya kinyama
yaliyofanywa na mfanyabiashara huyo ambaye pamoja na kupatikana kwa vidhibiti
juu ya mauaji aliyoyafanya jeshi la polisi limemuachia huru bila kumchukulia
hatua za kisheria.
Akizungumzia tukio hilo kwa njia ya simu kamanda
wa polisi mkoani Mbeya Diwani Athuman alisema kuwa alifikishiwa taarifa za wizi
na uharibifu wa mali na mmoja wa wafanyabiashara wa eneo hilo ambapo
alichokifanya ni kuamuru wahusika wakamatwe kwa kuwa walifanya kosa na kwamba
hakuna taarifa zilizofika kwake zinazohusu mauaji dhidi ya wananchi kwa imani
za ushirikina.
Aidha taarifa za awali zilidai kuwa mara baada
ya mfanyabiashara huyo kukutwa na vidhibiti vya nguo zenye damu na silaha
zinazodaiwa kutumika katika kutekeleza mauaji hayo aliachiliwa huru kwa kile
kilichoelezwa kuwa aliwahonga fedha baadhi ya viongozi wa polisi wa
wilaya ili kuficha ukweli wa tukio hilo.
|
Post a Comment
Post a Comment