NA SOLOMON MWANSELE,MBEYA.
BARAZA la Masheikh wa mkoa wa Mbeya, kwa kauli moja limemsimamisha
uongozi Sheikh wa wilaya ya Mbarali, Yassin Bambala, kwa tuhuma za kuhusika
kuwataka waislam kususia zoezi la Sensa ya Watu na Makazi.
Imeelezwa Sheikh Bambala amekuwa anashiriki na kuhudhuria
vikao vya baadhi ya waislamu wanaopinga Sensa inayotarajia kufanyika nchini
kote kuanzia Agosti 26, mwaka huu.
Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), mkoa wa Mbeya,
Sheikh Juma Killa, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na Uhuru ofisi ya
BAKWATA iliyopo eneo la Soko Matola mjini Mbeya.
Sheikh Killa alisema Agosti 21, mwaka huu Baraza la Mashekh
mkoani hapa, lilikutana ambapo moja ya ajenda ilionekana baadhi ya viongozi
wenzao walikuwa wakionekana kufanya kampeni za chini chini kuungana na taasisi
nyingine kuwataka waislam wasishiriki Sensa ya mwaka huu.
“Hawa walifanya hivi huku wakati wanafahamu fika, msimamo wa
BAKWATA na kiongozi mkuu wa Waislamu (Mufti), kuhusu kuhakikisha waislamu
wanashiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi” alisema Sheikh
Killa.
Aliongeza hivi karibuni masheikh wa ngazi za wilaya na wale
wa mikoa nchini, waliitwa na Mufti mjini Dodoma
kwenye kikao cha Tume ya dini.
Kwa mujibu wa Sheikh Killa, kupitia kikao hicho viongozi hao
wa kiislamu walipewa msimamo wa pamoja kuhusiana na zoezi la Sensa na
wakakubali kuwa wakirudi maeneo yao
kuwahamasisha waislamu wenzao juu ya umuhimu wa Sensa.
Aliongeza lakini wamebaini kuwa baadhi ya Masheikh, akiwemo
Sheikh Bambala baada ya kurudi kutoka Dodoma,
wameanza kufanya kazi tofauti na makubaliano ya pamoja yaliyofikiwa.
Katibu huyo wa BAKWATA mkoa, alisema kufuatia hali hiyo
wameanza kuchukua hatua kali kwa viongozi waliodhihirika na ushahidi kupatikana
kuwa wamekuwa wakienda kinyume na maagizo ya Tume ya Dini hiyo.
Sheikh Killa alisema:”Hivyo kwa kauli moja, Baraza la
Masheikh mkoa wa Mbeya, limemsimamisha kazi sheikh wa wilaya ya Mbarali,
Bambala kwa kosa la kuhudhuria vikao vya wale wanaopinga zoezi la Sensa”.
Aliongeza Baraza hilo limeanza na Sheikh Bambala baada ya
kuona hataki kuendana na misimamo ya pamoja iliyofikiwa na Baraza lao, na kuwa hatua kama hiyo haitaishia hapo
bali itashuka hadi misikitini na kwenye mitaa ili kukomesha hujuma hizo chafu.
Alisema nia ni kuhakikisha kuwa hakuna kiongozi wa dini hiyo
ya Kiislamu anayeamua kwa matakwa yake kupingana na misimamo ya Baraza pamoja
na ile ya serikali.
Post a Comment
Post a Comment