Na, Rashid Mkwinda
WAFANYABIASHARA zaidi ya 300 wa soko la Vwawa mjini Vwawa wilayani Mbozi wamesitisha kutoa huduma katika soko hilo baada ya kiongozi wa soko hilo na wafanyabiashara wengine wawili kukamatwa na askari polisi usiku wa manane nyumbani kwao.
Mara baada ya wafanyabiashara hao kukamatwa usiku wa manane, wafanyabiashara wenzao walifika asubuhi na kupata taarifa kuwa wenzao wamekamatwa hivyo na wakaamua kufunga biashara zao na kuungana na wenzao katika kituo cha polisi kwa ajili ya kuwachukulia dhamana.
Mmoja wa wajumbe wa soko hilo aliyejitambulisha kwa jina la Paschal Lwila alisema kuwa waliokamatwa ni pamoja na Katibu wa soko hilo Osward Mbughi, na wafanyabiashara wawili ambao ni Orasmo Nyingi maarufu kwa jina la Pompi na Amos Sanga ambao walifuatwa nyumbani kwao majira ya saa 7 usiku na askari polisi.
Alisema kuwa tatizo la kukamatwa kwao linahusishwa na mgogoro wa muda mreefu baina ya Halmashauri ya mji wa Vwawa na wafanyabiashara ambao walikubaliana kwa pamoja kusitisha kutozwa ushuru katika soko hilo hadi litakapoondolewa gulio la kila jumamosi eneo la Ichenjezya ambalo linachangia kwa namna moja ama nyingine kuharibu biashara katika soko kuu.
Alisema kuwa jana mchana walifika maofisa watendaji wapatao 9 akiwemo Bwana Afya, kwa nia ya kukusanya ushuru bila kupewa taarifa viongozi wa soko na kwamba kilichofanyika kilikiuka makubaliano yaliyoafikiwa baina ya pande mbili za wafanyabiashara na mamlaka ya mji mdogo wa Vwawa kwamba lilitakiwa kuondolewa soko la mnada wa Ichenjezya Julai mosi.
Alifafanua kuwa mnada huo wa soko ni wa kila jumamosi ambapo hata hivyo soko hilo la mnada lipo jirani na soko la kila siku na hivyo kuchangia kudorora kwa biashara katika soko hilo kuu.
Kundi hilo la wafanyabiashara lilikusanyika katika viwanja vya kituo cha Polisi Vwawa wakisubiri hatima ya wenzao ambapo muda mfupi baadaye walichukuliwa kupelekwa mahakamani.
TAARIFA ZAIDI ZA TUKIO HILO ZITAKUJIA...
Post a Comment
Post a Comment