MAKUNDI YA WANAWAKE NA MITAZAMO YAO KWA WANAUME
TUMSHUKURU Mungu kwa yote ambayo sisi tunayaona na mengine yaliyo juu ya
upeo wa macho yetu. Mzingo wa maisha umejaa changamoto nyingi, Mwenyenzi
anatulinda kila nukta, lakini hata kama hujui hilo, basi pumzi ya uhai ikupe
sababu ya kuamini kudura za Maulana.
Kwa uwezo niliojaliwa na Mola Mpaji, leo nachambua
mada inayohusu makundi ya wanawake na mitazamo juu ya wanaume. Ninachozingatia
hapa ni fikra katika makundi ambayo nayachambua hapa, vigezo vyao kwa wanaume
vipo kimtazamo zaidi.
Fikra zao ndizo zimetengeneza mtazamo kwa namna ambayo wao wamepima maslahi
yao kwa wanaume. Maisha yanavyosogea mbele ndivyo binadamu wanavyojihisi wana
akili na maarifa zaidi. Sasa wanajiona wana uwanja mpana zaidi wa kuchanganua,
kuchambua na kuchagua.
Wakati miaka ya nyuma kila mwanamke ndoto yake kuu ilikuwa kuolewa ili apate
mume wa kutulia naye, hivi sasa mambo yamebadilika. Makundi ni mengi, hata hilo
ambalo linaundwa na wale wanaoteswa na kupata waume lipo lakini halitambi,
linabezwa.
Sababu ya kundi hilo kubezwa ni mtazamo uliopo kwenye makundi mengine mawili
kuwa watu wanaoota kupata wanaume wa kuwaoa, mawazo yao ni ya kale. Kwamba
hayajitoshelezi kwa kizazi cha sasa ambacho kimeegemea teknolojia na
utandawazi.
Tamaa ya fedha na kupanuka kwa sanaa, video zinazowaonesha mastaa wa
Marekani na Ulaya pamoja na mitindo yao ya maisha, kumechangia kwa kiasi
kikubwa kuwafanya baadhi ya wanawake kutengeneza mitazamo yao ya kupenda.
KUNDI LA KWANZA
Mara nyingi linaundwa na wasichana wadogo na hata wanawake wakubwa wenye
fikra ambazo ni rahisi kuziita changa. Hawa hupenda wanaume kutokana na
muonekano wao. Inawezekana ikawa ni mtindo wa mavazi au umbile lake.
Katika kundi hili, ni rahisi kukuta mwanamke ameangukia kwa mwanaume asiye
na malengo yoyote ya maisha. Matokeo yake, mwanamke huyo ndiye anageuka mlezi
wa mwanaume husika, akimhudumia kila kitu.
Mathalan, anavutiwa na urefu, atafanya juu chini mpaka ahakikishe amemtia
kwenye himaya yake. Hata kama hana ujasiri wa kusimama mbele ya mwanaume na
kuwasilisha hisia za moyo wake lakini namna atakavyokuwa anaonesha kupagawa,
itatosha kufikisha ujumbe.
Inawezekana pia ikawa kwa umbo lake lililojengeka kimazoezi. Ipo mifano ya
mabaunsa wengi tu mjini ambao kimuonekano tu, ipo wazi kuwa wana nguvu za
kutosha ambazo wangezitumia katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali.
Ajabu ni kuwa misuli na nguvu zao havina faida, kwani wanalelewa tu na
wanawake.
Hata mavazi, jinsi mwanaume anavyobadili mavazi, inaweza kumsababishia
mwanamke kuingia kichwakichwa. Sura nayo ni kielelezo pamoja na sifa nyingine
ambazo huonekana wazi katika mwili wa binadamu. Ongezea rangi, mpangilio wa
meno, anaweza kupenda mwanya tu!
Yupo mwanamke ambaye anaweza kudondoka kwenye penzi kwa sababu mwanaume
mwenyewe huwa anavaa miwani.
Itaendelea wiki ijayo.CHANZO GLOBAL PUBLISHERS
|
Post a Comment
Post a Comment