-STORI NA RASHID MKWINDA-
MKAZI wa kitongoji
cha Iponjola kijiji cha Isange wilayani Rungwe mkoani Mbeya aliyefahamika kwa
jina la Riziki Mwangoka(27)anadaiwa
kufanya kitendo cha kinyama kwa kumuua mwanaye mdogo mwenye umri wa miaka
mitatu kwa kuchimba shimo sebuleni kwake na kumfukia akiwa hai.
Tukio hilo la kinyama linadaiwa kufanyika
Novemba mwaka jana ambapo mtuhumiwa alimchukua mtoto huyo kwa nguvu kutoka kwa
mama yake ambaye awali alikuwa ni mkewe aliyefahamika kwa jina la Esther
Mwambenja(23)na kulazimisha kwenda kuishi na mtoto huyo nyumbani kwake.
Kamanda wa polisi mkoa
wa Mbeya Diwani Athumani amesema kuwa mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa katika
mgogoro wa kindoa na mkewe alilazimisha kumchukua mtoto huyo aliyefahamika kwa
jina la Debora Riziki(3) kutoka kwa mama yake mzazi.
Amesema kuwa
mtuhumiwa alimfuata mtoto huyo kwa mama yake umbali wa zaidi ya
kilomita 30 katika kijiji cha Kiwira na kuibuka mzozo wa nani aishi na mtoto
huyo ndipo mtuhumiwa alipomchukua mtoto huyo kwa nguvu na kuondoka naye.
Amesema
kuwa alipofika nyumbani kwake mtoto alikuwa amechoka na kulala usingizi
ndipo baba alipochimba shimo sebuleni na kumzika mwanaye akiwa hai.
Amesema kuwa kwa
kipindi cha zaidi ya miezi minne mtuhumiwa alikuwa akiishi na maiti ndani ya
nyumba yake ambapo mama wa mtoto alikuwa akihitaji kumchukua mtoto huyo lakini
alikuwa akimpiga chenga ndipo alipotoa taarifa kituo cha polisi kuhitaji
kumpata mwanaye.
Kamanda Athumani amesema
kuwa polisi walifika nyumbani kwa mtuhumiwa na kuuliza alipo mtoto huyo ambapo
kwa muda mrefu hakutoa ushirikiano wowote hadi jana aliposema kuwa alimuua
mwanaye na kumzika katika shimo alilochimba sebuleni kwake.
Amesema kuwa polisi
walifika nyumbani kwa mtuhumiwa na kufukua shimo hilo na kuukuta mwili wa mtoto huyo na kusema kuwa
katika uchunguzi hawakuona dalili zozote za kuuawa kwa mtoto huyo na
kuthibitisha kuwa mtoto huyo alifukiwa shimoni akiwa usingizini na baadaye kufariki
dunia.
|
Post a Comment
Post a Comment