DIWANI wa
kata ya Tunduma kwa tiketi ya CHADEMA Bw.Frank Mwakajoka na Mchungaji wa Kanisa
la KKKT Tunduma Gidioni Mwamafupa wamejisalimisha polisi baada ya tamko la
jeshi la polisi mkoa wa Mbeya kuwataka wajisalimishe kutokana na vurugu za
uchinjaji.
Akizungumzia
tukio hilo kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya Bw.Diwani Athumani amesema kuwa Bw.
Mwakajoka na Mchungaji Mwamafupa wanahojiwa na polisi kufuatia taarifa za
kiintelijensia kwamba viongozi hao wamehusishwa na kuibuka kwa vurugu hizo.
Amesema kuwa
mara baada ya kuibuka kwa vurugu hizo ambazo zilisababisha uharibifu wa mali na
majeruhi, watu 94 walikamatwa na kufikishwa mikononi mwa polisi na baada ya mahojiano
watu 45 walijidhamini kutokana na polisi kujiridhisha na maelezo yao.
Aidha
Kamanda Diwani amesema kuwa kati yao watu 45 wamefikishwa mahakama ya wilaya ya
Mbozi kwa tuhuma za kujihusisha na makosa ya kula njama,kufanya vurugu, uharibifu
wa mali, kuvunja msikiti na kujeruhi ambapo kesi yao itarudi tena katika mahakama
hiyo April 18 mwaka huu.
Akizungumzia
mazingira ya kushikiliwa kwa Bw. Mwakajoka na Mchungaji Mwamafupa Kamanda
Athumani alisema kuwa mara baada ya kupata taarifa za kutafutwa na jeshi la
Polisi Bw. Mwakajoka amejisalimisha polisi leo asubuhi ambapo hadi sasa
anaendelea kuhojiwa ilhali mchungaji Mwamafupa ni miongoni mwa watu 45
walioachiwa kwa dhamana.
Kwa upande
wao CHADEMA mkoa wa Mbeya kimetoa tamko la kulaani kukamatwa kwa Diwani wa kata
ya Tunduma na kuhusishwa na vurugu za uchinjaji.
Katibu wa
CHADEMA mkoa wa Mbeya Bw. Boyd Mwabulambo amesema kuwa jeshi la polisi
linatumia mwanya wa vurugu hizo kukidhoofisha chama chao na hivyo kuendelea
kuvuruga amani na utulivu wa mji wa Tunduma.
|
Post a Comment
Post a Comment