Na, Bloga Wetu
MAHAKAMA ya hakimu mkazi wa
wilaya ya Mbeya imemhukumu kifungo cha miaka 30, mshitakiwa kosa la unyang;anyi
wa kutumia silaha,Ali Salum (32) baada ya kukiri kutenda kosa hilo mahakamani hapo.
Mshitakiwa ambaye alifikishwa
mahakamani hapo kwa mara ya kwanza pamoja na wenzie watatu Juni 17 alikiri
baada ya kusomewa mashtaka ya uvamizi wa kutumia silaha na kupora bunduki aina
ya SAR yenye namba za usajili TZ PS 39847164020 mali ya serikali inayomilikiwa na Jeshi
la Magereza.
Akitoa maelezo ya hukumu ya
kesi hiyo Hakimu mkazi wa wilaya Bi.Aneth Nyenyema alisema kuwa anatoa uamuzi
huo baada ya mshtaakiwa kukiri mwenyewe kutenda kos hilo na kwamba adhabu inayotolewa kwa
mshtakiwa hailengi kumkomesha bali inalenga kumfundisha.
‘’Adhabu zinazotolewa na
Mahakama hazina nia ya kukomesha bali zina nia ya kufundisha, kutokana na hilo mahakama inakutia
hatiani kufuatia kukiri kwako makosa, utatumikia kifungo cha miaka 30 jela,’’alisema
Hakimu Nyenyema.
Akisoma mashataka hayo kabla
ya hukumu mbele ya hakimu mkazi wa wilaya ya Mbeya Bi.Nyenyema, Wakili wa
serikali Bi. Mwajabu Tengeneza alisema kuwa mnamo Mei 5 mwaka huu katika eneo
la Songwe gerezani mshtakiwa pamoja na wenzake watatu walikula njama na
kumvizia askari magereza WDR Ambrose Ngonyani ambaye alijeruhiwa na kuporwa
bunduki.
Alisema kuwa mshtakiwa pamoja
na wenzie walimvizia askari huyo wakati anarejea nyumbani nyakati za jioni kwa
ajili ya kujipatia chakula cha jioni ndipo, washtakiwa wakiwa na panga
walimvamia na kumjeruhi mkononi kisha wakampora bunduki.
Wakili Tengeneza alisema kuwa
washtakiwa walikiuka sheria kifungu namba 287 A ya sheria kanuni ya adhabu sura
namba 16 iliyorejewa mwaka 2002 na kuongeza kuwa mahakama inapaswa kutoa adhabu
kali iwe fundisho kwa vijana wanaotumia silaha kuhatarisha usalama wa nchi.
Awali akitoa maelezo ya
mshtakiwa aliyoyathibitisha polisi, askari mpelelezi wa kesi hiyo Koplo Vicent
Henjewele alisema kuwa mshitakiwa alitoa maelezo polisi kwa kina ikiwa juu ya
ushiriki wake wa uvamizi na uporaji huo wa silaha na kuongeza kuwa historia ya
mshitakiwa inaonesha kuwa ameshiriki matukio mengi ya uporaji.
Koplo Henjewele alisema kuwa
mtuhumiwa alikiri mbele ya polisi kuwa yeye alifukuzwa kijijini kwao Lupa
Tingatinga wilayani Chunya ambapo wananchi walimchomea nyumba yake kutokana na
vitendo vyake vya wizi na uporaji ambapo baadaye alihamia katika mji mdogo wa
Mbalizi alikokutana na mmoja wa washtakiwa wa kesi hiyo.
Alisema kuwa alipokutana na
mshtakiwa mwenzie aliyemtaja kwa jina la Emanuel Martin aliyeweahi kukutana
naye gerezani ndipo walipopanga njia za kupata bunduki kwa ajili ya kutekeleza
kazi zao za ujambazi wakiwa uraiani.
Washitakiwa wengine katika
kesi hiyo ambao wakikana mashataka yao ni pamoja
na Martin, Bryson Sanga na John Waziri ambapo hata hivyo mshitakiwa Martin
aliichekesha mahakama hiyo kwa kusema kuwa haoni sababu ya kuisumbua mahakama
naye anakiri kosa hilo
ili afungwe.
Hata hivyo Hakimu Nyenyema
alisema kuwa utaratibu wa maelezo hayo utaletwa tena mahakamani hapo Julai Mosi
ambapo kesi hiyo imepangwa tena kusikilizwa.
Post a Comment
Post a Comment