Na, Rashid Mkwinda, Njombe.
SIKU moja baada ya Rais
wa Marekani nchini Tanzania Barack Obama kusisitiza uwekezaji kwa nchi za
Afrika,mwekezaji mkubwa wa zao la Pareto kutoka nchini humo kampuni ya MacLauglin
Gormley King (MGK) yenye hisa asilimia 100 kwenye kiwanda cha Pareto kilichopo
Mafinga wilayani Mufindi mkoani Iringa amedaiwa kujiondoa katika ununuzi wa zao
la Pareto nchini.
Hatua ya mwekezaji huyo ambaye amenunua hisa zote za kiwanda
cha Pyrethrum Company Of Tanzania (PCT) kilichopo Mafinga mkoani
Iringa imedaiwa kuwa imetokana na mvutano baina yake na serikali kwa madai ya
kuruhusu wanunuzi wanunuzi wengi wa zao
hilo ambao wamesababisha kushuka kwa thamani ya zao hilo kwa kununua pareto
isiyokidhi viwango vya Kimataifa.
Kampuni (PCT)hiyo ilikuwa na uwezo wa kununua asilimia 60 ya maua yenye sumu ya pareto
nchini ambapo asilimia 40 iliyobaki ilikuwa inanunuliwa na wanunuzi wadogo.
Kujiondoa kwa mwekezaji huyo kulibainika katika kikao cha wadau
wa zao la Pareto mwishoni mwa wiki kilichofanyika mjini Makambako mkoani Njombe
ambapo mwekezaji huyo alisusia kikao hicho na kudai kuwa ameamua kuachana na
ununuzi wa pareto na kwamba atafunga kiwanda hicho.
Akizungumza katika kikao hicho kilichowakutanisha wadau na
wakulima 180 wa pareto kutoka mikoa inayolima zao hilo ya Manyara,Kilimanjaro, Iringa,Njombe na Mbeya,
mgeni rasmi katika mkutano huo Naibu Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Bw. Adam Malima alisema kuwa mnunuzi
huyo mkubwa wa pareto nchini ameamua kujitoa katika ununuzi wa zao hilo nchini.
‘’Katika mkutano ambao niliuendesha Dodoma tarehe 29-30 Mei
tulikubaliana kwamba kampuni ya Pareto Tanzania (PCT) wataheshimu makubaliano
hayo ambayo naamini ameanza kutekeleza, cha kusikitisha hapa ni kwamba kampuni
PCT anakiuka makubaliano yaliyoridhiwa katika hati ya makubaliano-MOU(2009)’’
alisema Bw. Malima.
‘’Leo wakati napewa taarifa nimeambiwa kuwa mdau mkuu PCT
hatashiriki, nikatoa maamuzi ya pale kwa pale kwamba kama kuna watu ambao
hawawezi kwenda sambamba na sisi, waliobaki inabidi wachukue nafasi,’’alisema.
Bw. Malima alisema kuwa mwekezaji yoyote anayewekeza nchini
anapaswa kuwatambua Watanzania kwa kutoweka masharti magumu ambayo yataleta
kikwazo katika uwekezaji wao, ‘’Hatuwezi kukubali masharti magumu ya uwekezaji
wao, tunataka watambue kuwa kuna mkulima mkubwa na mkulima mdogo, serikali yetu
haiwezi kukubali wawekezaji wa aina hii,’’alisisitiza.
Alisema kuwa mwekezaji aliyejitoa ananunua asilimia 60 ya
maua yenye sumu ya pareto hivyo wanunuzi waliobaki wanayofursa ya kujipanga
upya kuangalia namna ya kuziba pengo hilo ili kuhakikisha wakulima wanaendelea
kunufaika na zao hilo.
Aidha Bw. Malima alisema kuwa serikali inapenda wawekezaji kwenye viwanda ili kuongeza thamani
ya zao hilo hadi kufikia hatua ya usalishaji wa sumu ghafi ya pareto na hata
kufikia hatua ya mwisho ya uchujaji wa sumu hiyo kwa ajili ya matumizi ya dawa
za kuulia wadudu na matumizi mengine ya sumu ya pareto.
Alisema kuwa ni muhimu sehemu kubwa ya utengenezaji wa
bidhaa ya pareto ifanyike nchini badala ya kusafirisha bidhaa ghafi nje ya nchi
jambo ambalo linapunguza ajira na thamani ya zao hilo.
Katika kikao hicho wadau walitangaziwa bei dira ya msimu wa
kilimo wa mwaka 2013-14 ambayo itaanzia sh.2000 hadi sh. 2300 kulingana na
madaraja ya zao hilo ambapo bei ya chini ya ununuzi wa zao hilo itakuwa ni
sh.2000.
Awali akizungumza katika kikao hicho Mkurugenzi wa Bodi ya
Pareto Bw. Ephrahim Mhekwa alisema kuwa Bodi
ya Pareto nchini iliwanyima PCT leseni kutokana na kudaiwa fedha za mfuko wa
wadau zaidi y ash. Milioni 700 lakini baadaye aliwarejeshea leseni baada ya
kuagizwa na Wizara ya Kilimo.
Alisema kuwa kujitoa kwao kunatoa fursa ya wanunuzi wengine
kujipanga kumudu kununua pareto kwa asilimia 100 ili kukidhi mahitaji ya
uzalishaji wa zao hilo nchini ambapo kwa msimu wa mwaka 2011-’12 kulikuwa na uzalishaji wa tani 5,700 ambapo
msimu unaoisha wa 2012-’13 uzalishaji uliongezeka hadi kufikia tani 6,100.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya PCT Bw.
Wildmel Mushi akizungumza kwa njia ya simu alisema kuwa, kampuni yake
haijajitoa katika ununuzi wa zao hilo,isipokuwa msimamo wao wa kusimamia ubora
wa zao hilo unatofautiana na msimamo wa serikali.
Alisema kuwa pareto ni zao linalopata ubora kutokana na sumu
iliyopo na kwamba wanunuzi wengi hawaangalii ubora na hivyo kusababisha kushuka
kwa zao hilo katika soko la dunia.
Alisema wao walikuwa wakinunua pareto kwa bei ya sh. 1900 kutokana
na thamani ya maua ya pareto ambapo baadhi ya wanunuzi waliopewa leseni
walikuwa wakinunua maua hayo hayo kwa bei y ash. 2400 bila kujali ubora na
thamani ya sumu iliyopo.
Bw. Mushi alisema kuwa hali hiyo imeleta ushindani usio na
tija kwa Taifa na kwamba matokeo ya hali hiyo kuna uwezekano mkubwa wa kuua zao
la pareto nchini.
‘’Hili zao si sawa na mazao mengine kama vile pamba, korosho
na mengineyo, zao hili linaangaliwa ubora wa sumu kwenye maua, kama wanunuzi
wanajitokeza kununua maua yasiyo na sumu sisi hatuko tayari, ‘’alisema Bw.
Mushi.
|
Post a Comment
Post a Comment