KLABU ya
waandishi wa habari mkoa wa Mbeya (MBPC) imeweka maazimio ya kuimarisha
mahusiano baina ya waandishi wa habari na wamiliki wa vyombo vya habari nchini ambao
kwa muda mrefu wamekuwa wakitumia kazi za waandishi wao kwa malipo yasiyokidhi mahitaji.
Maazimio hayo ya wanahabari yametolewa katika mkutano wa waandishi wa habari na wadau kufuatia
wanahabari kudaiwa kujiingiza katika kazi zinazoashiria kuwepo na mianya ya rushwa na hivyo kukosa weledi wa utendaji kazi
makini kwa taaluma ya habari.
Miongoni
mwa maazimio ambayo yalisomwa mbele ya Mgeni rasmi mkuu wa wilaya ya
Momba Bw. Abihudi Saideya ni pamoja na klabu hiyo kuweka msimamo kwa
waandishi wake kuwa na mkataba na vyombo wanavyoandikia.
Maazimio
hayo yalikuja baada ya kuibuka kwa malalamiko kutoka kwa waandishi
ambapo mmoja wa waandishi waandamizi na waanzilishi wa Klabu za
waandishi wa habari nchini Bw. Jonas Mwasumbi alisema kuwa waandishi
wengi wa
habari wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu kutokana na
wamiliki
kutowajibika vyema.
Alisema kuwa
wanahabari wanapaswa kuwezeshwa katika kuibua matatizo katika jamii lakini
wamiliki wamekuwa ni chanzo cha kudorora kwa taarifa za kijamii zinzopaswa
kuibuliwa ili kupatiwa ufumbuzi.
Naye
mwakilishi wa Star televisheni kutoka mkoani Mbeya Bw. Fred Bakalemwa alisema
kuwa waandishi wengi wa habari wamejikuta wakishindwa kutumia vyema taaluma yao
kutokana na kukosekana kwa ushirikishwaji baina ya wamiliki na wanahabari.
Alisema kuwa
wanahabari wengi wa mikoani wanashindwa kutumia vyema taaluma yao na hata
kushindwa kufuatilia kazi za kijamii kutokana na kushindwa kuwezeshwa na hata
kujikuta wakitumia uwezeshaji kutoka kwa vyanzo vya habari na hivyo kumnyima
fursa na uhuru wa kuibua udhaifu wa watendaji.
Aidha
alisema wanahabari wanapaswa kuwa wazalendo katika utoaji wa taarifa hususani
zile ambazo zina mgongano katika jamii ili kuepuka kuibua vurugu na kuchafuka
kwa amani na utulivu wa nchi.
Kwa upande
wake mwandishi maarufu aliyewahi kufanyia kazi katika vituo mbalimbali vya
runinga Bw. Jerry Muro alisema kuwa tatizo la waandishi wengi wa mikoani
wamekuwa wakibeba mabango na nembo za vyombo wanavyoviwakilisha bila maslahi.
Alisema
wamiliki wengi wa vyombo vya habari hawawajali waandishi wao hasa wa mikoani
ambapo wengi wao hufanya kazi bila mkataba na
wengine hucheleweshewa malipo kwa muda mrefu.
Awali
wakizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa wilaya ya Momba Bw. Abihudi Saideya na
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya Bw. Athumani Diwani walisema kuwa wanahabari
wanapaswa kuimarisha na kuboresha uhusiano na wadau ili kuwa karibu na jamii.
Mkuu wa
wilaya ya Momba Bw. Saideya alisema kuwa wanahabari ni nguzo muhimu katika
maendeleo ya jamii hivyo ni vyema wakatumia fursa hiyo kwa kuimarisha mahusiano
na jamii kwa nia ya kujenga umoja na mshikamano.
Naye Kamanda
wa polisi mkoa wa Mbeya Bw. Diwani alisema ili kujijengea uwezo ni vyema
wanahabari wakajiunga pamoja ili kupata fursa ya kuwezeshwa na kufanikiwa
kiutendaji.
Post a Comment
Post a Comment