Add caption |
Hii ni Bar katika Nyumba inayomilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi ambayo mapato yake yanadaiwa kutafunwa na wajanja |
MAMILIONI
ya
fedha za Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi yanayotokana na pango la nyumba 3
za halmashauri hiyo yanadaiwa kutafunwa na wajanja kwa takribani miaka
30, huku baadhi ya watendaji wakidaiwa kuficha vyanzo vya mapato hayo kwa nia ya kujinufaisha.
Fedha hizo
ambazo zinatokana na miradi ya nyumba tatu za halmashauri hiyo tangu mwaka 1983 ambavyo ni
vitega uchumi vilivyopo mjini Vwawa vimepangishwa kwa watu binafsi huku mapato
yake yakidaiwa kuishia mikononi mwa baadhi ya watendaji wa halmashauri hiyo.
Imedaiwa
kuwa baadhi ya watendaji wa halmashauri hiyo wamekuwa wakichukua kodi
katika nyumba tatu za halmashauri hiyo bila kuziwasilisha ofisini huku
wengine wakijimilikisha nyumba hizo na kufahamika kwa wapangaji kama ni
wamiliki wa nyumba hizo.
Nyumba hizo zimepangishwa watu na taasisi binafsi za
Tanganyika Famers Association(TFA) Chama Cha Akiba na Mikopo lililopo karibu na
soko la Vwawa na nyumba ya kulala wageni ya Mbozi Development Council(MDC)
ambazo tangu zilipopangishwa mwaka 1983 hakuna mapato yaliyoingizwa kwenye
halmashauri hiyo.
Aidha
mwandishi wa gazeti hili alitembelea nyumba hizo na kuwauliza baadhi ya
wapangaji kujua ni nani wanayemlipa kodi ya nyumba na kuwataja baadhi
ya watu ambao wanadaiwa kuwa ni watumishi wa halmashauri hiyo(majina
tunayo) kwamba ndio ambao huwalipa kodi hiyo kwa miaka yote.
Hoja hiyo
iliibuliwa katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya
Mbozi na Diwani wa kata ya Ihanda Bw. Joel Kasebele katika maswali ya papo kwa
papo kwa Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Bw. Levison Chilewa ambaye alitakiwa
kutoa ufafanuzi juu ya mahala zinapokwenda fedha za pango za nyumba hizo.
‘’Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kupata ufafanuzi juu ya mapato ya fedha zinazotokana na
nyumba tatu zinazomilikiwa na Halmashauri yetu, zinakwenda wapi, nyumba hizo ni
za Halmashauri mapato yake yanafanya kazi gani?,’’aliuliza Bw. Kasebele.
Katika
majibu yake Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bw. Chilewa alisema kuwa hajui fedha
za nyumba hizo zinakokwenda na kwamba tangu ameingie hapo miaka saba iliyopita
hajawahi kupewa taarifa kuhusu mapato ya nyumba hizo na kwamba hata hivyo ofisi
yake imewaandikia barua wapangaji ili kujua mkataba wa upangaji wa nyumba hizo.
‘’Lazima
niseme ukweli hili jambo nimelikuta, sijui lolote kuhusu mapato ya nyumba hizo,
tangu nimefika miaka saba sasa sijapewa mrejesho wowote kuhusu nyumba hizo’’,
alisema Bw. Chilewa.
Kufuatia
majibu hayo baadhi ya madiwani walisimama ili kupata ufafanuzi zaidi na kuhoji
sababu za ofisi ya halmashauri hiyo kuachia mapato ya nyumba hizo kwa takribani
miaka 30 bila kufuatiliwa.
Alisema kuwa
siku za nyuma hakukuwa na kumbukumbu wala taratibu zozote za vyanzo vya mapato
kutoka kwa uongozi uliopita na kwamba nyumba hizo zimeibuliwa hivi karibuni
ambapo jitihada zinafanyika ili kujua mikataba ya wapangaji.
Kwa upande
wake Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Bw. Elick Ambakisye alisema kuwa kikao cha
baraza la Madiwani kimeiagiza ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuandaa
taarifa sahihi ya kina juu ya vyanzo vingine vya mapato ambavyo fedha zake
zinaingia mifukoni mwa wachache.
Post a Comment
Post a Comment