Ads (728x90)


Mhandisi Gabriel Kalinga, mratibu wa Kitaifa mradi wa Bonde la Mto Songwe akizungumza wakati wa uzinduzi wa Jumuiya ya Watumia Maji wa Bonde la Mto Songwe, (JUWABOSO)

Mkuu wa wilaya ya Mbozi Dkt. Michael Kadeghe akizindua Jumuiya ya Watumia maji wa bonde la Mto Songwe




KATIKA hali isiyo ya kawaida serikali ya Kijiji cha Idiwili kilichopo kata ya Iyula wilayani Mbozi mkoani Mbeya imegomea mpango wa utunzaji wa mazingira unaoendeshwa na Bonde la Ziwa Nyasa kwa madai kuwa wamekuwa wakiendesha kilimo katika vyanzo vya maji tangu enzi za mababu.
Hali hiyo imeibuka mwishoni mwa wiki wakati wa uzinduzi wa Jumuiya ya Watumia Maji wa Bonde la Mto Songwe,(JUWABOSO) uliofanyika katika kijiji cha Nyimbili kata ya Iyula wilayani Mbozi.
Awali ilielezwa kuwa mara baada ya wataalamu wa utunzaji wa mazingira na wahifadhi wa bonde la mtu Songwe kutembelea katika kijiji cha Idiwili kwa nia ya kuwahamasisha wakazi wa maeneo hayo juu kuacha kulima katika vyanzo vya maji walisema kuwa hawako tayari kuacha kilimo kwa kuwa kinawanufaisha.
‘’Sisi tulifika pale kuwahamasisha uhifadhi wa mito na utunzaji wa mazingira, wenzetu wakiongozwa na Mwenyekiti wa kijiji cha Idiwili waligoma kabisa katika utunzaji wa vyanzo vya maji,’’alisema Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Bonde la Ziwa Nyasa Bi.Mishi Salim Kombo.
Bi. Kombo alisema kuwa kijiji cha Idiwili kina vyanzo vingi vya maji ambayo yanapita katika mto Songwe kuelekea Ziwa Nyasa na kwamba wananchi wake wanaharibu vyanzo kwa kuchimba madini ndani ya mto hali ambayo inasababisha mto kuhamahama mara kwa mara.
Kwa upande wake Ofisa wa Maji wa Bonde la Ziwa Nyasa Witgal Nkondola alisema kuwa  changamoto walizokutana nazo waratibu wa Bonde la Ziwa Nyasa ambao mto Songwe unaingiza maji katika Ziwa hilo, serikali ya kijiji cha Idiwili imekuwa kikwazo cha harakati za utunzaji wa mazingira na uhifadhi wa vyanzo vya maji.
Alisema kuwa wamekuwa katika harakati za kuhamasisha wananchi wa vijiji mbalimbali kutunza mazingira ikiwa ni pamoja na kutolima katika vyanzo vya maji ambapo Mwenyekiti wa kijiji cha Idiwili amekuwa kikwazo hivyo wamechukua hatua za kutoa taarifa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri na mkuu wa wilaya kwa ufuaatiliaji.
Akizungumza katika mkutano huo mkuu wa Wilaya ya Mbozi Dkt.Michael Kadeghe alisema kuwa serikali ya wilaya ya Mbozi itafuatilia suala hilo kwa kumuita Mwenyekiti wa kijiji na Ofisa mtendaji wake ili kupewa elimu juu ya matumizi na uhifadhi wa vyanzo vya maji.

Post a Comment

Post a Comment