ZAIDI ya sh.
milioni 300 fedha zinazotokana na mradi wa vibanda 120 vya chama Cha Mapinduzi (CCM)
Kata ya Tunduma wilayani Momba mkoani Mbeya zinadaiwa kutafunwa na kuingizwa
katika akaunti za watu binafsi.
Taarifa za
ndani ya chama hicho zinadai kuwa vibanda hivyo ni kati ya miradi mikubwa ya
chama katika kata hiyo ambapo uanzishwaji wake ulilenga kukiongezea kipato
chama ili kukabiliana na wimbi la upinzani lililoshamiri katika jimbo la Mbozi
Magharibi.
Vibanda
hivyo ambavyo viko jirani kabisa na kituo cha Polisi cha Tunduma karibu na
mpaka wa Tunduma na nchi jirani ya Zambia vinadaiwa kulenga kukipatia chama hicho mamilioni ya fedha ambapo hata
hivyo fedha zilizotokana na uzabuni wa vibanda hivyo zinadaiwa kutafunwa na
watu wachache.
Utata
uliogubikwa kuhusu fedha za uzabuni wa vibanda hivyo umeelezwa kuwa umetokana
na viongozi wa chama hicho ngazi ya kata kuwatoza wafanyabiashara waliohitaji
vibanda hivyo kiasi cha sh. 100,000 kwa kila mmoja ambapo hata hivyo fedha
zilizotokana na zabuni hiyo zinadaiwa kuingizwa katika akaunti za watu binafsi.
Kwa mujibu
wa vyanzo vya habari hii ni kwamba jumla ya wafanyabiashara 120 walijitokeza
kuomba vibanda hivyo na kulipia kiasi cha sh. 100, 000 kwa kila mmoja na hivyo
kuingiza kiasi cha sh. milioni 12 ambazo hazijulikani matumizi yake hadi sasa.
Aidha mara
baada ya wafanyabiashara 120 kukubaliwa uzabuni wao kila mmoja alitakiwa kutoa
kiasi cha sh. milioni 3 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vibanda hivyo ambapo
zilikusanywa kiasi cha sh. milioni 360 zilizopaswa kuingizwa katika akaunti ya chama.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia hali ya vibanda
hivyo vilivyoanza Mwezi Machi 2012 ambao ulitarajiwa kumalizika mwezi Juni mwaka
huu ambapo hata hivyo hadi sasa vibanda hivyo kwa sasa vinatumiwa kama hifadhi ya
wavuta bangi na sehemu ya kujisaidia haja kubwa na ndogo kwa wapita njia.
Gazeti hili
lilishuhudia vyumba hivyo vikiwa vimetapakaa vinyesi na vipisi vya sigara ambapo
ujenzi huo ambao umegharimu kiasi kikubwa cha fedha hauna gharama za
ujenzi(BOQ), Ramani wala mkataba wa ujenzi hali ambayo inazidi kuongeza maswali
juu ya matumizi halali ya fedha za mradi huo.
Kadhalika
uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa katika harakati zote za ujenzi hakukuwa
na uthibitisho wowote wa risiti ambazo zingepaswa kuwasilishwa katika vikao vya mapato na
matumizi ya chama ilhali fedha zilizopatikana kwa ajili ya gharama za ujenzi
ziliingizwa katika akaunti za watu binafsi.
Akaunti
zilizokuwa zikitumiwa kuingiza fedha hizo ni pamoja na akaunti yenye namba
615250658 ya NMB tawi la Tunduma ambayo Mei 5, 2012 ziliingizwa kiasi cha sh. milioni
20 na akaunti nyingine yenye namba 615500155 ambayo ilitumika kuingizwa fedha
kiasi cha sh. milioni 30 kati ya Mei 11 hadi Mei 16.
Kulingana na
taarifa za ndani ya chama hicho zinadai kuwa akaunti hizo ni za watu binafsi na
kwamba fedha hizo kiasi cha milioni 50 hazijulikani matumizi haye hadi sasa.
Kwa upande
wake Mwenyekiti wa CCM kata ya Tunduma Bw. Daniel Mwashiuya alisema kuwa fedha
zilizokuwa zikikusanywa kwa ajili ya ujenzi hazikuingizwa katika akaunti ya
chama bali zilikuwa zikipitiliza kwa mkandarasi kwa ajili ya kuendelea na
ujenzi wa vibanda hivyo.
Naye Katibu wa
CCM Kata ya Tunduma Bw. Hemed Steven alisema kuwa mradi huo wa vibanda 120
ulitarajiwa kugharimu kiasi cha sh. milioni 270 ambapo kila mpangaji alilipia
sh. milioni 3 fedha ambazo amelipwa mkandarasi kampuni ya Wazawa Company Group.
Hata hivyo kauli ya Katibu wa chama Bw. Steven inapingana na makusanyo halisi ya
fedha za wapangaji na kwamba kiasi hicho cha fedha sh. milioni 270 alizotaja
kumlipa mkandarasi hakilingani na fedha
halisi za malipo ya wapangaji 120 ya jumla ya sh. milioni 3 kwa kila mmoja ambazo
ni sawa na sh. milioni 360 ambazo ni pungufu kwa sh. milioni 90.
Baadhi ya Vibanda amb avyo ni sehemu ya mradi wa CCM kata ya Tunduma ambao fedha zake zinadaiwa kutafunwa |
Post a Comment
Post a Comment