Diwani wa Kata ya Nkangamo Weston Simwelu wa (kwanza kulia) ambaye watoto wake wameuawa kikatili kwa kuchinjwa na kunyongwa jana. |
Na Ripota Wetu Tunduma.
WATOTO
wawili wa Diwani wa Kata ya Nkangamo wilayani Momba mkoani Mbeya Weston Simwelu(55)
wameuawa kikatili na watu wasiofahamika kwa kuchinjwa na kunyongwa baada ya
kuvamiwa majira ya saa 8:00 mchana Disemba 19 nyumbani kwao eneo la Tazara
katika mji mdogo wa Tunduma uliopo mpakani mwa Tanzania na Zambia.
Mauaji hayo
ya kutisha yameteka hisia za wakazi wa eneo hilo kwa madai kuwa huenda
yanahusishwa na imani za nguvu za giza huku baadhi wakidai kuwa yametokana na
mgogoro wa kifamilia.
Taarifa
za awali katika eneo la tukio zimedai kuwa Diwani huyo alikuwa akiishi na mke
mdogo aliyefahamika kwa jina la Tumaini Yohana(29) ambaye ni mfanyakazi katika
halmashauri ya mji mdogo wa Tunduma ambaye wakati wa tukio hilo alikuwa kazini.
Imeelezwa
kuwa chanzo cha mauaji hayo kinadaiwa ni kitendo cha Diwani huyo kuwa mbali na
mke mkubwa kwa muda mrefu huku ikidaiwa kuwa mke mkubwa amenyimwa mali za
mumewe yakiwemo mashamba na nyumba.
Jeshi la
Polisi kupitia Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya Barakael Masaki amethibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kuwataja marehemu kuwa ni Kalibu Simwelu(6) ambaye
aliuawa kwa kuchinjwa shingoni kwa kutumia kisu na watu wasiofahamika ambapo
mtu mwingine aliyeuawa ni mfanyakazi wa ndani aliyetambulika kwa jina la Sista
Nyilenda(17).
Kamanda
Masaki alisema kuwa Mfanyakazi wa ndani aliuawa kwa kunyongwa kwa kutumia waya wa televisheni iliyokuwepo
sebuleni ambapo wauaji wanadaiwa kuwavamia na kuwaua kinyama ambapo miili ya
marehemu ilikutwa sebuleni.
Alisema
kuwa wakati wa tukio hilo baba wa watoto hao Bw. Simwelu alikuwa shambani
katika kijiji cha Kipaka wilayani humo ilhali mama wa mtoto Tumaini alikuwa
kazini kwake ofisi ya Halmashauri ya Mji mdogo wa Tunduma.
Aidha
katika tukio hilo Kamanda Masaki alisema kuwa mbali na kufanya mauaji hayo,
wauaji waliiba mabegi makubwa mawili yenye nguo mbalimbali ambayo yalikuwa
katika chumba wanacholala watoto.
Kamanda
Masaki alisema kuwa kufuatia mauaji hayo watuhumiwa watano wametiwa mbaroni
ambao ni Gabriel Simwelu(19)Enock Simwelu(23) na Alex Simwelu(16) ambaye ni
mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya Sekondari Mpakani ambao wote ni
watoto wa mke mkubwa wa Bw. Simwelu.
Wengine
waliokamatwa ni pamoja na Mussa Ngoba(19) mkazi wa mtaa wa Mwaka na Patrick
Msigwa(18) mkazi wa mtaa wa Majengo na kwamba miili ya marehemu imehifadhiwa
katika kituo cha Afya Tunduma.
Post a Comment
Post a Comment