Kaimu Mkurugenzi wa Mashindano TFF Idd Mshangama akiwa na baadhi ya viongozi chama cha Mpira wa miguu Mbeya MREFA wakati wa ukaguzi wa uwanja huo leo mchana |
Katibu wa CCM mkoa wa Mbeya Maganga Sengelema katikati akizungumza na Kaimu Mkurugenzi wa Mshindao TFF Idd Mshangama alipotembelea ofisi za CCM leo jioni. |
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Miguu mkoa wa Mbeya Omar Mahinya Mkwawa akimpa maelekezo Kaimu Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF juu ya maendeleo ya ukarabati wa uwanja wa Sokoine leo mchana |
Mjumbe wa Kamati ya Ufundi wa chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Mbeya MREFA Elizabeth Kalinga akimpa maelekezo Kaimu Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF Idd Mshangama alipotembelea uwanja huo leo. |
Dimba la Sokoine linavyoonekana kwa sasa |
Katibu wa CCM mkoa wa Mbeya Maganga Sengelema akizungumza ofisini kwake leo mchana |
WAKATI uwanja wa
Kumbukumbu ya Sokoine uliofungiwa kwa kutokidhi viwango vya mchezo wa
Ligi Kuu ukiwa ukingoni kukamilika, Wamiliki wa Uwanja huo Chama Cha
Mapinduzi (CCM) wamesema kuwa kuanzia sasa marufuku uwanja huo kutumika
kwa matamasha ya FIESTA na yale ya Nyimbo za Injili kwa madai kuwa
yamekuwa yakichangia kuharibika kwa uwanja huo.
Akizungumza
ofisini kwake leo jioni mbele ya Kaimu Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF,
Idd Mshangama aliyezuru ofisi za CCM,Katibu wa CCM mkoa wa Mbeya
Maganga Sengelema amesema kuwa wamegundua kuwa matamasha hayo
yuanachangia kuharibika kwa uwanja huo na kusababisha gharama kubwa
katika ukarabati.
''Tulijikita
sana katika mapato yanayotokana na maonesho ya Fiesta na Matamasha ya
Injili, tunasema kuanzia sasa hakuna FIESTA wala matamasha ya dini ndani
ya uwanja huo, jambo lililopita limetufundisha mengi,''anasema Katibu
huyo wa CCM mkoa wa Mbeya.
Aidha
anasema kuwa hata hivyo TFF haikuwashirikisha kuanzia mwanzo wakati
wanatangaza kufungiwa kwa uwanja huo na kwamba taarifa za kufungiwa kwa
uwanja huo wamezipata kupitia vyombo vya habari na wao TFF hawajawahi
kukiandikia barua CCM ambao ndio wamiliki wa uwanja huo.
Hata
hivyo anasema kuwa pamoja na mapungufu yote yaliyotokea anawashukuru
TFF na chama cha Mpira wa miguu mkoa wa Mbeya MREFA ambao wamehamasisha
wadau kujitokeza kuchangia ukarabati wa uwanja huo hadi ulipofikia.
Kadhalika
Katibu huyo wa CCM Mkoa alikilaumu chama cha Mpira wa miguu nchini TFF
kwa kukubali kuutumia uwanja huo kwa mechi za mzunguko wa kwanza na
kutaka kutangaza kuufungia kwa mzunguko wa pili jambo ambalo anasema
kuwa limewachanganya wanamichezo na wapenzi wa soka mkoa wa Mbeya.
''Ligi
imechezwa katika uwanja huo mzunguko wa kwanza baadaye mnatutangazia
katika vyombo vya habari kwamba uwanja unafungiwa, mchakato huu ulipaswa
kuanza wakati wa mzunguko wa kwanza kabla ligi haijaanza,''anasema.
Sengelema anaendelea kubainisha kuwa wao kama chama wasingekubali uwanja ufungiwe ingawa mapato yanayotokana na mechi za ligi hazisaidii chochote katika matengenezo ya uwanja huo na kwamba uwanja si vyanzo pekee vya mapato ya chama.
''Hatuwezi kutoa mapato ya vyanzo vingine ya Chama tukaingiza katika uwanja, uwanja una mapato yake na vibanda vinavyozunguka uwanja navyo vina mapato yake, hatuwezi kuukarabati uwanja kwa vyanzo vingine vya mapato''anasema.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF Idd Mshangama anasema kuwa wao kabla ya kuanza kwa michezo ya ligi kuu viwanja vyote vilikaguliwa na kuwa wakati michezo ya ligi inaendelea zikaonekana dosari ambazo walikubaliana kuzifanyia marekebisho wakati wa mapumziko ya miezi mitatu.
''Lengo letu ni kuboresha viwanja viwe katika viwango angalau vinavyokidhi viwango vya Kimataifa, mapungufu yaliyotokea ndani ya utendaji wa TFF yataendelea kurekebishwa,''anasema Mshangama.
Anasema kuwa ziara yake ni kwa ajili ya ukaguzi wa viwanja vitano vinavyochezea ligi katika mikoa ya Mbeya,Ruvuma na Iringa na kuwa alitembelea kiwanja cha Mbozi ambako inachezwa ligi daraja la Kwanza, uwanja wa Sokoine ambao ulifungiwa kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho,Uwanja wa Majimaji Songea, Uwanja wa Mbinga, Viwanja vya Samora na Mufindi vya Iringa.
Alisema kuwa TFF sio wamiliki wa viwanja hivyo lakini hata hivyo wanatoa ushauri wa kiufundi na maelekezo na wenye viwanja wanapaswa kukubali kushaurika ili kuviweka kuwa katika hadhi inayokidhi viwango vya soka.
Post a Comment
Post a Comment