MAPATO
kwa mechi ya ligi ya Vodacom kati ya timu za Mbeya City ya Jijini Mbeya
na Simba ya Jijini Dar es salaam yamevunja rekodi ya michezo yote
iliyowahi kuchezwa nje ya Jiji la Dar es salaam kwa kuingiza kiasi cha
sh. milioni 105.
Mechi
iliyowahi kuingiza kiasi kikubwa cha mapato katika uwanja huo ni ile
iliyochezwa kati ya Timu ya Mbeya City na Yanga ya Dar es salaam katika
uwanja huo mwaka jana na kuingiza kiasi cha sh. milioni 100.
Katika
mechi hiyo ya jana ambayo timu hizo zilitoka sare ya goli
1-1,jumla ya tiketi 21,000 ziliuzwa ambapo tiketi moja iliuzwa kwa
sh.5,000 hata hivyo tiketi hizo ziliisha mapema na kusababisha baadhi ya
mashabiki waliohitaji kushuhudia mchezo huo kubaki nje ya uwanja.
Mbali
na mashabiki waliokosa tiketi kushindwa kuingia uwanjani, mwandishi wa
habari hizio alishuhudia umati wa mashabiki ambao walikuwa na tiketi
mkononi kuendelea kubaki nje hadi kipindi cha kwanza kinamalizika
kutokana na msururu mrefu wa kuingia uwanjani.
Wapenzi wa soka
walianza kukata tiketi majira ya saa 2:00 asubuhi na kuanza kuingia
uwanjani saa 4:30 ambapo hata hivyo msururu mrefu wa wapenzi
waliohitaji kuiona mechi hiyo ilisababisha kushindwa kuingia uwanjani
kwa wakati.
Katika
hatua nyingine baadhi ya watu walipata fursa ya kujiongezea kipato kwa
kununua vitabu vya tiketi za mechi hiyo na baadaye kuziuza kwa bei ya
sh.8,000 hadi sh.10,000 badala ya bei ya kawaida iliyopangwa na TFF ya
sh. 5,000 kwa kila tiketi.
Mbali
na tiketi hizo kuuzwa kwa bei ya juu bado kuna baadhi ya tiketi
zilionekana kutokidhi viwango ambapo mwandishi wa habari hizi
alishuhudia mmoja wa wasemaji wa timu ya Mbeya City Freddy Jackson akiwa
na tiketi zisizopigwa mhuri na kusema kuwa tiketi hizo zimeghushiwa kwa
nia ya kuhujumu mapato ya mchezo huo.
Akizungumza
mapato ya mchezo huo Mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Miguu mkoa wa
Mbeya Elias Mwanjala alisema kuwa jumla ya tiketi 21,000 ziliuzwa na
kumalizika na kuingiza mapato jumla ya sh. milioni 105.
Katika
mapato hayo kila timu ilipata kitita cha sh. milioni 25.3 ambapo
sh.milioni 12.8 zilibaki kwa ajili ya uwanja,sh.milioni 7.7 kwa ajili ya
maandalizi na sh. milioni 7.7 kwa
ajili ya kamati ya ligi ilhali sh. milioni 3.8 zilikuwa ni kwa ajili ya
chama cha mpira wa miguu TFF.
Post a Comment
Post a Comment