Ads (728x90)



Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Mbeya Leonard Magacha(katikati) akiwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TFDA(kulia) wakati wa semina ya siku moja kwa wanahabari 120 wa mikoa 6 ya Nyanda za Juu Kusini leo asubuhi.

Baadhi ya waandishi wa habari kutoka mikoa 6 ya Nyanda za Juu Kusini wakiwa katika semina ya siku moja ya TFDA







Meneja wa Mamlaka ya Chakula na Dawa TFDA kanda Rodney Alananga akifafanua jambo wakati wa semina iliyowahusisha wanahabari 120 kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.


Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) imetakiwa kuwa na dhana shirikishi na nchi jirani kusaidia kutozagaa kwa bidhaa na vipodozi hatari kwa afya ya binadamu.
Akizungumza katika semina ya siku moja iliyowahusisha wahariri na waandishi wa habari wapatao 120 kutoka mikoa sita ya Nyanda za Juu Kusini, Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Mbeya Leonard Magacha ambaye alimwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya alisema TFDA inapaswa kushirikiana na nchi majirani kupunguza ongezeko la bidhaa hatari.
Alisema jitihada za TFDA zitakuwa hazina maana iwapo nchi jirani za Zambia, Malawi na kwingineko bado zinazalisha na kuuza bidhaa ambazo kwao si hatari kwa matumizi ya binadamu hivyo ni vyema mamlaka ikajenga uhusiano na nchi hizo ili kuondoa tatizo hilo ambalo limekuwa na athari kubwa kwa Watanzania.
''TFDA fanyeni mkakati wa ushirikiano na nchi jirani za Malawi, Zambia na kwingineko, huko bidhaa hizi si haramu, mkikaa pamoja tatizo hili litapatiwa ufumbuzi,''alisema Magacha.
Aidha aliitaka Mamlaka hiyo inayosimamia Chakula na Dawa nchini kutofanya kazi kwa zimamoto bali pia zinapaswa kuwa karibu na mamlaka zingine za kijamii kwa ngazi za serikali za mitaa ili kusaidia kuzagaa kwa bidhaa haramu nchini.
Alisema maduka mengi nchini kumezagaa bidhaa zisizosajiliwa na kwamba bila kuwepo kwa mkakati madhubuti suala hilo litakuwa gumu na hivyo kuendelea kuiathiri jamii.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TFDA Charys Ugullum alisema kuwa kumekuwepo na changamoto nyingi za utendaji baina ya mamlaka na jamii hivyo kwa kuwahusisha wadau mbalimbali katika maeneo ya kijamii itasaidia kupunguza tatizo la kuzagaa kwa bidhaa ambazo ni hatari kwa matumizi ya binadamu.
Alisema Mamlaka imeamua kutoa mafunzo kwa wahariri na waandishi wa habari kwa nia ya kusogeza taarifa za utendaji kwa jamii kutokana na vyombo vya habari kuwa na uwezo wa kufikisha taarifa kwa jamii kwa haraka.

Post a Comment

Post a Comment